Vodacom Tanzania yapendekeza gawio la Sh23.91 kwa hisa 2026
- Ikiwa gawio hilo litapitishwa itakuwa ni sawa na ongezeko la asilimia 23.8 ikilinganishwa na gawio la Sh20.20 lililotangazwa mwaka 2025.
Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC imependekeza gawio la faida la Sh23.91 kwa kila hisa ya kawaida kwa mwaka unaoishia Machi 31, 2026, ikiwa ni siku chache tu baada ya kutangaza faida ya kihistoria kwa robo mwaka unaoishia Juni 30, 2026.
Ikiwa gawio hilo litapitishwa katika Mkutano Mkuu wa mwaka 2026 unaotarajiwa kufanyika Agosti 20, 2026 itakuwa ni sawa na ongezeko la asilimia 23.8 ikilinganishwa na gawio la Sh20.20 kwa kila hisa lililotangazwa katika mwaka ulioishia Machi 31, 2025.
Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni hiyo inapendekeza kuwalipa wanahisa Sh53.558 bilioni sawa na asilimia 50 ya faida baada ya kodi ya mwaka wa fedha uliopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Vodacom, wenye haki ya kupata gawio hilo linalotarajiwa kulipwa Oktoba 15, 2026 ni wanahisa watakaokuwa wameandikishwa kwenye daftari la wanahisa pamoja na watakaonunua hisa kufikia Agosti 14, 2026 (cum-dividend).
Hii itakuwa ni mara ya tatu mfululizo gawio la kampuni ya Vodacom kuongezeka, fursa inayowapa wawekezaji wake marejesho ya uwekezaji wao.
Kulinganisha na miaka mitatu iliyopita gawio kwa kila hisa kutoka Vodacom limeongezeka kwa asilimia 66.7 baada ya kubaki katika kiwango cha Sh15 kwa kila hisa kwa miaka ya 2022 na 2023 kufuatia hasara ya Sh30.1 bilioni iliyorekodiwa mwaka 2021.
Kiwango cha gawio kilichopendekezwa na Vodacom ni sehemu ya Sh107.1 bilioni ya faida baada ya kodi iliyorekodiwa na kampuni hiyo katika kipindi cha mwaka ulioishia Machi 31, 2026.
Vodacom ni kampuni pekee ya mawasiliano iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Vodacom yenye hisa bilioni 2.24 katika soko la DSE inatoa gawio hilo ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa sera yake ya kugawa nusu ya faida kwa wanahisa.
Licha ya uwekezaji mkubwa katika uboreshaji wa miundombinu, faida baada ya kodi ya Vodacom mwaka unaoishia Machi 31, 2026 iliongezeka kwa asilimia 18 kutoka Sh90.5 bilioni iliyorekodiwa katika mwaka unaoishia Machi 31, 2025, kiwango cha juu zaidi kurekodiwa ndani ya miaka saba.
Hata hivyo, gawio pendekezwa bado lipo chini ukilinganishwa na viwango vilivyotolewa na kampuni kubwa nyingine zilizoorodheshwa DSE kama benki za biashara za CRDB na NMB.