Fahamu usalama, ufanisi wa chanjo ya Uviko-19
- Kabla haijaidhinishwa hufanyiwa majaribio kwa wanyama kisha binadamu.
- Chanjo ya Uviko-19 imeepusha zaidi ya vifo milioni 20 duniani kote.
Dar es Salaam. Ni takribani miaka minne sasa imepita tangu dunia ikabiliwe na janga la ugonjwa wa homa ya mapafu maarufu kama Uviko-19, ambao uliripotiwa kwa mara ya kwanza huko Wuhan nchini China Disemba 31 mwaka 2019.
Mwaka mmoja mara baada ya janga la Uviko-19 wanasayansi walifanikiwa kugundua chanjo ambayo inaweza kuuongezea mwili kinga na kupambana na virusi hivyo ambavyo vimeondoa uhai wa mamilioni ya watu duniani.
Badala ya ugunduzi wa chanjo kuleta ahueni kama ilivyotarajiwa ukaibuka mgogoro mwingine kati ya wataalamu wa afya na watu waliokuwa hawaamini katika chanjo ambao kwa kiasi kikubwa walikuwa na mitazamo hasi pamoja na fikra potofu kuhusu usalama wao na ufanisi wa chanjo.
Licha ya kwamba kwa kiasi kikubwa lengo la ugunduzi wa chanjo ya Uviko-19 limefanikiwa, bado kuna baadhi ya watu hawana imani nazo na wanaishi katika misingi ya fikra potofu. Kama wewe ni miongoni wao makala haya yanakuhusu.
Kwa mujibu wa wataalamu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kabla chanjo haijaruhusiwa kutumika kwa binadamu hupimwa kwanza katika mambo yafuatayo;
Usalama
Kabla chanjo haijaidhinishwa kutumika kwa binadamu hufanyiwa kwanza majaribio kwa wanyama katika kliniki maalum za majaribio. Baada ya hapo hufanyika majaribio mengine matatu kwa binadamu kwa ajili ya kuangalia ufanisi na usalama wa chanjo husika.
Zinazohusiana
Ni wakati gani unatakiwa kupata ‘booster’ ya Uviko-19?
Kraken: Kirusi kipya cha Uviko-19 kinachowatesa wanasayansi
Wanyama pamoja na binadamu wanaoshiriki kwenye majaribio huwa katika uangalizi maalum wa wataalamu wa afya kipindi chote cha majaribio ili kubaini kama kuna dosari au jambo lolote la kushughulikiwa.
Usalama wa chanjo ya Uviko-19 umedhihirika mara baada ya kutoripotiwa kwa visa vya matokeo hasi ya chanjo bali kupungua kwa vifo pamoja na kasi ya maambukizi.
Ufanisi
Kwa mujibu wa WHO, ufanisi wa chanjo hupimwa kwa kuangalia namna inavyopunguza hatari ya mwili kushambuliwa na ugonjwa tofauti ya yule ambaye hajachanja jambo ambalo hufanyika katika vituo maalumu vya majaribio.
Chanjo ikionyesha ufanisi kwa asilimia 90 maana yake waliopatiwa chanjo wana asilimia 90 za kuwa salama unapotokea ugonjwa kuliko wale ambao hawakuchanja.
“Hata hivyo asilimia 10 iliyosalia haimaanishi kuwa waliopatiwa chanjo watapatwa na ugonjwa,” inasema WHO.
Kutokana na ufanisi wa chanjo ya Uviko-19, WHO inaeleza kuwa zaidi ya watu milioni 20 wameepuka vifo ambavyo vingetokana na janga hilo.
Uwezo
Hapa sasa chanjo inaangaliwa namna inavyoweza kukabiliana na ugonjwa husika katika mazingira halisi, kama maambukizi, idadi ya watu wanaolazwa pamoja na vifo vinavyotokea.
Tafiti za kisayansi zimeonyesha kuwa asilimia kubwa ya watu wanaolazwa, kesi za maambukizi mapya pamoja na vifo ni wale ambao hawajapata dozi kamili ya chanjo.
Kwa mujibu wa data za WHO mpaka Februali 13 mwaka huu, jumla ya dozi bilioni 13.2 zimetolewa duniani kote huku watu bilioni 5.5 wakipata dozi moja ya chanjo na watu bilioni 5 wakipata dozi kamili.
Nchini Tanzania hali ni shwari, kwani kwa mujibu wa WHO zaidi ya watu milioni 29 wameshapata dozi kamili ya chanjo ya Uviko-19 ambapo lengo lilikuwa ni kuchanja watu milioni 30.
Hujapata chanjo, Unasubiri nini?