Chanjo ielekezwe kwa walio hatarini kupata Uviko-19

April 11, 2023 12:23 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni maeneo yanayokabiliwa zaidi na kirusi kipya cha Omicron.
  • Wazee na wenye magonjwa sugu wakumbukwe.
  • WHO yasisitiza matumizi ya ‘booster’ kuimarisha kingamwili. 

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limeendelea kusisitiza kuwa chanjo dhidi ya Uviko-19 ielekezwe katika maeneo yenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo ili kuokoa maisha watu. 

Hadi kufikia Aprili 6 mwaka huu watu milioni 762.2 wamepata ugonjwa huo huku vifo milioni 6.8 vikiripotiwa duniani kote, kwa mujibu wa WHO ambayo hadi Aprili 3 imeeleza kuwa dozi za chanjo bilioni 13.3 zimetolewa kukabiliana na ugonjwa huo.

Licha ya kazi nzuri inayofanywa na WHO, Kamati ya Wataalam wa Chanjo wa WHO (SAGE) hivi karibu ilifanya mapitio ya mpango wake wa kutoa chanjo ili kuendana na mabadiliko ya kirusi cha Omicron cha ugonjwa huo. 

SAGE katika taarifa yake iliyotolewa Machi 28, 2023 inasisitiza kuwa kumshinda adui huyo, chanjo ipewe kipaumbele katika maeneo yanayokumbwa zaidi na kirusi kipya cha Omicron (SARS-CoV-2) ili kuwaokoa watu wengi na janga hilo. 

Pia kamati hiyo inasisitiza kuimarisha mifumo ya huduma za afya huku ikichagiza matumizi ya dozi za chanjo za nyongeza (booster) kwa watu waliopata afua hiyo ili kuimarisha kinga za miili yao. 

“Mpango kazi wa sasa unasisitiza umuhimu wa kuwapa chanjo wale ambao bado wako katika hatari ya ugonjwa huo hasa wazee na wale walio na hali ya chini,” alisema Mwenyekiti wa SAGE Dk Hanna Nohynek wakati akitoa taarifa ya kuboresha mfumo wa usambazaji chanjo duniani Machi mwaka huu.

 “Nchi zinapaswa kuzingatia muktadha wao mahususi katika kuamua kama zitaendelea kutoa chanjo kwa vikundi vilivyo katika hatari ndogo, kama vile watoto wenye afya njema na vijana, huku zikizingatia chanjo za kawaida ambazo ni muhimu sana kwa afya na ustawi wa kikundi hiki cha umri,” alisisitiza Dk Nohynek. 

Baadhi ya makundi yanayopendekezwa kupewa kipaumbele ni wazee na watu wazima wenye magonjwa sugu ikiwemo moyo na kisukari. 

Wengine ni watu wenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na watoto wenye umri wa miezi sita na zaidi, wajawazito; na wafanyakazi wa afya walio mstari wa mbele.

Pia wataalam wa afya wanasisitiza watu kuvaa barakoa, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kutumia vitakasa mikono na kunawa mikono kwa maji tiririka. 

Enable Notifications OK No thanks