Sababu Rais Samia kutunukiwa PhD

November 30, 2022 2:16 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link

Rais Dk Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na wahitimu mbalimbali wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Mahafali ya 52ya Duru ya Tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City. Picha | Ikulu.


  • Atunukiwa tuzo hiyo miezi 11 baada ya kutamani kujiendeleza kimasomo.
  • Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lasema amestahili hupata shahada hiyo.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan  ametunukiwa shahada ya juu ya  udaktari  wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kutokana na mabadiliko makubwa ya maendeleo tangu alipoingia madarakani Machi 2021.

Rais Samia ametunukiwa udaktari huo  leo Novemba 30, 2022 na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Jakaya Kikwete kwenye mahafali ya 52 ya Chuo hicho  yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Milmani City uliopo  jijini Dar es Salaam.

“Kwa mamlaka niliyokabidhiwa, ninakutunuku digrii ya heshima ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hongera sana,” amesema Rais mstaafu Kikwete akimtunuku Rais Samia udaktari huo.

Akizungumza mara baada ya kutunikiwa shahada hiyo Rais Samia ameushukuru uongozi wa UDSM kwa kutambua na kuona mchango wake anaoufanya ndani ya nchi ya Tanzania huku akikiri kujaribu kuitafuta shahada hiyo lakini muda haukumpa nafasi.

“Suala la kupewa tuzo hii nimelipokea kwa unyenyekevu mkubwa, nilijiuliza maswali kadhaa sababu huko nyuma nilijaribu kuitafuta shahada hii lakini muda haukunipa nafasi,” amesema Rais Samia.

Miezi 11 iliyopita kiongozi hiyo mkuu wa nchi alisema alitamani kujiendeleza kimasomo lakini majukumu yalimzuia lakini tukio la leo limekamilisha ndoto yake ya kuwa daktari wa heshima

Maazimio ya senenti ya Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kikao chake cha 875 yalimpendekeza Rais Samia kutunukiwa shahada hiyo kutokana na mabadiliko makubwa yaliyoletwa na uongozi wake.

Kwa upande wa sekta ya uchumi baraza hilo limetambua juhudi zake katika kuimarisha kilimo na ufugaji, teknolojia, mawasiliano na nishati. Pia Upatikanaji wa fedha za msaada na mikopo nafuu iliyowezesha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kutolewa huduma za kijamii ikiwemo maji.

Sambamba na hayo uamuzi wake wa kuboresha  mpango wa sekta ya  kilimo nchini wenye lengo la kutatua changamoto mbalimbali na kuongeza mazao ya chakula na biashara

Katika sekta ya utalii, jitihada za Rais Samia zimeonekena katikakuongeza watalii nchini kupitia filamu ya Royal Tour ambapo kufikia Juni 2022 ambapo kumekuwa na ongezeko la asilimia 34 ya watalii.


Soma zaidi:


Marais waliowahi kupata udaktari wa heshima

Rais Samia anakuwa miongoni mwa marais wastaafu wa Tanzania waliowahi kupata shahada ya juu ya udaktari wa heshima.

Marais hao ni pamoja na Dk Ali Hassan Mwinyi aliyepata shahada ya juu ya udaktari wa heshima mwaka 2012 kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania(OUT) na Hayati Rais Dk Benjamin Mkapa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania aliyetunukiwa na Chuo Kikuu cha Cape Cost nchini Ghana.

Dk Jakaya Kikwete, Rais wa awamu ya nne alitunukiwa tuzo hiyo ya heshima mwaka 2010 na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na mwaka 2015 alitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PHD) ya Heshima ya Sheria (Degree of Doctors of Laws honoriscausa – honorarary LLD) katika Chuo Kikuu cha Newcastle cha nchini Australia.

Hayati Dk John Magufuli aliyefariki Machi 2021 akiwa madarakani alitunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mwaka 2019.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...