M-pesa, intaneti vyachangia Vodacom Tanzania kupata faida ya Sh90 bilioni

Nuzulack Dausen 0459Hrs   Mei 14, 2019 Biashara

Vodacom inaongoza nchini kwa idadi ya wateja wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi kwa kuwa na asilimia 38.6 ya soko ikifuatiwa na kampuni za Tigo (Tigo Pesa) na Airtel (Airtel Money) kwa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za hadi Desemba 2018. Picha|Mtandao.


  • Mapato yatokanayo na huduma yapaa kwa asilimia 5.4 hadi Sh1 trilioni.
  • M-Pesa inachangia kiwango kikubwa cha mapato ya kampuni hiyo.
  • Mapato yanayotokana na huduma za simu za sauti bado mtihani.

Dar es Salaam. Kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania PLC imeeleza kuwa mapato yake yatokanayo na huduma yamepaa kwa asilimia 5.4 katika mwaka ulioishia Machi 31, 2019 hadi kufikia Sh1.018 trilioni yakichagizwa zaidi na ukuaji imara wa mapato kutoka katika huduma za M-Pesa, intaneti na ujumbe mfupi.

Ripoti ya awali ya kifedha kwa mwaka ulioishia Machi 2019 iliyotolewa na kampuni hiyo imebainisha kuwa mapato ya M-pesa yameongezeka kwa asilimia 14.5 wakati yale ya intaneti (data) yakipaa kwa asilimia 17.9.

Hata hivyo, mapato yatokanayo na huduma za simu kwa sauti yameshuka kwa asilimia 1.1 kutoka Sh392.3 bilioni mwaka 2018 hadi Sh388.2 bilioni katika mwaka ulioishia Machi 2019.

“Mapato ya M-Pesa yaliongezeka kwa asilimia 14.5 na kufikia Sh333.5 bilioni yakichagizwa zaidi na ukuaji wa wateja na matumizi ya bidhaa za huduma za kifedha kupitia simu za mkononi. 

"Ukuaji huu ulifanikiwa licha ya uwepo wa presha ya ushindani mkali na utekelezaji wa mfumo wa malipo wa Serikali (government electronic payment gateway) ambao umepunguza mapato ya ada kwa waendeshaji wa huduma za malipo ya umeme (Luku),” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni hiyo, Ali Mufuruki.


Soma zaidi:


M-pesa inachangia kwa kiwango kikubwa mapato ya kampuni hiyo ambapo kwa mwaka ulioishia Machi 31, 2019 ilichangia asilimia asilimia 32.7 au theluthi ya mapato yote.

Vodacom inaongoza nchini kwa idadi ya wateja wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi kwa kuwa na asilimia 38.6 ya soko ikifuatiwa na kampuni za Tigo (Tigo Pesa) na Airtel (Airtel Money) kwa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za hadi Desemba 2018.

“Huduma zetu za M-Pesa zimewawezesha wateja wapya 620,000 kufanya miamala ya kifedha kwa kutumia simu za mkononi. Huu ni ukuaji wenye afya kwa watumiaji wa huduma hii baada ya ongezeko la wateja kwa asilimia 9.7,” amesema Hisham Hendi, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania.

“Huduma yetu ya Lipa kwa M-Pesa inayowawezesha wateja kulipia huduma na bidhaa imerekodi ukuaji wa hali ya juu. Kwa sasa huduma hiyo ina wafanyabiashara 11,000 ambao walifanikisha miamala yenye thamani ya Sh1.1 trilioni ndani ya mwaka huu ikiwa ni ongezeko la asilimia 186,” ameongeza.

Vodacom imeeleza kuwa katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, ilifanikiwa kuongeza wateja wapya milioni 1.2 na kufanya idadi ya wateja wote kufikia milioni 14.1 ikiwa ni ukuaji wa asilimia 9.6.

Katika kipindi hicho, Vodacom Tanzania imetangaza kuwa imepata faida ya Sh90.2 bilioni na kwamba wawekezaji wa kampuni hiyo watapata mapato ya Sh40.3 kwa hisa moja kutoka Sh83.8 iliyorekodiwa mwaka 2018.

Related Post