Jafo aomba Sh135.7 bilioni kukuza viwanda, biashara Tanzania

May 14, 2025 3:36 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Uchambuzi wabainisha upatikanaji wa fedha katika Wizara hiyo hauridhishi.
  • Kamati yaitaka Serikali kuongeza fedha kila mwaka 

Dar es Salaam. Wizara ya Viwanda na Biashara imeiomba Serikali iidhinishe bajeti ya Sh135.79 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22.4 kutoka Sh110.9 bilioni zilizotengwa mwaka wa fedha 2024/25 ili kukuza viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa nchini.

Ongezeko hilo linachochewa zaidi na mahitaji ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na mikakati ya kuimarisha sekta ya viwanda na biashara nchini ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kuzalisha ajira, kukuza mauzo ya nje na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje.

Katika hotuba ya bajeti bungeni leo, Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Selemani Jafo leo Mei 14,2025 Bungeni jijini Dodoma amesema kuwa kati ya kiasi kinachoombwa Sh93.9 bilioni sawa na asilimia 69.1 au theluthi mbili ya bajeti yote ni kwa matumizi ya kawaida. 

Baadhi ya wageni waliohudhuria leo Bungeni jijini Dodoma. Picha/ Bunge la Tanzania.

Kati ya fedha hizo, Sh75.82 bilioni ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi, ambayo ni sawa na asilimia 55.8 ya bajeti yote huku Sh18.08 bilioni zikiwa ni kwa matumizi mengineyo sawa na asilimia 13.3.

Kwa upande wa miradi ya maendeleo, wizara imeomba Sh41.89 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 30.9 ya bajeti yote.

Kati ya fedha hizo zinasubiri baraka za Bunge, Sh27.87 bilioni sawa na asilimia 66.6 ya fedha hizo zinatarajiwa kutoka vyanzo vya ndani huku Sh14.02 bilioni zikiwa ni fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Vipaumbele lukuki, fedha kidogo

Katika mwaka 2025/26, Wizara ya Viwanda na Biashara imepanga kuendeleza miradi ya kimkakati kama kuwezesha uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda nchini, kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kielelezo na kimkakati ya sekta.

Vipaumbele vingine ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma kwa kuboresha mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya mitaa ya viwanda (Industrial Clusters) kwa ajili ya viwanda vidogo na vya kati pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea ukuaji wa Sekta binafsi.

Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu akiongoza kikao cha 24 cha mkutano wa 19 wa Bunge mbapo baada ya kipindi cha maswali na majibu Waziri wa Viwanda na Biashara, aliwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo mwaka wa fedha 2025/26. Picha/Bunge Tanzania.

Wizara hiyo pia itaendelea na utafutaji wa masoko kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, kuchochea maendeleo ya watu kwa kuboresha miradi na programu kwa jamii inayohusisha elimu na mafunzo ya ujuzi na kuimarisha usimamizi wa ubora na usalama wa bidhaa nchini zikiwemo bidhaa za chakula na vipodozi. 

Baadhi ya miradi ya kimkakati ambayo wizara imepanga kuitekeleza ni Magadi Soda Engaruka, Makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma cha Liganga.

Katika mwaka wa fedha 2024/25, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh110.9 bilioni, ambapo hadi kufikia Machi 2025 ilipokea na kutumia Sh75.75 bilioni kwa matumizi ya kawaida sawa na asilimia 68.3 ya bajeti hiyo. 

Kiwango hicho cha utekelezaji kimejumuisha robo tatu za mwaka wa fedha hivyo Serikali itakuwa na kibarua cha kuhakikisha theluthi moja ya bajeti na mipango yake iliyosalia inatekelezwa ndani ya miezi mitatu ya mwisho inayoishia Juni mwaka huu.

Kati ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya mwaka 2024/25, Sh52.8 bilioni zilitumika kwa mishahara, sawa na robo tatu ya bajeti nzima (asilimia 77.25) ya fedha za mishahara zilizotengwa huku Sh9.17 bilioni zikitumika kwa matumizi mengineyo.

Aidha, kwa upande wa miradi ya maendeleo, wizara ilipokea Sh13.78 bilioni pekee, sawa na asilimia 46.25 ya fedha zote zilizotengwa kwa ajili hiyo. 

Uwekezaji katika miradi ya maendeleo hupigiwa chapuo zaidi kwa kuwa huchochea maendeleo nchini badala ya matumizi ya kawaida ambayo yamekuwa yakikosolewa na vyama vya upinzani na baadhi ya wadau kuwa mengine hayana tija zikiwepo posho za vikao ambavyo vingeweza kufanyika kwa mtandao.

Kamati yahofia utekelezaji

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara,Kilimo na Mifugo imeeleza kutoridhishwa na mwenendo wa upatikanaji wa fedha hali inayoathiri utekelezaji wa miradi muhimu ya maendeleo pamoja na uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. 

Kwa mujibu wa uchambuzi wa kamati hiyo kupitia Makamu Mwenyekiti wake, Mariam Ditopile amefafanua kuwa, wizara iliomba kuidhinishiwa Sh81.1 bilioni kwa matumizi ya kawaida katika mwaka wa fedha 2024/25 kupitia kifungu cha 44. 

“Uchambuzi wa kamati umebaini kuwa makadirio ya bajeti yameongezeka kwa asilimia 22, ongezeko zaidi lipo kwenye fedha za maendeleo za nje ambazo mwaka jana hazikuwepo ongezeko hili litakuwa na tija kama fedha zitapatikana kwa wakati,” amefafanua Ditopile.

Hata hivyo, mpaka kufikia Machi 2025, upatikanaji wa fedha kutoka hazina umeonekana kuwa chini ya lengo kwa asilimia 4.56 hali inayochochea kuathiri utekelezaji wa baadhi ya majukumu ya wizara hiyo.

 “Kamati inashauri kuwa Serikali iendelee kuipatia wizara fedha iliyoidhinishwa na Bunge kwa wakati ili iweze kukamilisha upatikanaji wa maagizo iliyopewa kwa kuwa baadhi ya maagizo hayajatekelezwa kutokana na kukosekana kwa fedha,” amesema Ditopile.

Serikali, amesema, inapaswa kuongeza bajeti ya wizara hiyo kila mwaka huku wananchi wakishirikishwa katika utekelezaji wa miradi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW