Rais Samia aeleza kilichomshawishi kuingia katika siasa za ushindani
- Ni kuyajua vizuri matatizo ya wananchi na kutaka kuyasemea.
- Aeleza jina la “Bibi Mchele” lilivyompa umaarufu kwa wananchi.
- Leo Januari 27, 2022 atimiza miaka 62.
Dar es Salaam. Wakati Rais Samia Suluhu akiadhimisha kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa amesema kufanya kazi kwa karibu na wananchi ndiyo kulimfanya aingie kwenye ulingo wa siasa ili kuwasemea na kuwapambania changamoto zao.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Januari 27, 2021 Ikulu jijini Dodoma katika hafla ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa amesema alivutiwa na siasa za hoja hasa katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar , hivyo akaona vyema aingie katika shughuli za kisiasa huku akiwa na lengo kuwawakilisha wananchi kikamilifu.
“Mwaka 2000 ndiyo nilipata mawazo ya kuingia kwenye siasa, ukiniuliza kwanini nilikuwa na sababu moja tu, nilikuwa naangalia Baraza la Wawakilishi linavyoendelea, wakati ule upinzania ulikuwa ndiyo unapamba moto kwa hiyo nikaamua kuingia ili nami niingie kwenye upambanaji,” amesema.
Amesema wakati huo yuko nje ya siasa alikuwa akizijua kwa undani changamoto za wananchi kutokana na uzoefu wake wa kufanya kazi na mashirika mbalimbali likiwemo la Shirika la Chakula Duniani (WFP).
“Niliamua kuingia niisimamie Serikali na kujibu hoja kwa sababu nilishafanya kazi na wananchi kupitia NGOs kwa hiyo changamoto zote nazijua, sasa unakuta waziri anaulizwa anachojibu ni tofauti na kililichoko kwa wananchi ndiyo nikaamua niingie kujibu hoja au kupeleka hoja za wananchi,” amesisitiza Rais.
Rais Samia Suluhu Hassan akikata keki kama ishara ya kusherehekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa leo tarehe 27 Januari, 2022 Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma. Mwaka huu, Rais Samia ametimiza miaka 62. Picha| Ikulu.
Rais Samia ambaye ametimiza miaka 62 amesema kilichomfanya kukubalika katika uwanja wa siasa na kwa mara ya kwanza kuchaguliwa kuwa mbunge wa viti maalumu ni jina la Bibi Mchele ambalo alikuwa akijulikana zaidi kwa wananchi wakati akifanya kazi WFP.
“Nilikuwa sijui mtu anaingiaje, nikauliza nikafahamishwa nikajaribu, nikaenda Kusini ya Unguja nikajitambulisha wengi walikuwa wananijua Bibi Mchele kwa sababu wakati nafanya kazi Shirika la Chakula Duniani (WFP) kulikuwa na tatizo la wadudu kuvamia mazao, kwa hiyo kukawa na uhaba wa chakula lakini kwa sababu niko kule nikafanya jitihada za kuomba chakula kwa ajili ya wananchi,” amesema na kubainisha kuwa,
“Tukapata mchele, samaki na mafuta ya kupikia kwa wingi tukagawa kwa wananchi, kwa hiyo wakanipa jina la bibi mchele, nilipokwenda kujitambulisha wakawa wanasema bibi mchele tunampa, kwa hiyo nikaibuka kuwa mshindi kwenye viti vya wanawake ndiyo nilipenyea huko.”
Samia ambaye ni rais wa kwanza mwanamke Tanzania amesema baada ya hapo siasa ilimkubali na akaendelea kupanda katika ngazi za kisiasa na vyombo vya maamuzi hadi kuteuliwa kuwa rais Machi 17, 2021 baada ya kifo cha Rais Dk John Magufuli.
Soma zaidi:
- Rasmi: Samia Suluhu Hassan aapishwa kuwa Rais wa Tanzania
- Huyu ndiye Samia Suluhu Hassan, Rais mwanamke wa kwanza Tanzania
Mipango yake ya kujielimisha zaidi
Katika hatua nyingine Rais Samia mwenye shahada ya uzamili (masters) amesema alikuwa na mipango ya kusoma zaidi hadi ngazi ya shahada ya uzamivu (PhD) lakini kutokana na majukumu aliyonayo hawezi kutimiza kusudio hilo kwa sasa.
“Nilijaribu kufanya PhD lakini ukweli ni kwamba pilika ni nyingi nimeshindwa, sijui niseme nimeshindwa au nitaimalizia baadaye, sijui. Labda nitaimalizia baadaye,” amesema Rais Samia.
Katika kuitafuta elimu, amesema kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha nne amesoma shule takriban 10 kwa sababu baba yake alikuwa mwalimu hivyo alikuwa anahamishwa vituo vingi vya kazi.
Watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa wametoa salamu zao heri kwa Rais Samia kwa kutimiza miaka 62 huku wakimtakia uongozi mzuri katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Latest
