Watanzania waliong’ara kitaifa, kimataifa 2023

January 2, 2024 12:45 pm · Daudi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na Ramadhan Brothers pamoja na Dk. Tulia Ackson.
  • Ubunifu, bahati, na matokeo ya kazi zao kwa jamii ndiyo umewaibua.

Dar es Salaam. Mwaka 2023, umeshuhudia Watanzania kadhaa waking’ara kitaifa na kimataifa kupitia shughuli zao wanazozifanya jambo lililowafanya watambulike zaidi.

Nukta Habari, imekuandalia orodha ya Watanzania waliong’ara mwaka 2023 katika nyanja mbalimbali ikiwemo uongozi na siasa, sanaa, michezo na kijamii.

1. Rais Samia Suluhu Hassan

Rais Samia Suluhu Hassan sasa anatimiza zaidi ya siku 1,000 tangu aingie madarakani Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Pombe Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.

Mwaka 2023, amekuwa miongoni mwa Watanzania waliong’ara kitaifa na kimataifa jambo lililosababisha atambuliwe katika orodha za watu mashuhuri pamoja na kutunukiwa Shahada za Heshima za Uzamivu.

Oktoba 10, 2023, Rais Samia alitunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa (Doctorate Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru Nchini India kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya Watu nchini Tanzania.

Rais Samia akihutubia mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu ya Utalii na Usimamizi wa Masoko. Picha l Ikulu 

Aidha, Disemba 28, 2023 Chuo Kikuu Cha Zanzibar (Suza) kilimtunuku Rais Samia Shahada ya Heshima ya Utalii na Usimamizi wa Masoko huku mchango wake kwenye utatuzi wa changamoto zinazoikabili jamii ukitajwa kama sababu.

Makamu wa Rais wa Suza Dk. Hashim Hamza Chande aliyekuwa akizungumza katika hafla ya mahafali ya 19 ya chuo hicho aliwaambia wahudhuriaji kuwa Rais Samia ametunukiwa shahada hiyo kutokana na mchango wake wa kuchechemua uchumi kupitia sekta ya utalii pamoja na mageuzi makubwa aliyofanya katika elimu.


Soma zaidi : Fahamu sababu za Rais Samia kutunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu


2. The Ramadhani brothers

Hili ni kundi la vijana wawili ambao wameipeperusha vema bendera ya Tanzania  kupitia vipaji vyao kwenye mchezo wa kuruka sarakasi.

Majina yao ni Fadhili Ramadhani na Ibrahim Jobu, ndugu  ambao waliupenda mchezo huu tangu wakiwa wadogo chini ya mkufunzi wao Winston Ruddle maarufu  kama Papa Afrika ambaye amekua akiwapa mafunzo mbalimbali kwa muda takriban miaka 20 sasa.

Mpaka sasa wamefanikiwa kufahamika ulimwengu mzima kwa kuonesha sanaa yao katika majukwaa mbalimbali ambapo kwa mwaka 2023 umekuwa bora zaidi kwa kuwa wamefanya maonesho katika majukwaa makubwa zaidi ikiwemo la kusaka vipaji nchini Marekani (American Got Talent) ambapo waliishia nusu fainali.

Hatua hiyo ilisababisha Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kupitia Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) kutoa pongezi kwao kutokana na kuliwakilisha Taifa vyema katika maeneo mbalimbali.

Ramadhani Brothers waling’ara pia katika majukwaa mengine ikiwemo Australia Got Talent ya Australia walikopata hati ya dhahabu (golden buzzer) na kuwafanya kuwa kundi la kwanza kupata hati hiyo mfululizo kwenye mashindano yote walioshiriki ikiwa ni pamoja na France got talent ya Ufaransa pamoja na Romania got talent ya nchini Romania.

3. Paul Makonda

Oktoba 22, 2023, jina la Paul Makonda lilitikisa vichwa vingi vya habari sambamba na mitandao ya kijamii baada ya kutangazwa uteuzi wake wa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akirithi mikoba ya Sophia Mjema.

Paul Makonda alishawahi kujizolea umaarufu kwenye anga za siasa kupitia CCM, akihudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo ukuu wa Wilaya ya Kinondoni pamoja na ukuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nafasi aliyoiachia mwaka 2020 baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo kwa miaka minne.

Akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda atakumbukwa kwa matamko yake mbalimbali yaliyoibua hisia tofauti kwa Watanzania, ikiwemo kuwataja hadharani watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya.


Soma zaidi : Spika Tulia ashinda urais Umoja wa Mabunge Duniani.


4. Tulia Ackson Mwansasu

Nyota ya Tulia Ackson Mwansasu imeendelea kung’ara zaidi mwaka 2023, mara baada ya Februali, Mosi 2022 kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Tanzania na Oktoba 27, 2023 ameng’ara kimataifa zaidi mara baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

Dk. Tulia anakuwa Spika wa 31 wa IPU akipokea kijiti cha Duarte Pacheco, Spika wa Bunge la Ureno, ambapo amekamilisha utawala wake katika mkutano wa 147 uliofanyika Angola.

Kwa mujibu wa IPU, Dk. Tulia ambaye ni Mbunge wa Mbeya Mjini anakuwa mwanamke wa tatu kuongoza umoja huo, akitanguliwa na Najma Heptulla wa India aliyeongoza kati ya 1999 na 2002 na Gabriela Cuevas wa Mexico aliyeongoza kuanzia 2017 hadi 2020.

Hata hivyo, Tulia anakuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kuwa rais wa IPU ambaye atashikilia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kwa muda wa miaka 25 iliyopita urais wa IPU, umekuwa ukizunguka katika nchi za Misri, Hispania, India, Chile, Italia, Namibia, Morocco, Bangladesh, Mexico na Ureno.

5. Jokate Mwegelo

Huenda Oktoba Mosi, 2023 ikawa siku isiyosahaulika kwa Jokate Mwegelo kwa kuwa ndiyo siku ambayo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilimteua kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake akitokea kuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga.

Jokate mwenye umri wa miaka 36 hivi sasa, anaingia katika orodha ya Watanzania waliong’ara kwa kuwa ni nadra nafasi hiyo nyeti katika jumuiya hiyo ya CCM kukaliwa na kijana wa kariba yake.

Safari ya Jokate katika uongozi ilianza mwaka 2018 baada ya kuteuliwa na Rais wa awamu ya tano wa Tanzania John Pombe Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, ambapo baadae alihamishiwa katika wilaya ya Temeke na Korogwe.

6. Hersi Said

Kwa wadau wa michezo nchini Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, jina hilo si geni machoni na masikioni mwao, akihudumu kama rais wa klabu ya mpira wa miguu nchini Tanzania, Young Africans.

Mwaka 2023, umekuwa wa neema zaidi kwake na klabu yake, pamoja na kufanikiwa kuvaa medali ya mshindi wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika Hersi ndiye Mtanzania wa kwanza kushika nafasi ya urais wa Chama cha Klabu Africa (ACA).

Miongoni mwa majukumu ya Hersi katika nafasi hiyo ni pamoja na kuhakikisha ACA inakuwa na programu za mafunzo ya uongozi, uongozi wa shule za soka, utafutaji masoko, usimamizi wa fedha na zaidi ya yote kuhamasisha ujenzi wa miundombinu ya soka, hasa viwanja vya mechi na mazoezi.

Kung’ara kwa Hersi ni dalili za soka la Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki kukua, ikitazamiwa kuleta ushindani kwa mataifa ya Afrika Kaskazini na Magharibi mwa Afrika yanayofanya vizuri kwa muda mrefu.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV