Mara itatoboa katika mtihani wa darasa saba 2019?

September 10, 2019 10:05 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mkoa huo umeshika nafasi ya mwisho kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara ikiwa ni tofauti kubwa ukilinganisha na matokeo ya mwaka jana ambapo ilishika nafasi ya 13. 
  • Pia umetoa wilaya mbili na shule moja zilizofanya vibaya kitaifa.
  • Baadhi ya watendaji wa sekta ya elimu katika mkoa huo wanatuhumiwa kuhusika na udanganyifu na wizi wa mitihani.
  • Mkoa kufanya tathmini ili kujinusuru na matokeo mabovu mwaka 2019.

Dar es Salaam. Kesho ni siku ambayo wanafunzi wa darasa la saba nchini kote, wanafanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE), ikiwa ni sehemu ya kupima uelewa wao katika kipindi chote walipokuwa shuleni. 

Pia mtihani huo ni daraja la kuwawezesha kwenda elimu ya sekondari ambapo kujiunga kwao hutegemea ufaulu wa mwanafunzi. 

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk Charles Msonde, wanafunzi 947,221 wa darasa la saba kutoka shule 17,051 za Tanzania bara wanatarajia kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa siku mbili mfululizo.

Katika matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa Oktoba 23, 2018 Jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonde, ufaulu uliongezeka kwa asilimia tano kutoka  asilimia 72.76 iliyorekodiwa mwaka 2017 huku Dar es Salaam ikiongoza kitaifa ikifuatiwa na Geita. 

Necta ilieleza kuwa wastani wa ufaulu kitaifa mwaka huu ni asilimia 77.12 ikiwa na maana kuwa kwa kila wanafunzi wanne waliofanya mtihani huo, watatu au zaidi ya robo tatu wamefaulu kuendelea na ngazi ya elimu ya sekondari. 

Watahiniwa 957,904 walisajiliwa kufanya mtihani huo ambapo kati yao 733,103 walifaulu mtihani huo.  Kati ya waliofaulu mtihani huo, ambao ulirudiwa katika baadhi ya maeneo baada ya kuvuja, wasichana walikuwa 382,830  na wavulana 350,273. 

Licha ya Dar es Salaam kufanikiwa kuingia katika 10 bora za mikoa iliyofanya vizuri na kuibua furaha kwa shule, wazazi na wanafunzi ambao wana uhakika wa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza, wenzao wa Mara walikuwa katika sintofahamu kwa sababu mkoa huo ulishika nafasi ya mwisho kitaifa. 

Hali hiyo huenda ikawaweka viongozi, watendaji na wazazi wa mkoa huo wa Kanda ya Ziwa katika tafakari ya kina kuhusu mstakabali wa elimu ya watoto wao . 

Mpangilio wa mikoa kwa ubora wa ufaulu katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) 2018 uliotolewa na NECTA unaonyesha kuwa Mara imeshika nafasi ya mwisho kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara ikiwa ikiporomoka kwa kasi kutoka nafasi ya 13 iliyorekodiwa mwaka jana. 

Mkoa huo ulikuwa na shule 797 na wanafunzi 58,033 waliosajiliwa kufanya mtihani huku ufaulu ukiwa ni asilimia 63.68 chini ya wastani wa kitaifa wa asilimia 77.12. 

Mara imeungana na mikoa mingine 10 iliyofanya vibaya kitaifa kama Kigoma, Lindi, Dodoma, Simiyu, Manyara, Tabora na Tanga ambayo katika matokeo ya mwaka jana ilikuwa katika nafasi nzuri ya ufaulu.

Wakati Mara ikijikongoja mkiani, baadhi ya halmashauri zake vimefanya vibaya pia na kuchangia mkoa huo kufanya vibaya kitaifa licha ya juhudi mbalimbali zinazofanyika na Serikali kutoa elimu bila malipo. 

Mathalani, mpangilio wa Halmashauri kwa ubora wa ufaulu katika mtihani PSLE 2018 unaonyesha Mara imeingiza Wilaya mbili za Butiama na Musoma Vijijini katika halmashauri 10 zilizofanya vibaya katika matokeo ya mtihani huo.

Halmashauri hizo zimeshika nafasi ya 183 na 184 kati ya 186 za Tanzania Bara zikiwa juu kidogo ya Meatu mkoani Simiyu na Nchemba (Dodoma).  Nchemba imekuwa ya mwisho kitaifa na wanafunzi wake wote walilazimika kurudia mtihani kwa sababu ya matukio ya wizi na udangajifu yaliyohusisha watendaji, walimu na wanafunzi.


Zinazohusiana:


Anguko la Mara katika matokeo hayo halikuishia ngazi ya Halmashauri limeshuka hadi katika ngazi ya chini ya shule ambapo imeingiza shule moja ya Magana miongoni mwa shule 10 zilizofanya vibaya kitaifa.

Magana ipo katika Wilaya ya Butiama ambapo Kiwilaya na Kimkoa imeshika nafasi ya mwisho na hata kitaifa matokeo yake sio mazuri ikiwakilisha shule zingine zilizofanya vibaya katika mkoa huo licha ya shule hizo kutokuwepo katika kundi la 10 za mwisho kitaifa.

Wakati viongozi wa Mara wakitafakari namna ya kujinusuru na matokeo mabovu katika mtihani wa 2019, watalazimika pia kupambana na jinamizi la udangajifu na wizi wa mitihani ambao umeikumba wilaya ya Rorya mkoani humo.

Sakata la wizi wa mitihani lilibainika katika kituo teule kilichopo katika Shule ya Msingi Nyanduga katika halmashauri hiyo ambacho kilitumika kutunza mitihani. 

Hata hivyo, Msonde amewatuhumu watendaji wasio waaminifu akiwemo Afisa Elimu Msingi, Zacharia Weibina na Thobias Ojijo ambaye alikuwa Afisa Elimu vifaa na takwimu walishirikiana na walimu kuchana bahasha za mitihani na kusambaza kwa njia ya WhatsApp katika baadhi ya shule za mkoa wa Dar es Salaam.  

“Baraza la Mitihani la Tanzania limeyafuta matokeo ya watahiniwa wote 357 (wakiwemo wa Rorya) waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi,” amesema Dk Msonde na kuongeza kuwa,

“Aidha Baraza limezishauri mamlaka kuwachukulia hatua wale wote waliohusika kwa namna moja au nyingine kutokea kwa udangajifu wa mitihani kwa mujibu wa kanuni za utumishi na sheria za nchi yetu.”

Maandalizi mazuri ni mbinu mojawapo ya kuwanusuru wanafunzi na matokeo mabovu. Picha| Ishi Kistaa.

Sababu za Mara kushika mkia 

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya elimu wameiambia Nukta kuwa watoto wanaoishi Kanda ya Ziwa wanakabiliwa na changamoto ya kukatisha masomo na kujiingiza katika shughuli za uchimbaji madini, uvuvi na kuchunga mifugo na wengine kuolewa katika umri mdogo jambo linalowafanya washindwe kuhudhuria masomo darasani.

Kwa mujibu wa Utafiti wa Kujipima kwa njia ya kujifunza Afrika unaoratibiwa na Chuo Kikuu cha Aga Khan kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Oxford cha nchini Uingereza umebaini kuwa kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi katika shule za msingi kunasababisha na kutokuwepo kwa mahusiano mazuri kati ya walimu na wanafunzi.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima ameiambia Nukta kuwa kwa sasa hawezi kuzungumzia sababu za mkoa wake kushika nafasi ya mwisho kitaifa mpaka akutane na watendaji wa elimu watakaotoa tathmini ya mwenendo na matokeo mabovu ya mtihani wa darasa la saba mkoani humo.

“Niko nje ya mkoa nikifika mkoani nitafuatilia nijue sababu ni nini. Nitakaa na Afisa elimu anieleze,” amesema Malima.

Amebainisha kuwa baada ya kupata majibu na kufanya tathmini ndipo wataweza kupanga mikakati ya kuunusuru mkoa huo na matokeo mabovu ya mwaka ujao wa 2019. 

Swali lililobaki, mwaka huu Mara itatoboa na kutoka katika nafasi ya mwisho kitaifa na hata kuingia 10 bora au ndiyo itaendelea kung’ang’ania mkiani?

(Habari hii imeboreshwa leo Septemba 10, 2018)

Enable Notifications OK No thanks