Zaidi ya Sh2 bilioni zitakavyotumika kupambana na ukatili wa kijinsia Tanzania

May 31, 2022 5:15 am · David
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali kutumia Sh2.6 bilioni mwaka ujao kutokomeza vitendo hivyo.
  • Fedha hizo zitasaidia kutoa elimu na kuwawezesha wanawake kiuchumi. 
  • Baadhi ya wabunge walalamika kuwa vitendo vya ukatili bado vinaendelea nchini

Dar es salaam. Serikali ya Tanzania imepanga kutumia Sh2.65 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2022/23 kwa ajili ya kupambana na ukatili wa kijinsia ili kujenga jamii yenye usawa inayozingatia haki za watu wote.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dk Dorothy Gwajima amesema hayo jijini Dodoma leo (Mei, 30, 2022) wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 ya wizara hiyo.

Waziri Gwajima amesema miongoni mwa vipaumbele vya wizara yake katika mwaka wa fedha 2022/23 ni katika kupambana na vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa vikiwaathiri zaidi wanawake na watoto.

Waziri Gwajima ameogeza kuwa vitendo vya ukatili bado vimeendelea kushamiri nchini hivyo jukumu lao kama Serikali ni kuweza kupambana na vitendo hivyo ili watu waweze kuwa salama.

Mbinu zitakazotumika

Waziri Gwajima amesema kuwa katika kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto watatumia mbinu kama kampeni, mafunzo wezeshi kwa watoa huduma za madawati ya jinsia vyuoni na taasisi pamoja na kusambaza mwongozo na uwezeshaji wa majukwaa ya wanawake kiuchumi.

“Katika kupambana na ukatili na usawa wa kijinsia Sh2.65 bilioni tumetenga kuwezesha hafua za kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto,” amesema Waziri Gwajima.

Kiasi hicho cha fedha ni sehemu ya Sh43.4 bilioni ambazo wizara hiyo mpya iliyogawanywa kutoka Wizara ya Afya inapanga kutumia mwaka ujao unaoanza Julai 1, 2022. 


Zinazohusiana: 


Ukatili wa kijinsia hasa vipigo na kiuchumi umekuwa ukikatisha ndoto za wasichana na wanawake wengi nchini katika kuboresha maisha yao na kutoa mchango wao katika maendeleo ya nchini.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wamelalamikia kuendelea kushamiri kwa vitendo vya ukatili na kuiomba Serikali kuangalia namna bora ya kudhibiti matukio hayo kwani sheria iliyopo inampa dhamana mtuhumiwa na hivyo kusababisha baadhi kutoroka.

“Sheria hii ya watu wanaofanya ukatili hasa kwenye suala zima la wanaobaka, wanaolawiti, wanaofanya vitendo vyovyote vile vya unyanyasaji wa kingono, sheria inampa dhamana muhusika, wakishapewa dhamana wanatoroka……kama inawezekana sheria iletwe hapa bungeni iweze kurekebishwa kwasababu kama mtu anahujumu uchumi anakuwa hana dhamana, je anayehujumu uhai wa mtu inakuwaje… hili halikubaliki.” amesema Mbunge wa Viti Maalum Dk Christina Mnzava.

Mjumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo, Salma Kikwete akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo bungeni jijini Dodoma. Picha| Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.

Kamati yaipa tano Serikali

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imesema kuanzisha wizara hiyo ambayo itaweza kushughulikia kwa upana masuala ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalumu ni hatua nzuri kuimarisha usawa wa kijinsia Tanzania.

Aidha, imeishauri Serikali kutoa fedha ambazo zimeidhinishwa katika bajeti kwa wakati na kiasi ambacho kiliombwa ili wizara hiyo iweze kutatua changamoto mbalimbali za kijamii. 

“Kamati inapenda kuipongeza Serikali kwa kuunda wizara hii na kuifanya ijitegemee kutoka Wizara ya Afya. Ni vyema sasa wizara hii kutengewa fedha za maendeleo za kutosha katika taasisi zake ili kutatua changamoto mbalimbali na kuwaletea wananchi maendeleo.” amesema Salma Kikwete, mjumbe wa kamati hiyo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW