Wizara ya Viwanda na Biashara imeomba kuidhinishiwa bajeti ya Sh110.9 bilioni kwa mwaka 2024-25
- Yaongezeka kwa Sh18.5 bilioni sawa na asilimia 21.
- Kamati haijaridhishwa na upatikanaji wa kusuasua wa fedha kwa wizara hiyo.
- Yaitaka Serikali kuongeza na kutoa fedha kwa wakati kufanikisha miradi ya wizara.
Dar es Salaam. Wizara ya Viwanda na Biashara imeliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya makadirio ya matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 Sh110.9 bilioni ili kufanikisha shughuli mbalimbali za wizara.
Bajeti hiyo kama itapitishwa na Bunge bajeti hiyo itakuwa imeongezeka kwa asilimia 21 kutoka Sh92.3 bilioni iliyoidhinishwa mwaka 2023/24.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Ashatu Kijaji, aliyekuwa akiwasilisha bajeti yake Mei 21, 2024 bungeni jijini Dodoma amesema kati ya fedha hizo Sh81.1 bilioni sawa na asilimia 73.1 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh29.8 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
“Katika Sh81.1 bilioni ya matumizi ya kawaida Sh68.4 bilioni ni kwa ajili ya mishahara na Sh12.8 bilioni zinaombwa kwa ajili ya matumizi mengineyo,” amesema Kijaji.
Uchambuzi zaidi wa bajeti hiyo unaonesha kupungua kwa fedha za miradi ya miradi ya maenedleo kutoka asilimia 27.7 ilyotengwa hadi asilimia 26.8 katika bajeti ya mwaka wa fedha ukaoanza Julai, 2024.
Soma zaidi:TASAC:Tumeanza kuchunguza chanzo cha meli kuzama ziwa Victoria
Upatikanaji wa fedha za miradi ya maendeleo hauridhishi
Wakati fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikipungua, Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda Biashara Kilimo na Mifugo imesema mwenendo wa utoaji wa fedha hizo hauridhishi na unasababisha kusua sua kwa miradi hiyo nchini.
“Mwenendo wa upatikanaji wa fedha za ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo haukuwa wa kuridhisha kwani hadi kufikia machi 2024, wizara ilipokea asilimia 37 ya fedha zilizoidhinishwa…
… hali hiyo inaonesha kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi hicho ulikuwa nyuma kwa asilimia 63,” amesema Francis Mtinga mjumbe wa kamati hiyo aliyemuwakilisha mwenyekiti wake Deodatus Mwanyika.
Pamoja na Serikali kuendelea kuongeza bajeti ya wizara ya viwanda na biashara, bado kamati inaona kuwa kiasi hiki ni kiwango kidogo kuweza kufikia mapinduzi ya viwanda yanayokusudiwa hivyo, inaomba Serikali kuendelea kuongeza na kutoa fedha kwa wakati.
“Serikali iboreshe mazingira ya uwekezaji ili sekta binafsi ziendelee kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vitakavyoongeza ajira, uongezaji wa tathmini ya mapato ya fedha za kigeni,” amesema Mtinga.
Vipaumbele 6 vya wizara hivi hapa
Katika mwaka wa fedha 2024/25 wizara imeainisha vipaumbele 6 ambavyo vitatekelezwa na shughuli za wizara ikiwemo kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kielelezo na kimkakati ikiwemo mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma na Chuma cha Liganga.
Waziri Kijaji amebainisha kuwa Serikali inaendelea na majadiliano na mwekezaji ilikuhitimisha na kuanza utekelezaji wa mradi huo kama ilivyoagizwa na Rais Samia Suluhu wakati akizindua kiwanda cha kuunganisha malori na matipa kinachomilikiwa na Kampuni ya Sturn Corporation Mei9,2024 jijini Dar es Salaam.
Licha ya ahadi hiyo, Kamati ya Viwanda, Kilimo na Mifugo imesema, haijaridhishwa na kusuasua kwa mradi huo kwa muda mrefu na imeishauri Serikali ikamilishe majadiliano na muwekezaji ili kazi za uchimbaji wa chuma na makaa yaanze haraka.
Vipaumbele vingine ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma kwa kuimarisha miundombinu na mazingira wezeshi kwa uwekezaji, viwandani na ufanyaji biashara.
Pia, wizara itachochea maendeleo ya watu kwa kuboresha miradi na programu katika sekta za kiuchumi na kijamii inayohusisha elimu na mafunzo ya ujuzi pamoja na kufanya intelijensia ya masoko ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini kwenye masoko ya kimkakati na kimataifa na kuchochea ukuaji wa sekta binafsi nchini.
Latest
