Waziri Ndaki atishia kurejesha taa za kalabai uvuvi wa samaki
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki akizungumza katika mkutano uliowakutanisha pamoja viongozi wa serikali na wadau wa sekta ya uvuvi kutoka Kanda ya Ziwa Victoria uliolenga kuwajengea uwezo dhidi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji kwa ukuaji wa uchumi wa bluu Picha | Mariam John.
- Ni baada ya kubainika kuwa taa za umemejua zinachangia uvuvi haramu.
- Aagiza kampuni zinatengeneza taa hizo kujitafakari.
- Wavuvi haramu nao watahadharishwa.
Mwanza. Serikali imetoa muda wa miezi miwili kwa taa za umemejua kufanyiwa tathmini ya kina kama zinafaa kuendelea kutumiwa na wavuvi baada ya kuhusishwa na vitendo vya uvuvi haramu hasa katika Ziwa Victoria.
Ujio wa umemejua ambazo ni rafiki wa mazingira umesaidia wavuvi wa kupata mwanga wa uhakika wakiwa ziwani kuvua samaki na dagaa bila hofu ya kukosa nishati hiyo muhimu.
Hata hivyo, kumekuwa matumizi yasiyo sahihi ya taa hizo za umemejua zenye mwanga mkali ambazo huchangia katika uharibifu wa mazalia ya samaki.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki aliyekuwa akizungumza kwenye mkutano uliokutanisha viongozi wa Serikari na wadau wa sekta ya uvuvi kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa leo Novemba 17, 2022 na kueleza kuwa tafiti za awali zimebainisha kuwa taa za umemejua zenye mwanga mkali zinachangia katika masuala ya uvuvi haramu.
Kutokana na changamoto hiyo, Waziri Ndaki ametoa miezi miwili kuanzia sasa hadi Januari 1 mwaka 2023 kwa kampuni zinazotengeneza taa hizo kuhakikisha zinafanyia majaribio taa zake kama zinafaa kwenye uvuvi.
“Tunatoa miezi miwili baada ya mapumziko ya sherehe za mwaka mpya tutakuja na mrejesho hapa kama taa hizo zinafaa kuvulia au lah! Vinginevyo, tutarudi kwenye matumizi ya kalabai na taa za chemli,” amesema Ndaki.
Agizo la Waziri huyo ni kufuatia kikao kilichoketi mwezi Juni mwaka huu kujadili sababu zinazochangia uvuvi haramu ambapo matumizi ya taa za umemejua yalitajwa kuwa chanzo kimojawapo.
“Tulipata mapendekezo mengi kwenye kikao cha mwisho na wadau wa uvuvi kuhusu matumizi ya sola, na katika kufanya ufuatiliaji tumebaini kuwa taa za sola zinachangia kwa kiasi kikubwa uvuvi haramu,” amesema Ndaki.
Zinazohusiana:
- Njia zilizotumika kufyekelea mbali uvuvi wa mabomu Dar
- Mpina apania kujenga viwanda vya samaki, nyama nchini
- Ripoti Maalum: Mbinu za kubaini samaki waliovuliwa kwa mabomu
Taa za umemejua wavuvi wengi walianza kuzitumia zaidi miaka mitatu iliyopita baada ya Serikali kupiga marufuku matumizi ya kalabai zinazotumia mafuta ya taa ambazo zilikuwa zinasababisha ajali ikiwemo milipuko na uchafuzi wa maji.
Pia Waziri Ndaki amemuomba Katibu wa Tamisemi kupokea majina ya baadhi ya watumishi wa serikali waliobainika kujihusisha na uvuvi haramu ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yao.
Waziri huyo pia amesema, Utafiti wa kisayansi uliofanywa mwaka 2021 umebainisha kuwa samaki aina ya Sangara wamepungua kwenye ziwa Victoria kwa asilimia 50 na kwamba wengi wapo kwenye hatari ya kutoweka kutokana na uvuvi haramu na uharibifu wa mazingira.
Utaratibu uliopo ni kuwa mtego mmoja wa samaki unatakiwa kuwa taa za umemejua zenye wati 5 na wati 9 na taa hizo hazitakiwi kuwa kwenye betri badala yake zinachajishwa kabla wavuvi hawajaingia ziwani.
Matumizi ya betri na taa kwa pamoja hayaruhusiwi ziwani ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea wakati wavuvi wakiendelea na kazi zao.
Ameiomba Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kusimamia kikamilifu maeneo yenye rasilimali za uvuvi kwa kutenga asilimia tano ya mapato yanayotokana na sekta hiyo kulingana na miongozo na kamati za ulinzi za vijiji na Kata kufanya doria kwa wavuvi haramu na kuwachukulia hatua stahiki.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 katika ukanda wa Afrika zenye utajiri mkubwa wa maji ambayo ni fursa kubwa ya kukuza uchumi wa wananchi kupitia shughuli za uvuvi na kwamba inachangia asilimia 1.8 ya pato la Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima amebainisha kuwa mkoa huo unaendelea kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato kwenye sekta hiyo ili kusaidia ukuzaji wa uchumi wa nchi kupitia sekta hiyo ili kufikia malengo ya kukusanya Sh5.6 bilioni kwa mwaka 2022/23.
Latest



