Wizara tano zilizoidhinishiwa fedha nyingi 2022-23

June 14, 2022 4:43 am · David
Share
Tweet
Copy Link
  • Ipo Wizara ya Fedha na Mipango, Ujenzi na Uchukuzi.
  • Wizara hizo tano kwa pamoja zitatumia zaidi ya nusu ya bajeti yote.
  • Bajeti Kuu ya Serikali kuwasilishwa Juni 14 mwaka huu.

Dar es Salaam. Wakati macho na masikio ya Watanzania yakisubiri Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/23 itakayowasilishwa wiki ijayo, wizara tano ikiwemo ya Fedha na Mipango ndiyo zitakazotumia kiwango kikubwa cha fedha cha bajeti hiyo. 

Bajeti hiyo ambayo ni ya pili kwa kipindi cha kwanza cha miaka mitano ya Rais Samia Suluhu Hassan inatarajiwa kuwa Sh41 trilioni ikiwa imepanda kutoka Sh37.9 trilioni ya mwaka huu wa 2021/22 unaoishIa Juni 30.

Uchambuzi wa bajeti uliofanywa na Nukta (www.nukta.co.tz) umebaini kuwa Wizara za Fedha na Mipango, Nishati, Ujenzi na Uchukuzi na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ndiyo zimeidhinishiwa kiwango kikubwa cha fedha katika bajeti zao.

Nyingine ni Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Fedha zilizoidhinishwa kwa wizara hizo ni zaidi ya Sh1 trilioni kwa kila moja. Jumla ya fedha zitakazotumika katika wizara hizo ni zaidi ya nusu ya bajeti yote.

1. Wizara ya Fedha na Mipango

Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo imepangiwa kiasi kikubwa kuliko wizara zote ambapo itatumia Sh14.9 trilioni sawa na asilimia 36.3 ya bajeti yote.

Kati ya kiasi hicho cha fedha, Sh13.6 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kiasi kilichobaki ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.  

Hata hivyo, sehemu kubwa ya fedha hizo zitatumika kulipa deni la Serikali ambalo linaongezeka kila mwaka.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake hivi karibu alisema Sh9.09 trilioni sawa na asilimia 60.8 ya bajeti ya wizara yake zitatumika kulipa deni la Serikali. 

Dk Nchemba amesema kwa mwaka 2022/23 wizara yake itajikita katika  vipaumbele nane ikiwemo kukusanya, kutafuta na kudhibiti mapato na matumizi ya Serikali, kuhudumia kwa wakati deni la Serikali pindi linapoiva na kufanya tathimini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ikiwa ni maandalizi mahususi ya Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Soma zaidi:


2. Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)

Wizara ya pili itakayotumia kiasi kikubwa cha fedha ni Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambayo imeidhinishiwa Sh8.7 trilioni. 

Kati ya fedha zinazoombwa, Sh5.5 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida yanayojumuisha mishahara na matumizi mengineyo.

Waziri wa Tamisemi Innocent Bashungwa aliliambia Bunge kuwa baadhi ya mipango itakayotekeleza na wizara yake mwaka 2022/23 ni pamoja kusimamia utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Ofisi ya Rais- Tamisemi ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi, ufuatiliaji, na tathmini kuhusu utekelezaji wa shughuli za Serikali, taasisi na miradi katika ngazi ya mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

3. Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi nayo imebahatika kuingia katika orodha ya wizara zilizopata fedha nyingi baada ya kuidhinishiwa na Bunge Sh3.8 trilioni.

Kati ya fedha hizo, Sh1.4 trilioni ni kwa ajili ya sekta ya ujenzi huku uchukuzi ikipata Sh2.4 trilioni sawa na theluthi mbili au asilimia 66 ya bajeti yote ya wizara hiyo. 

Fedha hizo za uchukuzi zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya usafiri wa majini na nchi kavu.

Katika mwaka wa fedha wa 2022/23, Serikali itaendelea na uboreshaji wa usafiri wa majini ili kurahisisha shughuli za biashara. Picha| Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

4. Wizara ya Nishati

Namba nne imeenda kwa Wizara ya Nishati ambayo ina jukumu kubwa la kuwaangazia wananchi kwa nishati ya umeme unaotumika nyumbani na maeneo ya uzalishaji. 

Waziri January Makamba aliyewasilisha bajeti ya wizara yake hivi karibuni mwaka 2022/23 amesema Wizara ya Nishati inakadiria kutumia Sh2.7 trilioni ikilinganishwa na Sh2.3 trilioni iliyotengwa 2021/22.

Hata hivyo, hadi kufikia Mei 2022 Wizara ilipokea jumla ya Sh1.82 trilioni sawa na asilimia 76.3 ya bajeti yote ya wizara hiyo ya mwaka huu.

Aidha, Wizara hiyo imebainisha kuwa miongoni mwa vipaumbele katika mwaka wa fedha 2022/23 ni kuendelea kupeleka nishati vijijini, kukamilisha mradi wa gesi asilia (LNG) pamoja na kujenga hifadhi za kimkakati wa mafuta nchini.

5. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeshika nafasi ya tano baada ya kuidhinishiwa bajeti ya Sh2.7 trilioni katika mwaka wa fedha 2022/23 ikiongezeka kutoka Sh2.3 trilioni iliyopitishwa mwaka 2021/22.

Hadi kufikia Aprili 2022 wizara ilipokea Sh1.9 trilioni sawa na asilimia 81.80 ya bajeti iliyoidhinishwa kwa mwaka huu.

Hata hivyo bajeti hiyo ya mwaka ujao ndiyo bajeti ya kiwango cha juu kabisa kwa wizara hiyo ndani ya miaka minne iliyopita. 

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema kati ya fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya mwaka ujao, Sh230.3 bilioni sawa na asilimia 8.5 ya bajeti yote zitaelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama katika mapendekezo yake kuhusu bajeti hiyo imeishauri Serikali kutoa fedha zilizoidhinishwa kwa wakati kwa wizara hiyo ili shughuli zilizopangwa zifanyike kwa wakati.

Wizara tano zalizopata ndogo 

Wakati wizara hizo tano zikiidhinishiwa kitita kikubwa cha fedha zipo baadhi ya wizara zimeambulia kiasi kidogo cha fedha ikiwemo ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ambayo imeidhinishiwa Sh99.1 bilioni.

Wizara nyingine ni Madini iliyopata Sh83.4 bilioni, Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira (Sh53 bilioni), Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum (Sh43.4 bilioni) na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iliyoidhinishiwa Sh35.4 bilioni.

Bajeti Kuu ya Serikali itakua na sura gani? Vipi kodi zitapanda au kushuka? Na vipaumbele? Tukutane Jumanne Juni 14, 2022, Waziri Nchemba atakaposilisha mapendekezo ya Serikali.

Enable Notifications OK No thanks