Mikakati ya Tanzania kukabiliana na virusi vya Corona
- Imeandaa mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza kwa wagonjwa endapo watajitokeza.
- Yaimarisha ukaguzi mipakani na katika viwanja vya ndege.
- Yasema mpaka sasa hakuna mtu yeyote nchini aliyeambukizwa virusi hivyo.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema wanachukua hatua mbalimbali kukabiliana na tishio la virusi vya Corona ikiwemo kuandaa maeneo maalumu ya matibabu kwa wagonjwa endapo watajitokeza na kutoa mafunzo kwa watumishi wa sekta ya afya.
Virusi hivyo ambavyo chimbuko lake ni katika mji wa Wuhan nchini China vimeua watu zaidi ya 106 na wengine zaidi ya 4,000 wakiambukizwa.
Ummy aliyekuwa akizungumza jijini Dodoma leo (Januari 29, 2020) amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huo kwenye mipaka na vituo vyote vya huduma ambapo watoa huduma wanazingatia na kuwa makini zaidi kwenye uchunguzi hasa kwa watu wanaotoka nje ya nchi.
“Tufanya uchunguzi wa wasafiri wote kutoka bara la Asia kwenye mipaka yetu ikiwemo viwanja vya ndege vya Mwalimu Julius Nyerere, Kilimanjaro na Mwanza; na bandari ya Dar es Salaam,” amesema Ummy mbele ya wanahabari.
Amesema katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, wamefanya uchunguzi wa raia 1,520 waioingia nchini kutokea China na Asia kupitia mipakani na abiria kwa ndege zote zinazoingia nchini.
Pia wizara hiyo ina vipima joto 140 (vya mkono 125 na vya kupima watu wengi kwa mpigo 15) ambavyo vimefungwa na vinatumika katika maeneo ya mipakani ikiwemo viwanja vya ndege na bandari.
“Katika ufuatiliaji wa ugonjwa huu na magonjwa mengine ya aina hiyo wizara inaendelea kuchukua na kupima sampuli kutoka maeneo ya ufuatiliaji na yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu sampuli zitafikishwa kwenye maabara ya Taifa kupimwa,” amesema Waziri huyo.
Soma zaidi:
- Watanzania waishio China watolewa hofu virusi vya corona
- Picha, sauti ya uzushi virusi vya corona zinavyojipenyeza mtandaoni Tanzania
Mikoa mitatu yatengwa kwa watakaopata maambukizi
Katika hatua nyingine, Ummy amesema wameandaa maeneo maalumu ya matibabu kwa wagonjwa endapo watajitokeza katika maeneo ya Mawenzi mkoani Kilimanjaro), Buswelu (Mwanza) na Kigamboni (Dar es Salaam).
Wizara inaendelea kujiandaa kukabiliana na tishio la ugonjwa huu kwa kuhakikisha vifaakinga, dawa na vifaa tiba vya kutosha vinapatikana kukabiliana na ugonjwa huu endapo utaingia nchini.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, mpaka sasa watumishi wa afya 2,297 wamekwishapatiwa mafunzo kuhusu kukabiliana na virusi hivyo.
Akihitimisha maelezo yake mbele ya wanahabari, Ummy amesema “hapa nchini hadi sasa hakuna mgonjwa wala mtu yeyote anayehisiwa kuwa na ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya “novel Corona”.
“Hivyo Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu, waendelee kuchukua hatua za tahadhari katika kujikinga na ugonjwa huu na kutosambaza taarifa zisizothibitishwa na Wizara.”
Virusi hivyo vinasambaa kwa kasi
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), tangu mlipuko wa ugonjwa huu toka uanze katika mji wa Wuhan uliopo katika jimbo la Hubei nchini China Disemba, 2019 hadi Januari 28, 2020 watu 4,593 wamethibitishwa kuugua ugonjwa huu duniani kote, ambapo kati yao wagonjwa 4,537 na vifo 106 vimetokea nchini China.
Aidha, ugonjwa huu umesambaa katika mataifa mengine 14 duniani zikiwemo Japan, Jamhuri ya Korea, Vietnam, Sangapore, Australia, Malaysia, Cambodia, Thailand, Nepal, Sri Lanka, Marekani, Canada, Ufaransa na Ujerumani.
Taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika, walioripotiwa washukiwa katika bara la Afrika wanaoendelea kufuatiliwa na kufanyiwa uchunguzi katika nchi za IvoryCost, Ethiopia, Mauritius, Kenya na Zimbabwe. Tutatolea taarifa rasmi baada ya uthibitisho kufanyika.
Dalili za ugonjwa wa Corona
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, ugonjwa huo unasababishwa na kirusi jamii ya Corona na ni kipya “Novel (New) Corona virus 2019” (2019-nCOV) ambacho ni tofauti na virusi vingine vya jamii hiyo ambavyo viliwahi kusababisha milipuko ya ugonjwa uliojulikana kama ‘SARS-CoV’ mwaka 2003 na MERS-CoV Corona Virus mwaka 2013.
Ugonjwa huu huambukizwa kwa njia ya hewa kwa kuingiwa na majimaji yenye virusi kutoka mtu mmoja kwa njia ya kukohoa au kupiga chafya au kwa kugusa majimaji au makamasi kutoka kwa mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na dalili za ugonjwa huo na dalili huanza kuonekana kati ya siku moja hadi 14 tangu kupata maambukizo.
— Wizara ya Afya Tanzania (@wizara_afyatz) January 29, 2020
Jinsi ya kujikinga
Wizara ya Afya na WHO inawataka wananchi kuchukua hatua zifuatazo ili kujikinga na ugonjwa huo:
- Kuzingatia kanuni za afya na usafi ikiwa ni pamoja na kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua mwenye historia ya kusafiri katika nchi zilizokumbwa na mlipuko au mwenye dalili zilizotajwa hapo juu.
- Unashauriwa kuepuka safari zisizo za lazima kwenda kwenye maeneo yaliyoathirika na inapolazimu kusafiri basi wapate maelezo ya kitaalamu kabla ya kuondoka nchini.
- Funika mdomo na pua wakati wa kukohoa kwa kitambaa safi au nguo uliyovaa sehemu za mikono.
- Epuka kugusana na mgonjwa mwenye dalili za magonjwa ya njia ya hewa.
- Zingatia usafi binafsi ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
- Wahi kwenye kituo cha kutolea huduma za afya endapo utakuwa na dalili zilizoainishwa.