WHO yaja kivingine mapambano dhidi ya Uviko-19
- Yafanya moboresho ya mkakati wa utoaji chanjo ya Uviko-19.
- Itaongeza kasi kuwafikia watu walio hatarini wakiwemo wazee na wahudumu wa afya.
Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limefanya maboresho ya mkakati wa utoaji chanjo ya Uviko-19 ili kukabiliana na kuenea kwa virusi vipya ya Omicron, kuendeleza ushahidi unaopatikana kutokana na kutolewa chanjo na kujifunza kutokana na matokeo ya programu za utoaji chanjo duniani kote.
Maboresho yamefanyika kuutokana na kuendelea kunyumbulika kwa virusi vya ugonjwa huo, jambo linaloleta changamoto katika ufanisi wa chanjo inayotolewa.
Taarifa ya WHO iliyotolewa Julai 22 jijini Geneva Uswisi imesema lengo la kuu la mkakati huo ni kutumia dozi mbili zinazotolewa za Uviko-19 ili kupunguza vifo pamoja na wagonjwa mahututi ili kulinda mifumo ya afya , jamii na uchumi.
Hii ni njia mojawapo ya kufikia lengo la utoaji wa chanjo kwa asilimia 70, nchi zikielekea katika utoaji chanjo kwa asilimia 100 kwa wafanyakazi wa sekta ya afya na makundi mengine ambayo yanaweza kuathirika zaidi wakiugua Uviko-19 kama wazee na wale wasio na kinga madhubuti.
Mkurugenzi Mtendaji wa WHO Dk Tedros Ghebreyesus amesema utoaji chanjo kwa wote walio hatarini zaidi ni njia bora zaidi ya kuokoa maisha, mifumo ya afya na kuweka jamii na uchumi wazi.
“Hata pale ambapo chanjo imetolewa kwa asilimia 70, ikiwa idadi kubwa ya wafanyakazi wa sekta ya afya, wazee na watu walio katika makundi hatarishi wakiwa hawajapata chanjo, vifo vitaendelea , mifumo ya sekta ya afya itasalia katika shinikizo kubwa na dunia itashindwa kupona kutoka kwenye hatari hii,” ameeleza Dk Tedros.
Zinazohusiana:
- Mikakati ya Tanzania kukabiliana na virusi vya Corona
- Picha, sauti ya uzushi virusi vya corona zinavyojipenyeza mtandaoni Tanzania
- Unayotakiwa kufahamu kuhusu virusi vya Corona
Katika kuhakikisha utoaji chanjo unafikia makundi yanayolengwa, mkakati huo umehimiza haja ya kupima mafanikio ya utoaji chanjo katika makundi hayo pamoja na kutengeneza mbinu zinazolenga kuwafikia.
Mbinu hizo ni pamoja na kutumia takwimu za kwenye jamii na kuzishirikisha jamii husika katika kuendeleza utoaji wa chanjo na kuwafikia kila kundi ndani ya jamii.
Mkakati huo pia una lenga kurahakisha maendeleo na kuhakikisha kuna upatikanaji sawa wa chanjo ili kupunguza kiasi kikubwa cha uambukizanaji wa virusi kama kipaumbele cha kwanza lakini pia kinga ya kudumu na kinga kwa jamii..
Utoaji chanjo ya Uviko-19 ndiyo umekuwa mkubwa na wa haraka duniani kote katika historia lakini bado watu wengi walio hatarini wanasalia bila kuwa na ulinzi huo.
Ni asilimia 28 pekee ya wazee ndiyo wamepata chanjo huku wafanyakazi wa sekta ya afya waliopata chanjo wakiwa ni asilimia 37 katika nchi zenye kipato cha chini. Na kati yao wengi bado hawajapokea dozi ya pili ya kinga dhidi ya Uviko-19.
Katika awamu ya kwanza ya utoaji chanjo ya Uviko-19 inakadiriwa maisha ya watu milioni 19.8 yaliokolewa.
Kupitia mpango wa utoaji chanjo wa pamoja unaosimamiwa na umoja wa Mataifa (GAVI) zaidi ya chanjo bilioni 12 zilitolewa duniani.
Latest