Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo yapewa asilimia 45 ya bajeti 2022-23
- Yapata asilimia 32 tu ya bajeti ya miradi ya maendeleo
- Ni wizara iliyopata bajeti ndogo zaidi mwaka 2022/23
- Bajeti ya mwaka 2023/24 yashuka zaidi, Kamati ya Bunge yasema haijaridhishwa
Dar es Salaam, Huenda azma ya Serikali ya kukuza, kuendeleza na kufanya mageuzi katika sekta ya sanaa na michezo nchini ikasalia kuwa ndoto mara baada ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuidhinishiwa fedha kidogo kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli zake.
Kati ya Sh35.4 bilioni zilizoombwa na wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ni asilimia 45 tu ya fedha hizo zimetolewa na Serikali.
Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Husna Juma Sekiboko aliyekuwa akisoma uchambuzi wa bajeti uliofanywa na kamati hiyo leo Juni 6, 2023 amewaambia wabunge kuwa mpaka mwezi Februari 2023, Serikali imetoa jumla ya Sh19.3 bilioni pekee.
“Serikali imetoa asilimia 33.6 ya fedha za mishahara zilizoombwa asilimia 35.1 ya fedha za matumizi mengineyo na asilimia 32 ya fedha za miradi na maendeleo zilizoidhinishwa,” amesema Sekiboko Bungeni jijini Dodoma.
Kwa mwaka 2022/23 bunge liliidhinisha Sh15.8 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo Serikali imetoa Sh5.2 bilioni pekee wakati zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya kuanza mwaka mpya wa fedha yaani Julai mosi.
Soma zaidi
-
Wizara tano zilizoidhinishiwa fedha nyingi 2022-23
-
Deni la Serikali Tanzania laongezeka, lavuka Sh60 trilioni
-
Zaidi ya nusu ya bajeti Wizara ya Fedha kulipa deni la Serikali
Kwa mujibu wa kamati hiyo kiasi hicho ni kidogo ukilinganisha na majukumu ya Wizara hiyo ambayo ni kukuza, kulinda, na kuendeleza utambulisho wa mtanzania katika nyanja ya ubunifu, utamaduni, sanaa na michezo.
Ufinyu wa bajeti pamoja na kutotoa fedha kwa wakati ni miongoni mwa sababu zinazokwamisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika sekta hiyo.
Bajeti ya maendeleo 2023/24 yashuka
Pamoja na Wizara hiyo kupokea fedha chini ya asilimia 50 ya bajeti iliyoidhinishwa pamoja na asilimia 32 tu ya fedha za miradi ya maendeleo, fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwa mwaka 2023/24 imepungua kwa asilimia 25 kulinganisha na mwaka uliopita kutoka Sh15.8 bilioni hadi Sh11.8 bilioni.
“Kamati haijaridhishwa na hatua ya Serikali kupunguza bajeti ya miradi ya maendeleo, hatua hii haiendani kabisa na nia ya Serikali hususani maelekezo ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ya kukuza na kuimarisha sekta ya utamaduni na sanaa nchini na haiakisi muamko wa Watanzania ya kupenda na kukumbatia sekta hii muhimu,” amesisitiza Sekiboko.
Ili kuiongezea nguvu wizara hiyo kufanya kazi ipasavyo, kamati imeishauri Serikali kuongeza fedha za miradi ya maendeleo angalau kuwa sawa na ya mwaka uliopita au zaidi.
Hivi karibuni sekta ya michezo na sanaa imekuwa na mwamko mkubwa kupitia ushiriki wa wanamichezo na wasanii katika mashindano na majukwaa mbalimbali na kuiwakilisha vyema nchi.
Mafanikio makubwa zaidi ya hivi karibuni ni pamoja na Klabu ya michezo ya Yanga kushika nafasi ya pili katika Mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, pamoja na Mtanzania Gabriel Geay kushinda nafasi ya pili katika mbio ndefu nchini Uingereza.
Kwa mwaka 2023/24 Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imepanga kutumia Sh35.4 bilioni ambapo kati ya fedha hizo Sh23.4 bilioni ni kwa ajili ya mishahara na matumizi mengineyo na Sh11.8 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Bajeti ya maendeleo ya wizara hiyo kwa mwaka ujao ni sawa na asilimia 0.04 ya bajeti ya Serikali katika shughuli za maendeleo ambayo ni zaidi ya Sh15 trilioni.