Maumivu kwa wawekezaji wa kampuni ya bia soko la hisa Dar

Mwandishi Wetu 1222Hrs   Mei 24, 2019 Biashara

EABL ndiyo kampuni iliyofanya vibaya zaidi leo sokoni huku nyingi zikibaki katika viwango vilivyokuwepo jana zikiwemo Vodacom, benki ya CRDB, DCB na NMB. Picha|Mtandao.


  • Hisa za kampuni hiyo ya bia ya Afrika Mashariki (EABL) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) zimeshuka kwa asilimia 0.85. 
  • Wawekezaji wake wamepoteza Sh40 kwa kila hisa moja leo sokoni.
  • Kampuni ya habari ya NMG na Acacia wako kicheko tu.

Dar es Salaam. Wawekezaji wa kampuni ya Bia ya Afrika Mashariki (EABL) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) leo wamepoteza Sh40 kwa kila hisa ya moja baada ya thamani ya hisa za kampuni hiyo kushuka kwa asilimia 0.85 kutoka kiwango cha jana Mei 23, 2019.

Ripoti ya soko ya siku ya DSE ya Mei 24 inaonyesha kuwa hadi soko linafungwa thamani ya hisa moja ya EABL ilikuwa ni Sh4,640 kutoka Sh4,680 iliyorekodiwa jana. 

Licha ya thamani ya hisa za kampuni hiyo kushuka, haikufanikiwa kuuza hata hisa moja leo.

Wakati wawekezaji wa EABL wakiugulia maumivu leo, wenzao wa kampuni ya Kenya Airways(KA) watalala na kicheko baada ya thamani ya hisa za kampuni hiyo kupanda kwa asilimia 6.67 kutoka Sh75 kwa hisa moja iliyorekodiwa jana wakati soko linafungwa hadi Sh80 leo hii jioni. 

Kampuni nyingine ambazo thamani ya hisa zake imeongezeka ni kampuni ya Habari ya NMG (National Media Group) ambayo imepanda kwa asilimia 3.33 na  Acacia (asilimia 1.33).


Zinazohusiana: 


EABL ndiyo kampuni iliyofanya vibaya zaidi leo sokoni huku nyingi zikibaki katika viwango vilivyokuwepo jana zikiwemo Vodacom, benki ya CRDB, DCB na NMB.

Hata hivyo, benki ya CRDB  imeongoza kwa  kuuza kiwango kikubwa cha hisa sokoni leo kwa kuuza hisa 64,355 sawa na asilimia 66.8 ya hisa zote zilizouzwa ikifuatiwa na TBL (asilimia 27.9) na Vodacom (asilimia 5.2). 

Related Post