Matokeo darasa saba 2021 haya hapa
- Watahiniwa 907,820 kati ya 1,107,460 waliofanya mtihani huo wamefaulu sawa na asilimia 81.97.
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2021 huku ufaulu wa jumla ukiongezeka kwa asilimia 6.6 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka jana.
Watahiniwa 907,820 kati ya 1,107,460 waliofanya mtihani huo wamefaulu sawa na asilimia 81.97 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 74,130 ikilinganishwa na mwaka jana.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde akitangaza matokeo hayo leo Jijini Dar es Salaam amesema kati ya watahiniwa waliofaulu, wasichana ni 467,967 ambao ni sawa na asilimia 81.43 na wavulana ni 439,835.
“Watahiniwa hawa. wamepata alama 121 au zaidi kati ya alama 300. Idadi hii ya watahiniwa waliofaulu ni sawa na asilimia 81.97,” amesema Dk Msonde.
Watahiniwa 1,132,084 wa shule za msingi walisajiliwa kufanya mtihani huo wakiwemo wasichana 584,614 sawa na asilimia 51.64 ya watahiniwa wote. Kati ya watahiniwa waliosajiliwa, watahiniwa wenye mahitaji maalum walikuwa 3,238.
“Watahiniwa 1,108,023 sawa na asilimia 97.87 ya waliosajiliwa walifanya mtihani. Kati yao wasichana walikuwa 574,998 sawa na asilimia 98.36 na wavulana walikuwa 533,025 sawa na asilimia 97.36,” amesema Dk Msonde wakati akitangaza matokeo hayo.
Watahiniwa 24,061 sawa na asilimia 2.13 hawakufanya mtihani huo uliofanyika Septemba 8 na 9 mwaka huu nchi nzima kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo utoro na ugonjwa.
Ufaulu Kimasomo
Takwimu za matokeo ya Necta zinaonyesha kuwa ufaulu katika masomo yote upo juu ya wastani isipokuwa ufaulu wa somo English Language, lenye ufaulu wa asilimia 48.02.
Watahiniwa wamefaulu zaidi katika somo la Kiswahili ambapo ufaulu ni asilimia 88.50.
Latest
