Serikali kuzindua sera mpya ya elimu na mafunzo Januari 31
- Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
- Uzinduzi huo utachochea maboresho katika sekta ya elimu nchini.
Arusha. Serikali ya Tanzania imesema itazindua sera mpya ya elimu na mafunzo Januari 31,2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dodoma ili kuendelea kuimarisha sekta hiyo muhimu nchini.
Sera hiyo iliyopewa jina Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 toleo la 2023 ni miongoni mwa maboresho makubwa yaliyowahi kufanyika katika sekta ya elimu nchini ikilenga utolewaji wa elimu inayoendana na mahitaji yaliyopo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda aliyekuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo Januari 10, 2025 amesema kuwa sera hiyo italeta mageuzi makubwa katika elimu huku utekelezaji wake ukitarajiwa kuchukua muda.
“Mageuzi yaliyopo kwenye sera ni makubwa sana ni mabadiliko yatakayogusa vizazi na vizazi, ukamilifu wa utekelezaji wake kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha sita utachukua muda,” amesema Prof Mkenda.
Kwa mujibu wa Mkenda uandaaji wa sera hiyo uliochukua miaka mitatu ulishirikisha makundi mbalimbali ikiwemo wanafunzi, walimu, wananchi na wadau wa sekta ya elimu ambao walitoa maoni yao kupitia njia zilizoanishwa na wizara hiyo.
Mpaka sasa tayari sera hiyo imeshaanza kutekelezwa kwa awamu mbalimbali ikileta mabadiliko katika mfumo wa elimu ya awali, amali, shule ya msingi na sekondari, ikiwa ni baada ya kusainiwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Prof. Mkenda amesema kuwa sera hiyo imebeba majibu ya maswali ya Watanzania yanayohusu masuala mbalimbali ya muhimu ikiwemo matumizi ya lugha ya kiingereza shuleni.
“Tunasikia bado kuna watu wanatoa michango kuhusu mabadiliko ya elimu…yapo majibu karibia ya hoja zote katika sera na mitaala mipya kwa mfano mjadala mkubwa unaoendelea hapa nchini ni kuhusu lugha ya kiingereza, ukienda kwenye sera utaona suala la lugha ukienda kwenye mitaala utaona suala la lugha,” amesema Mkenda.
Mbali na suala hilo Mkenda amesema kuwa maswali mengine katika mada za akili mnemba, masomo ya sayansi, teknolojia na hesabu (Stem) pamoja na kumuandaa mwanafunzi kuwa na ujuzi unaohitajika kwenye dunia ya sasa yote yameainishwa katika sera na mitaala hiyo.
Katika hatua nyingine Mkenda amewataka wananchi kufuatilia matangazo ya moja kwa moja ya uzinduzi huo kupitia vyombo vya habari na wale watakaoweza kufika kujiandikisha mapema ili waweze kuwa sehemu ya uzinduzi huo.