Levina Magafu: Mwanamke mvuvi mpambanaji Ziwa Victoria
- Amekuwa akisifika kwa uhodari wake wa kuvua samaki ziwani.
- Amevua samaki ziwa kwa miaka 20 akipambana na changamoto za kijinsia.
- Serikali kumuunga mkono kutoa hamasa kwa wanawake wengine.
Mwanza. Wakati wanawake wenzake wakiwasubiri wavuvi watoke ziwani ili wanunue samaki na dagaa kwa ajili ya yeye kuzisambaza mtaani, yeye anafanya tofauti.
Badala ya kuwasubiri wavuvi, ameamua kuingia ziwani kusaka samaki hao. Ni Levina Magafu, mvuvi wa samaki katika mwalo wa Kirumba jijini Mwanza.
Levina mwenye uzoefu wa kuvua samaki katika Ziwa Victoria kwa miaka 20, anasema kazi hiyo ya uvuvi anaipenda kwa sababu imemfanya kuwa huru kifedha na kumuwezesha kuihudumia familia yake vizuri.
“Tulitengena na baba yao miaka mingi iliyopita hivyo nahudumia familia mwenyewe kama baba na mama pia,” anasema Levina, mama wa watoto watatu ambaye kila siku anahakikisha watoto wake wanakula na kwenda shule.
Mwanamke huyo ambaye awali alikuwa mkulima wa mboga mboga kando ya Ziwa Victoria anasema alipata ujuzi wa kutumia mitumbwi na kuvua samaki kutoka kwa mmoja wa wavavi ziwani hapo.
“Nilimuomba mmoja wa wavuvi wa kiume kunifundisha namna ya kusukuma mtumbwi, kulaza nyavu ili nianze kuvua ombi ambalo lilifanikiwa kwa asilimia 100,” anasema Levina kuwa tangu wakati huo amekuwa mvuvi mashuhuri.
Licha ya changamoto za ziwani ikiwemo dhoruba na upepo mkali ambao huatarisha maisha yake, anasema uvuvi ni kazi ambayo imemuhakikishia kipato cha uhakika kwa siku anaweza kuingiza Sh50,000 hadi Sh100,000.
“Kipato siyo kikubwa sana na siyo siku zote huwa naingia majini siku zingie siendi nafanya shughuli ndogo ndogo za hapa nyumbani,” anasema Levina.
Levina ni miongoni mwa wanawake nchini Tanzania ambao wmekataa kuwa tegemezi na hivyo kutumia rasilimali zinazowazunguka kujiletea maendeleo bila kusubiri kusaidiwa.
Baadhi ya wanawake wavuvi mkoani Mwanza wakisheherekea Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2022. Uvuvi ndiyo sehemu ya kujipatia kipato. Picha| Mariam John.
Kibarua alichonacho katika kazi hiyo
Levina anasema siyo rahisi kufanya kazi ya uvuvi kama siyo mvumilivu kwa sababu ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakati wakifanya shughuli hizo ikiwemo gharama kubwa za vifaa vya uvuvi na uokozi na kuporwa vitendea kazi.
“Changamoto nyingine ni kuibiwa zana zao za uvuvi ziwani hali inayowakatisha tamaa lakini pia mawimbi na upepo mkali unapovuma tunavumilia huku tukimwomba Mungu atuepushe na majanga ya ziwani,” anasema Levina.
Pamoja na changamoto hizo kwa sasa, Levina anamiliki mitumbwi miwili ya kuvulia na ameajiri vijana ambao humsaidia kwenye shughuli hiyo.
Siyo Levina peke yake ambaye anafanya kazi ya uvuvi kwenye mwalo huo. Yeye ni miongoni mwa jeshi la wanawake 20 ambao wamewekeza nguvu zao katika uvuvi kwa sababu ni miongoni mwa sekta muhimu za kiuchumi inayochangia kuondoa umasikini na kukuza uchumi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mwaka 2020, sekta ya uvuvi ilikuwa kwa asilimia 6.7 na mchango wake katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 1.71.
Sekta hiyo imetoa ajira za moja kwa moja kwa wavuvi wapatao 195,435 na wakuzaji viumbe maji 30,064 katika mwaka 2020/2021 huku zaidi ya Watanzania milioni 4.5 wameendelea kupata mahitaji yao ya kila siku kutokana na shughuli mbalimbali kwa kuunda na kutengeneza boti, kushona nyavu, biashara ya samaki na mazao yake pamoja na baba na mama lishe.

Jamii inamtazamaje Levina?
“Ni mwanamke wa mfano na wa kuigwa, kwa kuwa anaweza kufanya kazi yake bila kumtegemea mwanaume kwa kweli anastahili pongezi,” anasema Nasra Abraham, mkazi wa jijini Mwanza.
Nasra anasema pamoja na kazi yake hiyo bado anashiriki kwenye shughuli zingine za kijamii ikiwemo misibani, kwenye sherehe na hata kwenye vikundi vya akina mama.
“Tunakikundi chetu tunakaa pamoja na tumehamasika kwenda kuomba fedha za mkopo zinazotolewa na halmashauri ili ziweze kutusaidi kujikwamua kiuchumi,” anasema Nasra
Mjumbe wa ulinzi wa rasilimali za uvuvi katika mwalo wa Kirumba mkoani hapa, Marwa Rubirya anasema Levina ni mmoja wa wanawake jasiri ambaye anafanya kazi kama mwanaume.
Rubirya anasema wakati anaanza shughuli hiyo, Levina alikutana na changamoto nyingi lakini kwa sasa anafanya vizuri na ana uwezo wa kuvua kuliko hata mwanaume.
“Huwa tunamwita shujaa kwa sababu kazi anazozifanya kuna wanaume hawaziwezi, na na ushirikiano mkubwa kwa viongozi na watu wengine,” anasisitiza Rubirya.
Soma zaidi:
- Jessica Mshama: Mwanamuziki, Mjasiriamali anayebadilisha maisha ya Watanzania kwa biashara
- Simulizi ya mcheza ngoma aliyeng’atwa na nyoka zaidi ya mara 10
- Utajiri uliojificha ufugaji wa kuku wa kisasa
Kauli ya serikali na wadau wa sekta ya uvuvi
Afisa Uvuvi Mwandamizi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Liliani Ibengwe anasema wavuvi wadogo wana mchango mkubwa katika pato la Taifa, ajira na lishe.
“Kwa kutambua mchango wao , Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Chakula Duniani (FAO) tumeungana pamoja kusherekea mwaka huu ambao unajulikana kama mwaka wa wavuvi wadogo na wafugaji wa viumbe kwenye maji kwa kutambua mchango wao katika kuinua pato la Taifa lakini pia katika kuboresha afya za Watanzania kwa ujumla,” anasema Liliani
Anasema wanatambua mchango wa wanawake kwenda kuvua licha ya kuwa hawatambuliki na wanakutana na changamoto nyingi na kwamba Serikali imeunda jukwaa litakalowasaidia wanawake kuondokana na changamoto zinazoweza kuwakabili.
“Tumeandaa jukwaa la akina mama wanaojishughulisha na masuala ya uvuvi lengo ni kuwasaidia waweze kuchakata na kuuza mazao yao na pia tunawasaidia kupata soko la kuuza bidhaa zao bila bugudha yoyote,” anasema Liliani
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Emmanuel Bulay anasema Serikali imekuja na mikakati ya kuwasaidia wavuvi ikiwa ni pamoja na kuwainua kiuchumi na kuwawezesha kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo mikopo ili waweze kufanya uvuvi wenye tija.
“Asilimia 75 ya mazao ya samaki nchini yanatoka katika Ziwa Victoria hivyo tumeamua kuja na mkakati utakaowasidia wavuvi kujua kuwa Serikali iko pamoja nao katika kukabiliana na changamoto zao,” anasema Bulay.
Baadhi ya wanawake wakipiga makasikia katika Ziwa Victoria kuonyesha wanavyotumia mitumbwi kujivua samaki. Picha| Mariam John.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, samaki katika Ziwa Victoria waliongezeka kutoka tani milioni 2.6 mwaka 2019 hadi tani milioni 3.4 mwaka juzi, sawa na ongezeko la asilimia 29.27.
Ongezeko hilo limechangia kiasi cha samaki kilichopo katika maji yote kufikia tani milioni 4.1.
Naibu Waziri wa Uvuvi, Abdalah Ulega anasema serikali inaenda kuweka Mazingira mazuri ya wavuvi ikiwa ni pamoja na kuondoa utitiri wa tozo zinazowakandamiza lengo ni kuhakikisha wanasaidia katika kuchangia ukuaji wa pato la taifa.
“Kwenye kikao cha bajeti cha mwaka huu, tutapeleka mswada bungeni kurekebisha kanuni za tozo na ushuru unaotozwa na Halmshauri kwenye sekta ya uvuvi zinazomgandamiza mvuvi ili kuwe na tozo za aina moja kwenye kila halmsahauri zitakazowawezesha wavuvi kufanya kazi yao bila manung’uniko,” anasema Ulega.
Latest
