WHO: Mataifa maskini yajumuishwe utoaji wa chanjo
- Kuna ombwe kubwa kati ya nchi masikini na zilizoendelea katika uuzaji wa chanjo mbalimbali ikiwemo ya Uviko-19
- WHO yashauri mabadiliko yafanyike ili kuokoa maisha ya watu na kujiandaa na majanga yajayo.
Dar es salaam. Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk Tedros Ghebreyesus amesema ni muhimu kufanya mabadiliko katika soko la dunia la chanjo ili kuokoa maisha ya watu, kujikinga na magonjwa na kujiandaa na majanga yajayo.
Tedros ameitoa kauli hiyo wakati ripoti ya soko la chanjo duniani iliyotolewa Novemba 9 mwaka huu ikionyesha bado kuna ombwe kubwa katika uuzaji wa chanjo za magonjwa mbalimbali ikiwemo ya Uviko-19 kati ya mataifa tajiri na nchi zinazoendelea.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa chanjo za homa ya ini pamoja na shingo ya kizazi zimetolewa kwa asilimia 41 tu katika nchi zinazoendelea huku mataifa yaliyoendelea wakipata kwa asilimia 87, jambo ambalo kwa mujibu wa Tedros linapunguza haki ya kuwa na afya.
Soma zaidi
“Haki ya kuwa na afya nzuri inahusisha haki ya kupata chanjo, ripoti imeonyesha baadhi ya nchi masikini zimekuwa zikitengwa kuipata haki hii. WHO inatoa wito wa kufanyika mabadiliko ili kuokoa maisha,” amesema Tedros.
Jumla ya dozi bilioni 16 za chanjo ziliuzwa mwaka 2021 ikiwa ni mara tatu ya chanjo bilioni 5 zilizouzwa mwaka 2019, mabadiliko ambayo yamechochewa kwa kiasi kikubwa na mlipuko wa Uviko -19.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa uhaba wa wazalishaji wa chanjo ni miongoni mwa sababu inayochochea mataifa maskini kutopewa kipaumbele katika uuzaji wa chanjo hivyo WHO imeshauri mataifa hayo kuweka mikakati ya kujitengenezea chanjo.
“WHO inatoa wito kwa serikali kuchukua hatua juu ya kuwa na mipango ya wazi ya chanjo na uwekezaji katika sekta ya afya, uzalishaji na usambazaji wa chanjo, pamoja na kuwa na vituo vya utafiti na utengenezaji wa chanjo wa kikanda,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Latest