Watumiaji wa huduma za kifedha waongezeka licha ya tozo kwenye miamala ya simu
- Wameongezeka kwa asilimia 3.4 ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
- Wachambuzi wa uchumi wasema sababu ni urahisi wa upatikanaji wa huduma hizo za fedha.
Dar es Salaam. Huenda maumivu yatokanayo na tozo ya Serikali iliyowekwa kwenye miamala inayofanyika kwa njia ya simu yamepungua au kuzoeleka baada ya watumiaji wa huduma hizo kuongezeka kwa asilimia 3.4 ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
Ripoti mpya ya Takwimu za Mawasiliano ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 2022, kulikuwa na watumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu milioni 40.9 ukilinganisha na watumiaji milioni 39.5 waliokuwepo Septemba mwaka jana.
Hilo ni sawa na ongezeko la watumiaji milioni 1.4 ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
Tangu kuanza kwa utekelezaji wa tozo hiyo, watumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu wamekuwa wakiongezeka kinyume na matarajio ya baadhi ya watu waliodhani tozo zingepunguza watumiaji wake.
Mathalan, Oktoba mwaka jana kulikuwa na watumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu milioni 40.1 lakini wakaongezeka hadi milioni 40.3 mwezi uliofuata kabla hawajaongezeka zaidi hadi milioni 40.9 Desemba 2022.
Kwa mujibu wa TCRA, kuongezeka huko kwa watumiaji wa huduma za kifedha Desemba kulichangiwa na shughuli za sikukuu za mwisho wa mwaka jana.
Soma zaidi
“Miamala mingi imefanyika mwezi Disemba kuliko mwezi mwingine wowote ndani ya kipindi cha miezi mitatu kutokana na shughuli nyingi za mwisho wa mwaka ikiwemo sikukuu,” imesema ripoti hiyo ya TCRA.
Huduma za kifedha za kwenye simu zinasaidia kuongeza mzunguko wa fedha nchini na kutatua changamoto mbalimbali za kibenki ikiwemo kuweka fedha, kukopa na kulipia huduma na bidhaa mbalimbali.
Hata hivyo, watumiaji wa huduma hizo waliingia kwenye sintofahamu mara baada ya Serikali kupitisha tozo kwenye miamala ya simu jambo lililotishia baadhi ya watumiaji kuacha kutumia huduma hizo.
Sheria ya Tozo za Miamala ya Simu ya Kutuma na Kupokea kwa njia ya Kielektroniki ya mwaka 2021, ilianzisha tozo kwenye miamala ya fedha kwa njia ya simu kuanzia Julai 2021.
Kiwango cha tozo kilipunguzwa kwa asilimia 30 Septemba 2021 na kikapunguzwa tena Septemba 20, 2022 kwa asilimia 10 hadi asilimia 50 kwa kuzingatia makundi na gharama za miamala husika.
Huduma za kifedha hurahisisha kutuma fedha kwa ajili ya bishara familia na shughuli nyingine za kijamii.Picha | Daudi Mbapani.
Nini kinasababisha watumiaji kuongezeka
Dr Sylvester Jotta, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (Saut) na mchambuzi wa masuala ya uchumi anasema chanzo kikubwa cha kuongezeka kwa watumiaji wa huduma za kifedha ni urahisi wa kutumia huduma hizo.
“Watu wengi wanapenda kufanya mambo kwa urahisi mfano wafanya biashara wanapenda kufanya miamala kwa urahisi hapo hapo auze, atume pesa yake apate mzigo mwingine,” amesema mchambuzi huyo wa uchumi.
Hata hivyo, anasema idadi kubwa ya Watanzania bado hawana ufahamu wa kutosha wa viwango vya tozo vilivyowekwa hali inayofanya kufanya miamala kama kawaida.
“Watanzania wengi hawafahamu hata viwango vya makato na tozo zilizopo unakuta mtu anatoa na kupokea fedha akiwa hajui chochote kwa hiyo unakuta miamala inaendelea kama kawaida,” amesema Dk Jotta.
Mchambuzi huyo anasema ni vyema Tanzania kuiga mfano wa nchi nyingine zilizoweka mabango ya kuonyesha viwango vya tozo unazokatwa wakati wa kutuma na kupokea pesa.
“Hapa Tanzania wanapenda kufanya mambo kwa kificho kificho naiomba Serikali na mamlaka husika iweke mambo wazi watu wajue,” ameongeza Dk Jotta.