Rais Samia: Wazazi timizeni wajibu wenu wa malezi
- Awataka wazazi kulea watoto wao kikamilifu na kuacha kuilaumu Serikali.
- Ni kutokana na kuwepo kwa msukumo wa kulazimisha baadhi ya tamaduni za kigeni ambazo ni mbaya.
- Awataka Watanzania kusheherekea Eid kwa umakini ili wasisababishe majonzi.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi nchini kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wao ili kuhakikisha wanakua katika misingi ya maadili mema, mila na desturi za Kitanzania.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika Baraza la Eid al-Fitr leo Aprili 22, 2023 jijini Dar es salaam, amebainisha kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakiilaumu Serikali pale watoto wao wanapomomonyoka kimaadili ili hali wao hawakutimiza wajibu wao vile inavyotakiwa.
“Vizazi vyetu vunapotea, na vinapopotea lawama zote ni kwa Serikali, huyo Serikali ni nani? Kama ni mimi sitaweza kulea watoto wote Tanzania….
“Kila mzazi kile ulichokitoa tumboni nenda kakidhibiti, kina mama wenzangu twendeni tukadhibiti malezi, taasisi ya kwanza ya kuchunga maadili ni familia,” amesema Rais Samia akihutubia ndani ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere (JNICC).
Kwa mujibu wa Rais Samia, kumekuwepo na msukumo wa kulazimisha baadhi ya tamaduni za mataifa ya magharibi ambazo zina madhara kwa vijana na watoto wa Kitanzania.
Kutokana na hilo viongozi wakuu wa kiserikali pamoja na viongozi wa taasisi za dini wakiwemo Maaskofu na Masheikh wamekuwa wakijitokeza hadharani kukemea vitendo hivyo..
Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally ametoa rai kwa Watanzania kutunza tamaduni zao kwani mtu anayezikataa tamaduni na kuiga za watu wengine ni mtu ‘jahili’ ambaye hatoweza kutumika kuleta matokeo chanya kwa jamii yake.
Rais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dk Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally mara baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuhudhuria Baraza la Eid El-Fitr Aprili, 22 2023. Wengine katika picha ni Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Walid Alhad Omar pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Mama Shamim Khan.
Watumiaji wa barabara wakumbushwa umakini
Rais Samia amewaasa watumiaji wa barabara hususani madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali ambazo zimekuwa chanzo cha vifo pamoja na majeruhi.
“Mwenyezi Mungu atujaalie sikukuu njema pamoja na sisi wenyewe kuwa waangalifu ili tusisababishe kero na ajali tukaleta huzuni badala ya furaha..
“Madereva wetu, vijana wetu wale wanaopiga vitu halafu wakaingia barabarani warudi kwa Mungu wao, kama Rais natoa salamu za rambirambi hadi nachoka,” amesema Rais Samia wakati akihitimisha hotuba yake.
Swala ya Eid El Fitri kwa mwaka 2023 imeswaliwa katika msikiti wa Mfalme Mohammed VI uliopo makao makuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Kinondoni jijini Dar es salaam, na kufuatiwa na Maulid iliyofanyika katika ukumbi wa JNICC.