Masomo ya sayansi yawatoa jasho watahiniwa wa darasa la saba 2026
- Somo la hisabati limeonesha kuimarika kwa asilimia 62.56.
Dar es Salaam. Serikali na wadau wa sekta ya elimu huenda wakahitaji kuongeza juhudi za kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya sayansi, baada ya ufaulu wa masomo hayo katika matokeo ya Darasa la Saba ya mwaka 2026 kushuka.
Kwa mujibu wa matokeo ya mitihani hiyo, yaliyotangazwa leo Novemba 3, 2026 jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Prof. Said Ally Mohamed ufaulu wa somo la Sayansi na Teknolojia umeshuka kwa asilimia 4.09 ukilinganisha na mwaka 2025.
“Ufaulu wa somo la Sayansi na Teknolojia mwaka 2026 ni asilimia 80.34 ukiwa umeshuka kwa asilimia 4.09 ikilinganishwa na mwaka 2025. Katika somo hili, Wasichana waliofaulu ni asilimia 76.25 na Wavulana waliofaulu ni asilimia 85.31,” amesema Prof Mohamed.
Kwa upande wa ubora wa ufaulu unaopimwa kwa wanafunzi kupata dara A na B, Prof Mohamed amesema pia umeshuka kutoka asilimia 48.14 mwaka 2025 hadi asilimia 33.60 mwaka 2026, sawa na upungufu wa asilimia 14.54.
Licha ya ufaulu kushuka, Prof Mohamed amesema kiwango cha jumla cha ufaulu katika somo hilo bado ni kizuri kwa kuzingatia mfumo wa upangaji madaraja wa mtihani huo.
“Bado somo lina ufaulu wa asilimia 80, asilimia 80 katika ‘grading system’ ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi bado ni kiwango cha A kwa hiyo umeshuka lakini bado upo katika kiwango kizuri,” ameongeza Prof. Mohamed.
Ufaulu masomo mengine yapaa
Wakati masomo ya sayansi yakiwatoa jasho watahiniwa wa darasa la saba, hali n tofauti katika masomo mengine hususan Kiswahili na Uraia na Maadili ambayo yamepata viwango vya juu vya ufaulu mwaka 2026.
Kwa mfano, Kiswahili limeongoza kwa ufaulu wa asilimia 93.13, likiwa na ongezeko la asilimia 5.56 ikilinganishwa na mwaka 2025.
Aidha, ubora wa ufaulu katika somo hili umeongezeka kutoka asilimia 59.65 hadi asilimia 73.81 kwa watahiniwa waliopata madaraja A na B.
Upande wa masomo ya Sayansi Jamii, Uraia na Maadili imeendelea kuwa na ufaulu wa juu wa asilimia 90.12, huku Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi ikifikia asilimia 76.53.
Hata hivyo, kuna tofauti katika ubora wa ufaulu, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi imeimarika kutoka asilimia 27.87 hadi asilimia 36.53, wakati Uraia na Maadili imeshuka kutoka asilimia 56.68 hadi asilimia 54.
Kwa upande mwingine, somo la Hisabati limeonesha kuimarika, ambapo ufaulu wa jumla umeongezeka kutoka asilimia 56.66 mwaka 2025 hadi asilimia 62.56 mwaka 2026, sawa na ongezeko la asilimia 5.90.
Aidha, ubora wa ufaulu katika somo hilo, unaopimwa kwa watahiniwa waliopata madaraja A na B, umeongezeka kutoka asilimia 21.92 mwaka 2025 hadi asilimia 32.47 mwaka 2026, sawa na ongezeko la asilimia 10.55.