Watoto wasiotunza wazazi wao kuchukuliwa hatua kisheria
- Yasema inaendelea kufanya tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Wazee kabla ya kutunga sheria.
Dar es Salaam. Serikali imesema itatunga sheria ya kuwaadhibu watoto wasiowatunza wazazi wao iwapo tathmini itaonesha kuna utekelezaji hafifu wa tamko la Sera ya Wazee ya Mwaka 2023 linalowataka familia, jamii na ndugu wa karibu kuwatunza wazee.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mwanaidi Ali Khamis leo Juni 18, 2025 bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Prof Patrick Ndakidemi aliyetaka kujua ni lini Serikali itatunga sheria itakayowataka watoto kuwatunza wazazi wao wanapozeeka.
Waziri Mwanaidi amesema Serikali itaendelea kuwalea na kuwatunza wazee ambao hawana makazi katika vituo maalumu 13 vilivyopo nchini huku wakiendelea kufanya tathmini ya Sera ya Wazee inayowataka watoto kuwajibika kuwatunza wazazi wao.
“Itakapoonekana kwamba sera hii haifanyi kazi vizuri, tutatunga sheria na kuileta hapa bungeni kuhakikisha wazee wanatunzwa na watoto wao na hatua kali zitachukuliwa kwa wale ambao wanadharau au kuto kuwajali wazee wao,” amebainisha Naibu Waziri Khamisi.
Kwa mujibu wa Sera ya Wazee ya Mwaka 2023, toleo la 2024, suala la matunzo kwa wazee katika jamii ni jukumu la familia, jamii na ndugu wa karibu ambapo kama itabainika mzee hana ndugu wa kumtunza katika jamii basi Serikali huchukua jukumu hilo kupitia vituo vyake maalumu.
Katika kipindi cha 2015 hadi 2022, jumla ya wazee 2,135 walihifadhiwa kwenye makazi ya wazee, huku wazee 270 wakihudumiwa kila mwaka katika makazi ya Serikali, na 268 katika makazi yanayoendeshwa na mashirika binafsi.
Takwimu za Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa idadi ya wazee Tanzania Bara ilifikia 3,406,464 ambapo wanaume 1,546,221 na wanawake 1,860,243, kutoka idadi ya 2,507,568 iliyorekodiwa mwaka 2012 jambo linaloibua hoja ya uhitaji wa mifumo madhubuti ya matunzo kwa wazee.
Aidha, Katika utekelezaji wa Sera ya Wazee ya 2023, Serikali imeainisha maeneo 15 ya kipaumbele, yakiwemo huduma za afya, matunzo ya wazee, ushirikishwaji katika shughuli za maendeleo, hifadhi ya jamii, na uelimishaji kuhusu maisha ya uzeeni.Hadi kufikia Juni 2023, Serikali ilikuwa imeshawatambua wazee 2,203,414 kwa ajili ya huduma mbalimbali ikiwemo kutoa vitambulisho vya matibabu bure kwa wazee 1,256,544.
Latest



