Tozo miamala ya simu bado “pasua kichwa”
- Utafiti wasema zaidi ya nusu ya wananchi wazipinga.
- Asilimia 63 ya wananchi wako tayari kulipa tozo kama wanaweza kufuatilia matumizi yake.
Dar es Salaam. Licha ya wananchi wengi wa Tanzania kufahamu kuhusu mabadiliko ya hivi karibuni ya kodi na tozo kwenye huduma za fedha kwa njia ya simu, zaidi ya nusu hawaungi mkono mabadiliko hayo, utafiti mpya umeeleza.
Sheria ya Tozo za Miamala ya Simu ya Kutuma na Kupokea kwa njia ya Kielektroniki ya mwaka 2021, ilianzisha tozo kwenye miamala ya pesa kwa simu kuanzia Julai mwaka jana.
Kiwango cha tozo kilipunguzwa kwa asilimia 30 mwezi Septemba 2021 na kikapunguzwa tena Julai mwaka huu na hivyo kufanya punguzo la jumla la asilimia 60 ya kiwango cha kilichowekwa awali.
Ripoti ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza kati ya Juni na Julai 2022 uliolenga kukusanya maoni ya wananchi kuhusu hali ya uchumi wa Taifa, na tozo za miamala ya fedha kupitia simu za mkononi inaelezwa kuwa wananchi nane kati ya 10 (asilimia 80) wanafahamu kuwa kodi na tozo za huduma za fedha kwa njia ya simu ziliongezwa mwaka 2021.
Pia ripoti hiyo inaeleza kuwa zaidi ya nusu (asilimia 55) wanafahamu kuwa tozo hizo zilipunguzwa baadaye.
Licha ya ufahamu huo kuhusu tozo za miamala ya simu, zaidi ya nusu au asilimia 57 ya wananchi hawakubaliani na tozo hizo tangu kuanzishwa kwake mwaka jana.
“Wananchi walio wengi hawakubaliani (asilimia 23) au hawakubaliani kabisa (asilimia 34) na tozo tangu ilipoanzishwa mara ya kwanza,” imeeleza ripoti hiyo ya Twaweza iliyotolewa leo Agosti 25, 2022.
Hata hivyo, walipoulizwa katika utafiti huo uliopewa jina la Sauti za Wananchi awamu ya saba, maoni yao kuhusu kupunguzwa kwa kiwango cha tozo, bado wananchi wengi zaidi hawakubaliani (asilimia 32) kuliko kukubaliana kwa asilimia 18 na mabadiliko hayo.
Utafiti huo ulikusanya maoni ya watu 3,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini ambapo kati yao watu 960 walipinga mabadiliko ya tozo hizo licha ya kupunguzwa huku watu 540 ambao ni sawa na asilimia 18 walikubaliana na mabadiliko ya tozo hizo.
“Miongoni mwa wale wanaokubali kwamba tozo hiyo ni njia muhimu ya kuongeza mapato kwa Serikali asilimia 26 kati yao wanasema viwango vya kodi hiyo ni kubwa” inaeleza ripoti hiyo.
Soma zaidi:
Sababu za kupinga tozo hizo
Utafiti huo pia umeweka wazi sababu za baadhi ya wananchi kupinga kuanzishwa kwa tozo hiyo ikiwemo kutokufahamu matumizi ya fedha zinazopatikana kupitia tozo hiyo.
“Asilimia 63 ya wananchi wako tayari kulipa tozo kama wanaweza kufuatilia matumizi yake,” inasema ripoti hiyo.
Sambamba na hilo wananchi 1,980 walioshiriki katika utafiti huo hawajui fedha za tozo zinapoenda, huku wengine 1,560 wakisema tozo sio tatizo, bali ni gharama za miamala zinzotozwa na watoa huduma huku wengine wakitaka tozo ziwekwe kwenye miamala mikubwa.
Mkurugenzi Mtendaji kutoka shirika la Equality For Growth (EFG), Jane Magigita amesema kuanzishwa kwa tozo hizo kumechangia kuvuruga mfumo mzima wa mnyororo wa thamani wa vyakula vya kilimo ambapo muathirika mkubwa ni mwanamke.
“Wamama wengi hawaweki fedha kwenye simu wanashika mkononi wanafanya malipo kwa mkono risk (hatari) kubwa ipo kwa kinamama, usalama wa fedha yao umekuwa mdogo,” amesema Magigita.
Tangazo
Miamala ya kifedha kwa njia ya simu yapungua
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 44 ya wananchi waliohojiwa katika utafiti huo wameripoti kupunguza kutuma fedha kwa njia ya simu tangu Julai 2021 kuliko wale wanaoripoti kuongeza kutuma fedha kwa njia hiyo (asilimia 15).
“Idadi ya wanaopokea fedha kwa njia ya simu imepungua tangu Julai 2021 (46%) kuliko wale wanaoripoti kupokea zaidi (14%),” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze wakati akiwasilisha matokeo ya ripoti hiyo amesema wakazi wengi wa Mkoa wa Dar es Salaam wameripoti kupunguza kutuma/kutumia pesa kupitia huduma za fedha kwa njia ya simu kwa asilimia 71%.
“Hii ni fursa kwa makampuni ya simu na serikali kutoa taarifa kwa wananchi juu ya umuhimu wa tozo na nini kinafanyika kupitia hiyo fedha ya tozo,” amesema Eyakuze ambapo kumechangiwa na tozo iliyowekwa na Serikali.
Fedha za tozo zipelekwe wapi?
Licha ya baadhi ya watu kupinga tozo, wangependa kuona mapato ya tozo hizo yakielekezwa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo huku kipaumbele kikiwa huduma za jamii ikwemo afya kwa asilimia 57.
Kipaumbele kingine ambacho wananchi wangependa kuona fedha za tozo zinaelekezwa ni pamoja na elimu (asilimia 50) ujenzi wa barabara (asilimia 38), huduma za maji ( asilimia 33), umeme (asilimia 20), kilimo (asilimia 18) na mikopo kwa asilimia asilimia 17.
Latest



