Ukatili wa dhidi ya watoto washuka, Serikali yaanika mikakati
- Umepungu kwa asilimia 9.5 ndani ya mwaka mmoja.
- Ukatili mwingine waongezeka hadi kufikia matukio 388 mwaka 2025.
Dar es Salaam. Licha ya jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuimarisha ustawi na ulinzi wa watoto, vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vimeendelea kuongezeka suala linalotishia ustawi wa kundi hilo nchini.
Vitendo hivyo vya ukatili vinahusisha matukio ya ubakaji, ulawiti, shambulio la aibu, kuzini na maharimu, kumpa mwanafunzi mimba, kutupa mtoto, kutelekeza mtoto, na wizi wa watoto.
Kwa mujibu wa Dk Dorothy Gwajima, Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, matukio 10,290 ya ukatili dhidi ya watoto yaliripotiwa mwaka 2025.
Dk Gwajima aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2026/27 bungeni Dodoma leo Juni Mosi, 2026 amesema takwimu hizo zinaonesha ukubwa wa tatizo la ukatili dhidi ya watoto nchini Tanzania.
“Takwimu hizi zinaonesha ukubwa wa changamoto ya ukatili dhidi ya watoto katika jamii yetu na zinatoa wito kwa Taifa kuendelea kuchukua hatua madhubuti zaidi za kulinda kizazi cha sasa na kijacho, Wizara itaendelea kwa kasi zaidi kuratibu wadau wake ili kuhakikisha ukatili wa kingono dhidi ya watoto unatokomezwa,” amesema Dk Gwajima.
Ukatili wa kingono ambapo 6,500 walibakwa, 1,549 walilawitiwa, 1,105 walipewa mimba wakiwa shuleni, 712 walifanyiwa shambulio la aibu na 36 walizini na maharimu.
Matukio hayo ya ukatili wa kingono yamepungua kwa asilima 8.67 kutoka watoto 11,267 walioripotiwa mwaka 2024.
Mbali na ukatili wa kingono, watoto 388 waliripotiwa kufanyiwa aina nyingine za ukatili mwaka 2025, ambapo 165 walitupwa, 137 walitelekezwa na 86 waliibwa.
Siku za hivi karibuni, suala la ukatili dhidi ya watoto limeendelea kupewa kipaumbele na viongozi wa Serikali pamoja na wadau wa haki za binadamu, kufuatia kuongezeka kwa matukio hayo huku wakitaka hatua za haraka dhidi ya wahusika kuchukuliwa.
Wizara yaweka mikakati kuimarisha ulinzi
Ili kukabiliana na matukio hayo ya ukatili Dk Gwajima amesema, wizara itaendelea kwa kasi zaidi kuratibu wadau wake ili kuhakikisha ukatili wa kingono dhidi ya watoto unatokomezwa ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya kutatua changamoto hii.
Vilevile, wizara kwa kuunganisha nguvu na wadau wake itaendelea kuelimisha jamii kuimarisha ulinzi wa watoto, kutoa malezi mbadala na kwa wale wenye uhitaji wa watoto badala ya kuwaiba wafahamu kuhusu uwepo wa huduma rasmi ya kisheria ya kuasili watoto.
Tofauti na mwelekeo huu, Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote wanaojihusisha na vitendo vya ukatili na kuhujumu haki za watoto.