Wanafunzi zaidi ya 70 wanusurika kifo, bweni la shule likiteketea kwa moto

June 30, 2022 11:27 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Mabaki ya vifaa vya bweni la Shule ya Sekondari ya Wavulana Bwiru iliyopo Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza lililoteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo Juni 30. Picha | Mariam John.


  • Ni bweni la Shule ya Sekondari ya Wavulana Bwiru iliyopo Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza.
  • Limeteketea kwa moto usiku wa kuamkia Juni 30, 2022.
  • Hakuna majeruhi wala kifo licha kuharibu mali zote za wanafunzi.

Mwanza. Zaidi ya wanafunzi 70 wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Bwiru iliyopo Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza wamenusurika kifo baada ya bweni walilokuwa wanalala kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo Juni 30. 

Wakizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) baadhi ya wanafunzi shuleni hapo wamesema moto huo ulianza wakati wakiwa darasani wakijisomea masomo ya jioni.

“Tulisikia kengere ya dharura ikipigwa na baada ya kukusanyika eneo la dharura tuliona bweni letu likiteketea kwa moto, bado hatujajua chanzo ni nini na tumeambiwa wanaendelea kufanya uchunguzi,” amesema Jamal Idd, mwanafunzi kidato cha kwanza shuleni hapo.

Zakaria Mkongo anasema pamoja na kwamba uchunguzi unaendelea lakini huenda moto huo umesababishwa na hitilafu ya umeme kwa kuwa ulikuwa unasumbua.

Kwa mujibu wa uongozi wa shule hakuna aliyejeruhiwa kutokana na moto huo ulioanza majira ya saa 3 usiku wakati wanafunzi wakiwa darasani huku vitu vyote vilivyokuwepo yakiwepo magodoro na vifaa vya wanafunzi vikiteketea kwa moto.


Zinazohusiana


Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Mwanza, Ambwene Mwakibete amesema walipokea wito wa tukio la moto na waliweza kufika shuleni hapo lakini walikuta bweni hilo linalotumiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza limeshateketea.

Amesema ndani ya bweni hilo kulikuwa na vitanda 37, nguo, magodoro na madaftari.

“Athari imekuwa kubwa kutokana na jengo hilo kuwa kuukuu ni la muda mrefu na ndiyo maana moto umeweza kushika kwa kasi na kuteketeza vitu vyote vilivyokuwemo ndani ya bweni na kwamba hakuna madhara yaliyotokea kwa wanafunzi kwa kuwa wakati moto unatokea wanafunzi walikuwa darasani wakijisomea,” amesema Kamishna Mwakibete.

Amesema uchunguzi wa tukio hilo umeanza mara moja kujua chanzo nini na kwamba anatoa rai kwa wazazi kuwa na subira wakati uchunguzi ukiendelea.

Shule hiyo ina mabweni 11 yanayotumiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita, ambapo mabweni mengine hayajaguswa na moto huo. 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel ametoa pole kwa wanafunzi hao na kuwataka kuwa watulivu. 

Ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Ilemela kuhakikisha bweni la wanafunzi hao linajengwa haraka na likamilike kwa muda mfupi ili wanafunzi waweze kupata sehemu ya kulala lakini pia vifaa vingine vilivyoteketea kama magodoro na vifaa vya shule vipatikane.

 “Niwatahadharishe wanafunzi kuwa  jengo hilo limepasuka hivyo  wasizunguke eneo hilo waache uchunguzi uendelee na wakati huo  Serikali itasimamia kuhakikisha vifaa vyao vyote  vinapatikana,” amesema Mhandisi Gabriel.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW