Tanzania namba nne uzalishaji tumbaku Afrika

Mwandishi Wetu 0923Hrs   Mei 31, 2023 Afya & Maisha
  • Yatanguliwa na nchi za Zimbambwe, Malawi na Msumbiji
  • Wataalamu wa afya watahadharisha ongezeko hilo
  • WHO wazitaka serikali kuacha kutoa ruzuku kurahisisha kilimo cha zao hilo

Dar es Salaam. Tanzania imeingia katika orodha ya nchi vinara katika uzalishaji wa tumbaku barani Afrika, licha yazao hilo kuwa na madhara lukuki kwa afya ya binadamu kwa kusababisha magonjwa  pamoja na mazingira.

Ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa Mei  25, 2023 ikiwa ni siku ya kupinga matumizi ya bidhaa za tumbaku, imeitaja  Tanzania kushika nafasi ya nne kwa nchi za Afrika zenye maeneo makubwa ya uzalishaji wazao hilo ikiwa na jumla ya hekta 80,678.

Eneo hilo linalolimwa tumbaku nchini Tanzania ni sawa na nusu ya eneo zima la jiji la Dar es Salaam ambalo lina kilomita za mraba 1590 sawa na hekta 159,000.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo nchi zinazoongoza kwa kilimo cha zao hilo barani Afrika ya kwanza ni Zimbabwe yenye hekta112,770 ikifuatiwa na Malawi (hekta 100,962) na Msumbiji yenye hekta 91,469.

WHO iimebainisha kuwa wakati maeneo yanazotumika kuzalisha zao hilo duniani yamepungua hali ni tofauti barani Afrika ambako kilimo cha zao hilokimeendelea  kuongezeka ndani ya kipindi cha miaka 15. 

“Kuanzia 2005 hadi 2020 eneo linalolimwa tumbaku lilipungua duniani kote kwa asilimia 15.8, wakati Afrika liliongezeka kwa asilimia 19.8. Afrika Mashariki inachukua asilimia 88.5 kwa uzalishaji wa tumbaku,” imeainisha sehemu ya ripoti ya hiyo.


Soma zaidi


Uzalishaji wa tumbaku nchini wapaa

Hata hivyo, ripoti hii ya WHO inaoana na  takwimu za uzalishaji wa zao hilo nchini zilizo orodheshwa katika makadirio ya bajeti ya Wizara ya Kilimo ambazo zinaonyesha kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo.  

Waziri wa Kilimo hussein Bashe alipokuwa akisoma Bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24 aliwaambia wabunge kuwa Serikali imepanga kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka tani 60 874 hadi tani 160,000 mwaka 2024 ambapo mauzo ya zao hilo pia yameongezeka.

“Mauzo ya zao la tumbaku  nje ya nchi yamefikia Sh364 bilioni zinazotarajiwa kuongezeka hadi kufikia Sh881 bilioni ifikapo mwaka 2060,” amesema Bashe.

Ongezeko hilo lina maana gani ?

LIcha ya faida za kiuchumi ambazo zao la tumbaku linaipatia  Tanzania ikiwemo fedha za kigeni zinazopatikana baada ya mauzo, wataalamu wa afya wanatahadharisha ongezeko la uzalishaji huo linaweza kusababisha kuongezeka kwa watumiaji na kuchangia afya zao kuzorota.

“Tumbaku inapozalishwa kwa wingi inakuwa inapatikana kiurahisi hivyo kuongeza watumiaji ambapo moja kwa moja inaenda kuathiri afya za watumiaji,”amesema Daktari George Munisi kutoka Hospitali ya Kibondo Mkoani Kigoma.

Kwa mujibu wa Dk. Munisi sumu ya nikotini iliyopo katika zao hilo inaweza kusababisha magonjwa mbalimbali kama kansa ya mapafu, kifua kikuu, na aina nyingine za magonjwa.

“Gramu moja ya nikotini ukitumia kwa kipindi cha mwezi mmoja inaweza kusababisha hatari kubwa sana ya kupata kifua kikuu kuliko fundi anayefanya kazi kwenye  cement (saruji),” ameongeza Dk.Munisi.

Ili kuzuia athari za moja kwa moja za ongezeko hilo Dk.Munisi anashauri utoaji wa elimu juu ya madhara ya tumbaku kwa wananchi pamoja na Serikali kuweka sheria za kudhibiti makali ya bidhaa ikiwemo kupunguza makali ya tumbaku.

WHO watoa mbinu

katika kukabiliana na madhara yatokanayo na tumbaku duniani ikiwemo magonjwa na athari za kimazingira WHOimeshauri kuwa ni vyema Serikali ikapunguza ruzuku ya mazao hayo na kugeukia katika uzalishaji wa mazao ya chakula.

Kwa wakulima wa zao hilo WHO imewataka kutumia programu zinazoungwa mkono na serikali kwa ajili ya kulima  mazao mbadala na kuachana na tumbaku.

Related Post