Wizara ya Uwekezaji na Viwanda yawasilisha bajeti, yaomba Sh 119 bilioni

May 4, 2023 11:29 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Uchambuzi wabainisha upatikanaji wa fedha katika Wizara hiyo hauridhishi.
  • Yatajwa kama sababu ya kukwamisha miradi ya maendeleo.
  • Kamati yaitaka Serikali kuongeza na kutoa fedha za miradi ya maendeleo ili kuongeza mchango wa sekta ya biashara kwenye pato la Taifa.

Dar es Salaam. Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imewasilisha bajeti yake kwa mwaka wa Fedha 2023/24 na kuomba Bunge kuwaidhinishia Sh119 bilioni.

Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni leo Mei 5, Waziri wa wizara hiyo Dk Ashatu Kijaji amesema kati ya fedha hizo Sh75.5 bilioni  ni za matumizi ya kawaida.

“ Aidha, Sh43.5 zinaombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo Sh30.3 bilioni ni fedha za ndani na Sh13 bilioni ni fedha za nje,” amesema Kijaji bungeni jijini Dodoma.

Bajeti hiyo ikiwa itapitishwa na Bunge itakuwa imeongezeka kwa Sh20 bilioni ikilinganishwa na ya mwaka 2022/23 ambapo wizara hiyo iliomba na kuishinishiwa Sh99 bilioni.

Vipaumbele vya wizara hiyo kwa mwaka ujao ni kutekeleza miradi ya kielelezo, kufanya uwekezaji katika maeneo maalumu ya kiuchumi na kongani za viwanda.

Pia kuimarisha uwezo wa  uzalishaji viwandani, kuratibu majadiliano ya kibiashara baina ya nchi na nchi na kuimarisha huduma za biashara na masoko.


Soma zaidi


Mwenendo wa upatikanaji wa fedha hauridhishi

Hata hivyo, imebainika kuwa mwenendo wa upatikanaji wa fedha katika wizara hiyo si wa kuridhisha hii ni baada ya uchambuzi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kubaini kuwa mpaka Februali 23 mwaka huu wizara hiyo ilipokea asilimia 53.7 tu ya bajeti iliyoidhinishwa.

Kanuni zinaitaka Serikali kuwa imewasilisha kuanzia  asilimia 66.7 ya kiasi cha bajeti kilichoidhinishwa na bunge mpaka kufikia mwezi Februari kabla ya mwaka fedha kuisha.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mariam Ditopile aliyekuwa akisoma maoni ya kamati kuhusiana na utekelezaji wa bajeti na mapendekezo ya mapato na matumizi ya wizara hiyo amewaambia wabunge kuwa kutokana na kusuasua kwa upatikanaji wa fedha kumesababisha miradi ya maendeleo kutofanyika kwani ni asilimia 35.2 pekee ya fedha ya miradi ya maendeleo ndiyo zimepokelewa wizarani.

“Hadi kufikia Februari 2023, wizara ilipokea jumla ya Sh10.7 bilioni ya fedha za ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo sawa na asilimia 35.2 ya fedha zilizotengwa, hadi kamati inakamilisha uchambuzi hakukuwa na fedha za nje zilizowasilishwa wizarani kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” amesema Ditopile.

Ditopile amesisitiza kuwa upatikanaji wa fedha katika wizara hiyo hautoi mwelekeo mzuri wa ukamilishaji kwa miradi iliyopangwa hivyo kamati hiyo imeishauri Serikali kuongeza fedha kwenye wizara hiyo ili kuongeza mchango wa sekta ya biashara katika pato la taifa.

Licha ya bajeti ya wizara hiyo kuongezeka, Kamati hiyo imesema huenda utekelezaji wake ukawa mgumu kwa sababu ya kutokuwasilishwa kwa fedha kwa wakati na kutegemea fedha za nje. 

“Ni maoni ya kamati kuwa wizara hii iongezewe fedha za miradi ya maendeleo ya ndani ili iweze kutekeleza shughuli zake na kuhakikisha kuwa mchango wa sekta ya biashara kwenye pato la Taifa unaendelea kuimarika na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi na wananchi kwa ujumla,” amesisitiza Ditopile.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dk Ashatu Kijaji alipokuwa akisoma hotuba ya utekelezaji na mapendekezo ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/24 bungeni jijini Dodoma. Pichal Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW