Wawekezaji wa Acacia soko la hisa Dar tabasamu tupu

Nuzulack Dausen 1157Hrs   Mei 14, 2019 Biashara
  • Wawekezaji wa kampuni hiyo ya madini leo wamevuna Sh100 zaidi kwa kila hisa kutoka bei ya jana.
  • Wenzao wa CRDB ni miongoni mwa waliopoteza zaidi leo.

Dar es Salaam. Wawekezaji wa kampuni ya Acacia (ACA) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) leo watalala na tabasamu baada ya thamani ya hisa za kampuni hiyo kupanda kwa asilimia 2.25 na kuwafanya waweke kibindoni Sh100 zaidi kwa kila hisa moja kutoka kiwango cha jana Mei 13, 2019.

Ripoti ya soko ya siku ya DSE ya Mei 14 inaonyesha kuwa hadi soko linafungwa thamani ya hisa moja ya Acacia ilikuwa ni Sh4, 550 kutoka Sh4,450 iliyorekodiwa jana.

Hata wakati wawekezaji wa Acacia wakinehemeka leo, wenzao wa CRDB watalala na maumivu baada ya thamani ya hisa za benki hiyo kushuka kutoka Sh130 kwa hisa moja iliyorekodiwa jana wakati soko linafungwa hadi Sh120 leo hii jioni. 


Zinazohusiana: M-pesa, intaneti vyachangia Vodacom Tanzania kupata faida ya Sh90 bilioni


Licha ya thamani za hisa za CRDB kushuka, bado ndiyo kampuni iliyoongoza kwa kuuza kiwango kikubwa cha hisa sokoni leo.

Kampuni nyingine ambazo thamani ya hisa zake imeshuka leo ni Shirika la Ndege la Kenya (KA) kwa asilimia 5.88, Kampuni ya Habari ya NMG (asilimia 2.34) na Kampuni ya bia ya East African Breweries Ltd (EABL).

Acacia ndiyo kampuni iliyofanya vizuri zaidi leo sokoni huku nyingi zikibaki katika viwango vilivyokuwepo jana zikiwemo Vodacom, na TICL licha ya kutangaza mwenendo mzuri wa kimapato wa kampuni zao hivi karibuni.

Related Post