Wakimbizi 200,000 hatarini kukumbwa na upungufu wa chakula Tanzania

June 20, 2023 1:34 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutokana na WFP kukumbwa na ukata na kuanza kutoa asilimia 50 tu mahitaji ya chakula kwa wakimbizi.
  • Bilioni 49.6 zinahitajika ili kutatua uhaba huo wa chakula kwa wakimbizi.

Dar es Salaam. Huenda zaidi ya wakimbizi 200,000 waishio nchini Tanzania wakakabiliana na changamoto ya upatikanaji wa chakula hivi karibuni baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani (WFP) kukumbwa na ukata.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo Mei 30, 2023 inasema wamepunguza utoaji wa chakula hadi asilimia 50 kutokana na kuchelewa kwa misaada waliyokuwa wanapokea awali. 

Kwa mujibu wa WFP kila mkimbizi anatakiwa kupata mlo wa siku wenye kiwango cha chini pendekezwa cha lishe chenye kalori 2,100, ambapo  kutokana na ukata kuanzia mwezi Machi mwaka huu, mgao ulipunguzwa kutoka kukidhi asilimia 80 ya mahitaji ya kalori hadi asilimia 65 ambazo nazo zimepunguzwa.

Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Tanzania Sarah Gordon aliyekuwa akizungumza wakati  wa kutoa taarifa hiyo amesema kwa sasa wanahitaji fedha zaidi ili kukidhi mahitaji ya chakula kwa wakimbizi yanayozidi kuongezeka.

“Tunahitaji Sh49.6 bilioni kwa dharura ili kutoa msaada wa chakula kwa zaidi ya wakimbizi 200,000 kwa muda wa miezi sita ijayo na kuepuka kuendelea kuwapunguzia chakula,” amesema Mkurugenzi huyo.


Soma zaidi


Licha ya pendekezo hilo WFP inasema tangu mwezi Machi mwaka huu, wakimbizi waliopo nchini wameshindwa kupata kiwango hicho cha chakula kinachoshauriwa na wataalamu wa afya kutokana na ukata.

Tunaomba jumuiya ya kimataifa, Serikali, wafadhili, na sekta binafsi kujitokeza na kukabiliana na janga hili ili kuhakikisha watu walio katika mazingira magumu wanaweza kukidhi mahitaji yao ya msingi ya chakula na lishe,”ameongeza Gordon.

Tanzania ni moja kati ya nchi zinazopokea wakimbizi kutoka mataifa mbalimbali kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)  na Burundi kutokana na machafuko ya kisiasa yanayozikumba nchi hizo kwa nyakati tofauti.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamadi Masauni aliyekuwa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi, hadi kufikia Mei, 2023, Tanzania inahifadhi jumla ya wakimbizi 269,749 ambapo jumla ya wakimbizi 10,335 waliokuwepo nchini walipatiwa suluhisho la ikiwemo kurudishwa nchini kwao au kupelekwa nchi nyingine.

Hata hivyo asilimia 70 ya wakimbizi hao 200,000 watakaokumbwa na changamoto ya kupunguziwa chakula wanatoka katika nchi ya burundi na  asilimia 30 ni kutoka DRC.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW