‘Apps’ zinazoweza kuwasaidia wazazi katika malezi ya watoto

August 22, 2019 6:04 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Programu hizo za simu ni zile zinazotumika Tanzania na lugha ya Kiswahili. 
  • Zinawasaidia wazazi na watoto katika malezi na kupata elimu bora.

Dar es Salaam. Teknolojia inakua kwa kasi na kubadilisha namna ambavyo watoto hujifunza, kucheza, na kufanya mambo yao. 

Tofauti na zamani ambapo watoto walikua wanajifunza zaidi kwa wazazi wao na watu wanaowazunguka. Sasa teknolojia inawapa kila kitu, jambo linalotoa fursa kwa wabunifu kubuni programu za simu (Apps) zinazowasaidia watoto kupata maarifa na kupata mweleko mzuri wa maisha. 

Kwa Tanzania huwezi kuzitaja Apps za watoto bila kuitaja Ubongo Kids lakini zipo zaidi hiyo ambazo zikitumiwa vizuri chini ya uangalizi wa wazazi zinaweza kuwa na mchango mkubwa katika malezi ya watoto. 

Baadhi ya programu hizo ni zile zinazogusa sekta ya elimu, fasheni na masuala ya imani (dini): 

Hesabu za panya

App hii inayowasaidia watoto katika swala zima la elimu ili kuwafunza somo la hesabu na namna nzuri ya kuchezea namba.

Programu hii iko chini ya App mama ya watoto ya Ubongo Kids iliyoanzishwa na mwanamama Nisha Ligon inayohusisha vipindi tofauti vya watoto katika televisheni na mtandaoni.

Programu hii inaendeshwa na timu nzima ya Ubongo inayowalenga moja kwa moja watoto wa kitanzania kwa kutumia ya lugha ya Kiswahili. 

Programu hii imepata muitikio mzuri kwani imeweza kufikia watoto wengi mpaka nje ya Tanzania na kulazimika kuongeza lugha nyingine ya Kiingereza ili kuwafikia watoto wengi zaidi.


Soma zaidi: 


Herufi na Akili

Hii ni programu nyingine iliyopo pia chini ya Ubongo Kids ikiwa na lengo la kuwafundisha watoto namna ya kupanga herufi na somo la mwandiko kama moja ya kiini cha kusaidia watoto katika kujifunza na kukua kiakili.

African kids Fashion

Hii ni programu nyingine ya mitindo na fasheni za watoto. Inaonyesha na kuelekeza nguo mbalimbali zinazowafaa watoto ili kuwafanya wapendeze kwa muonekano wa aina mbalimbali ya mavazi. 

Kwa mzazi unayependa mtoto wako apendeze na kuonekana vizuri, basi app hii itakusaidia.

Muonekano mzuri wa mavazi ya watoto ni njia pekee ya kuwajali. Picha|Mtandao.

Hadithi za bibilia 

Hii ni programu nyingine iliyojikita kidini zaidi ambapo huwasaidia watoto katika makuzi ya kiimani  na kujua mambo mbalimbali yanayoweza kuwafahamisha misingi mbalimbali ya malezi.

Inawapatia hadithi mbalimbali zilizopo katika kitabu hicho kitakatifu za watoto wa zamani na jinsi walivyokua katika misingi ya hekima na hata kufikia ndoto za maisha yao.  Inawalenga watoto wa miaka 6 hadi 8. 

Mbali na programu tumishi za simu zinazoweza kuwasaidia watoto, pia kuna tovuti zenye maudhui ya watoto. 

Moja ya tovuti hiyo ni pamoja na “Kid’s health” tovuti inayohusisha malezi ya mtoto kuanzia kuzaliwa kwake mpaka anapofikisha umri wa miaka 18 ambapo anakua na uwezo wa kuchambua mambo. 

Inawasaidia watoto kujua mambo yanayowahusu kama ukuaji wa mwili, jinsi ya kutekeleza majukumu ya shuleni na namna bora ya kukua kiakili. 

Pia wazazi na walimu wanaweza kuitumia katika kupata miongozo ya kuwasaidia watoto katika shughuli za ufundishaji na malezi. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW