Mbinu zinazotumika kutokomeza magugu maji Ziwa Victoria
- Ni pamoja na kuyang’oa, kukausha na kuyachoma moto.
- Pia kupandikiza wadudu aina ya mbawakavu ambayo huyatafuna magugu maji.
- Wadau washauri kuunganisha nguvu kuyatokomeza kabisa.
Mwanza. Ziwa Victoria ndiyo kitega uchumi chake. Kila aamkapo asubuhi mawazo na akili yake ni kufikiri namna ya kuingia katika ziwa hilo ili kujipatia samaki.
Samaki anaovua katika Ziwa hilo linalounganisha nchi tano za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania huwauza ili kujipatia kipato cha familia.
Ni Robert Charles (38), mvuvi katika mwalo wa Muswahili jijini Mwanza, ambaye anasema licha ya kujipatia kipato katika kazi hiyo ya uvuvi, magugu maji ni changamoto inayotishia shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.
Charles mwenye uzoefu wa miaka 13 katika kazi ya uvuvi anasema uvamizi wa magugu maji katika maeneo yao umesababisha kupungua kwa ufanisi wa mitumbwi ya kuvulia samaki.
Wakati mwingine hulazimika kuyaondoa magugu maji yaliyotanda kwenye maji ili kupata njia ya kupitisha mitumbwi, jambo ambalo limekuwa likipunguza muda wa kuvua samaki na faida wanayoipata.
“Unakuta gugu maji limetanda kwenye njia ambazo mitumbwi hupita, hali hiyo husababisha mvuvi kushindwa kuendelea na shughuli zake kwa kuwa anaweza kuingia hasara ya kutengeneza mtumbwi,” anasema Charles.
Mvuvi huyo mwenye watoto wanne anasema kadhia hizo za magugu maji zimekuwa zikiwapatia hasara ikiwemo kuharibika kwa mitumbwi na mashine za uvuvi.
“Binafisi nimepata hasara nyingi za kupoteza taa na nyavu zangu nakumbuka mwaka 2013 na 2014 kulikuwa na gugu maji kubwa ziwani upepo unavuma linasukumwa na kwenda kutanda kwenye maeneo ambayo tumeweka nyavu na kuondoka nazo,” anasema Charles.
Magugu maji ni ni mimea inayoota na kuenea majini na ina uwezo wa kuzaliana kwa wingi na kuchukua sehemu kubwa ya ziwa, mto au bwawa na hivyo kuathiri shughuli mbalimbali ikiwemo uvuvi.
Baadhi ya magugu maji hayo hutanda sehemu za mazalia ya samaki au nyavu zilipotegwa na hivyo kuathiri uzalishaji wa samaki.
“Gugu maji linaposafiri linakuwa linabeba vitu vingi vya hatari ikiwemo miiba, nyavu na hata linapotanda linasababisha kuwa nyumba za wanyama wakali ikiwemo nyoka na mamba,” anasema mmoja wa wavuvi ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Magugu maji siyo kero tu kwa wavuvi, bali yamekuwa yakiwatesa watumiaji wengine wa ziwa hilo zikiwemo mamlaka za usafirishaji maji zinazosimamia vivuko na meli kwa kusababisha ajali na madhila mengine ya ziwani.
Baadhi ya vijana wakiondoa magugu maji katika Ziwa Victoria. Picha| Mariam John.
Sera ya Maji ya mwaka 2002 inaziagiza mamlaka zinazozimamia maji kuhakikisha zinachukua hatua mbalimbali kudhibiti kuzaliana kwa magugu maji ili kulinda rasimali za Ziwa Victoria na ubora wa maji yanayotumika.
Ziwa Victoria ndilo ziwa kubwa zaidi Afrika likiwa chanzo kikuu cha Mto Nile, ukubwa wake ukiwa kilomita za mraba 251,000.
Tanzania inachukua sehemu kubwa ya ziwa hilo kwa asilimia 44, ikifuatiwa na Kenya (asilimia 22), Uganda (asilimia 16), Rwanda (asilimia 11) na Burundi ni asilimia 7.
Ziwa hili ni muhimu kwa watu wanaoishi karibu nalo kwa shughuli za kilimo, maji ya matumizi ya nyumbani, umememaji, uvuvi na utalii.
Sababu zinachongia kuongezeka kwa magugu maji
Kuenea na kuongezeka kwa magugu maji katika Ziwa Victoria ni matokeo ya sababu mbalimbali za kibinadamu na asili.
Afisa Kilimo Masaidizi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Enrisha Mbwambo anasema uchafu na virutubisho vinavyoingizwa katika Ziwa Victoria kutoka kwenye makazi ya watu na kilimo cha bustani kinachofanyika ndani ya mita 60 ya ziwa hilo huchangia kwa sehemu kubwa ongezeko la mimea hiyo.
“Wakazi wengi wanaoishi milimani kwenye makazi holela hawana mfumo wa kuondoa maji taka na hivyo kumwaga au kutitirishia ndani ya Ziwa Victoria.
“Pia wakulima wa bustani za mboga mboga nao huchangia kwa kiasi kikubwa kutokana na mbolea ya kienyeji na viwandani inayotumika katika kilimo hicho ambapo mvua inaponyesha huzoa virutubisho hivyo na kwenda kuvimwaga ziwani,” anasema Mbwambo.
Soma zaidi:
- Mabadiliko ya tabianchi: Simulizi ya mtaa unaomezwa na Ziwa Tanganyika
- Kitendawili: Mtaa unaomezwa na maji Ziwa Victoria
Afisa Misitu na Mratibu wa shughuli za mazingira mkoani Mwanza, Mangabe Mnilago anasema magugu maji ni ‘homa’ kwa sababu yanaweza kuondoka na kurudi tena.
Mmea huo ambao husukumwa na upepo, kwa mujibu wa Mnilago uliingia katika Ziwa Victoria baada ya kusafirishwa na abiria waliokuwa kwenye meli kutoka bahari ya Mediterania hadi mto Nile.
“Kutokana na hali hiyo gugu maji hustawi na kutanda sehemu kubwa hali inayosababisha madhara kwa wavuvi na wasafiri,” anasema Mnilago.
Madhara yanayoweza kutokea iwapo magugu maji yataachwa bila kudhibitiwa ni pamoja na baadhi ya viumbe hai kushindwa kuishi na samaki kupungua au kuhamia sehemu nyingine.
Madhara mengine ni kuwa kificho cha viumbe hatari kama kenge, nyoka, mamba na kiboko na kutumia gharama kubwa ya kusafisha maji yanayotumiwa majumbani.
Kwa mujibu wa TPHPA, tathmini iliyofanyika mwaka 1999, magugu maji yalitanda ziwani hapo kwa hekali 2,000 kwa upande wa Tanzania ambapo yalipungua hadi hekaloi 106 mwaka 2017 baada ya kazi kubwa ya kuyaondoa kwa njia mbalimbali.
Wavuvi katika mwalo wa Mswahili wakiwa wameegesha vyombo vyao kabla ya kuingia katika Ziwa Victoria kusaka samaki ambao wanadai soko lake limeyumba. Picha| Mariam John.
Hatua zilizochukuliwa na wavuvi
Wavuvi wa ziwa hilo wanasema licha ya kutumia zana duni, wamekuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali kuyaondoa magugu hayo kila yanapomea katika maeneo wanayofanyia kazi kwa kuyakusanya, kuyakausha na kuyachoma.
“Huwa tunashirikiana na wadau wa mazingira katika kuliondoa gugu maji ndani ya Ziwa Victoria ingawa kazi hiyo siyo rahisi maana tunatumia njia za kienyeji katika kuliondoa,” anasema mvuvi Nyamhanga Marwa.
Marwa anasema hutumia mitumbwi kuyakusanya magugu maji hayo kwa mikono na kuyapeleka nchi kavu na baadaye kuyachoma moto.
“Tunanunua gloves(mipira ya mikononi) zetu wenyewe tunatumia mitumbwi yetu kuliondoa ingawa kuna lingine ni kubwa haliwezi kubebwa kwenye mitumbwi na baada ya hapo tunaliweka pembeni likauke ili kulichoma,” anasema Mwajuma Chamliho, Mjumbe wa Ulinzi wa Rasilimali za Ziwa Victoria (BMU).
Mwanajuma anasema hivi sasa kwenye mwalo wa Muswahili, magugu maji yamedhibitiwa ingawa hawezi kujua kama yatatarudi tena kwa kuwa husukumwa na upepo.
Baadhi ya wananchi jijini Mwanza wanasema ili kushinda vita dhidi ya magugu maji, ushirikiano na juhudi za pamoja za watumiaji wa ziwa hilo unahitajika.
“Taasisi ziendelee kushirikiana ili kuleta tija ya kazi hii turejee sera zinazohusu udhibiti wa viumbe vamizi kama gugu maji kwa ajili ya kukabiliana nao ili kulinda ziwa lisiharibiwe na gugu maji,’ anasema mkazi wa Nera jijini hapa, Yohana Kwilijiwa.
Kwilijiwa anasema amekuwa mdau anayeshiriki kampeni mbalimbali za kudhibiti mimea hiyo ndani ya Ziwa Victoria na kupandikiza mbawakavu wanaoangamiza magugu hayo.
Anasema Ziwa Victoria lina umuhimu kiuchumi kwa wananchi na Serikali hasa shughuli za uvuvi na usafirishaji, magugu maji yataachwa yatasababisha shughuli hizo kukwama na kuibua hasara hivyo jukumu ni kila mdau wa maendeleo kutokomeza mimea hiyo vamizi.
Baadhi ya wafanyakazi wa Bodi ya Bonde la Maji YA Ziwa Victoria pamoja na wafanyakazi wa kamati za rasirimali za Ziwa Victoria wakiwa wanaondoa gugumaji ndani ya Ziwa Victoria Juni mwaka 2021. Picha|Mariam John.
Serikali na wadau wanavyopambana
Kwa mujibu wa Afisa Misitu na Mratibu wa shughuli za Mazingira Mkoa wa Mwanza, Mangabe Mnilago, zipo njia mbalimbali zinazotumika kuyaondoa magugu maji ziwani ikiwa ni pamoja na kutumia njia ya kibaiolojia ya kupandikiza wadudu aina ya mbawakavu ambao hutatafuna na kumaliza mimea hiyo.
Njia nyingine ni kuyaondoa magugu maji ziwani kwa kuyazoa au kutumia mashine maalumu kisha kuyamwaga nchi kavu na baada ya muda yanakauka na kuchomwa moto.
Afisa Kilimo Masaidizi wa (TPHPA, Enrisha Mbwambo anasema wameanzisha mradi wa kuwajengea uwezo watu waliopo kwenye vikundi namna ya kujitolea katika kazi za kutokomeza magugu maji kila yanapojitokeza ziwani.
Mbwambo anasema mpaka sasa vikundi zaidi 40 vya Mkoa wa Mwanza vinafanya kazi ya kuyaondoa na kupandikiza nguvumbawa ili kuweka salama mazingira ya ziwa hilo.
Jitihada nyingine inayotolewa ni kutoa elimu kwa jamii kuacha shughuli za kilimo kando ziwa na kudhibiti usafirishaji wa magugu maji kutoka eneo moja kwenda lingine.
“Juhudi kubwa zinazofanyika ni kuwaelimisha wakulima, wanatakiwa wasifanye shughuli zozote ndani ya mita 60 za kwenye ziwa,” amesema Mbwambo.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la WAN-IFRA-Press Freedom. WAN-IFRA haihusiki kwa namna yeyote na maudhui haya.
Latest