Rais Samia aelekeza Shahada ya Udaktari wa Heshima kwa wasichana Tanzania

October 10, 2023 7:17 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Awataka kuweka bidii na kujituma kukabiliana na vikwazo.
  • Ni Rais wa kwanza kutoka barani Afrika kutunukiwa shahada hiyo.
  • Wengine waliowahi kutunukiwa ni Rais wa Urusi Vladimir Putin na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa (Doctorate Honoris Causa) na Chuo Kikuu Cha Jawaharlal Nehru nchini India ambapo ameielekeza kwa wasichana waishio katika maeneo ya vijijini Tanzania.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza mara baada ya kutunukiwa shahada hiyo Leo Oktoba 10, 2023 amewaambia viongozi pamoja na wageni walioshiriki hafla hiyo kuwa anaielekeza shahada hiyo kwa wasichana wa Tanzania huku akiwataka kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kuvishinda vikwazo vitakavyojiinua.

“Shahada hii naielekeza kwa wasichana waishio katika mazingira ya vijijini, nataka wafahamu kuwa ni kwa kujituma na bidii, wanaweza kukabiliana na vikwazo vyote vinavyojitokeza,” amesema Rais Samia jijini New Delhi.


Soma zaidi : Rais Samia: Tanzania, India, kufungua ushirikiano maeneo ya kimkakati


Rais Samia amejitolea mfano yeye kama miongoni mwa wasichana waliotokea familia za kawaida kisiwani Unguja, lakini kujituma na kujifunza kwa bidii ni miongoni mwa mambo yaliyochangia yeye kushika wadhifa huo wa juu kabisa katika nchi.

Shahada hiyo aliyotunukiwa Rais Samia na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru Profesa Santishree Dhulipudi Pandit ni ya kwanza kutunukiwa na chuo cha nje ya Tanzania na ya pili kwa Rais Samia ikitanguliwa na ile aliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kwa mujibu wa Profesa Pandit chuo hicho kimemtunuku Rais Samia shahada hiyo ya heshima kutokana na mchango wake kwenye kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na India na mafanikio ya Rais Samia kwenye kuimarisha diplomasia ya uchumi.

Rais Samia ni mwanamke wa kwanza kutunukiwa shahada hiyo kutoka barani Afrika ambapo ni viongozi wawili tu ambao wametunukiwa shahada hiyo duniani  akiwemo Rais wa Urusi Vladimir Putin pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Hayati Shinzo Abe.

 Kifahamu Chuo Kikuu Jawaharlar Nehru 

Ni miongoni mwa vyuo vikongwe na maarufu ulimwenguni ambacho kimekuwepo kwa zaidi ya miongo mitano tangu kuanzishwa kwake mwaka 1969 ambapo asili ya jina lake ni aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa taifa hilo kubwa barani Asia Jawaharlal Nehru ambaye alifariki mwaka 1964.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW