Tanzania yaongeza kasi utafutaji masoko ya nafaka kimataifa

January 26, 2022 7:51 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imefanya mazungumzo na WFP ili inunue nafaka zake.
  • Yafungua vituo viwili vya nafaka nchini Sudan Kusini na Congo DRC.
  • Huenda wakulima wakapata ahueni ya soko la mazao yao.

Dar es Salaam. Huenda ikawa kicheko kwa wakulima wa mahindi kunufaika na kilimo cha zao hilo baada ya Serikali kuimarisha na mipango ya kutafuta masoko ya kimataifa ikiwemo kuzungumza na wahisani ili kununua nafaka za Tanzania. 

Hatua hiyo ya Serikali ni kutafuta suluhu ya kuwepo kwa hifadhi kubwa ya mahindi nchini, jambo linalowafanya wakulima waliowekeza fedha zao washindwe kufaidika kikamilifu na kilimo. 

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Lameck Nchemba ameliomba Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP), kununua shehena ya nafaka kutoka kwa wakulima hapa nchini kwa ajili ya matumizi yake ya kulisha wakimbizi maeneo mbalimbali wanayoyahudumia.

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka sita kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2021, Tanzania imezalisha ziada ya chakula kiasi cha tani milioni 17.8 na kwamba ukosefu wa soko la mazao hayo ya kilimo unakwamisha juhudi za wakulima kujikwamua kiuchumi.

“Rai ya Wizara na Serikali kwa ujumla ni kuendelea kushirikiana katika maeneo ambayo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ameyawekea kipaumbele cha kutafuta masoko ya bidhaa za wakulima wetu kwa hiyo WFP na maeneo mnayoyahudumia mnaweza kusaidia kupata masoko ili wakulima waweze kunufaika na uzalishaji wao,” amesema Dk Nchemba.

Dk Nchemba ametoa wito huo Jijini Dodoma Januari 27, 2022 alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo, Sarah Gibson, ambapo wawili hao wamejadiliana masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya Serikali na WFP.

Pia ameliomba Shirika hilo kusaidia upatikanaji wa masoko na fedha kwa ajili ya kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji ili kuiwezesha nchi kuzalisha chakula kwa wingi na Tanzania kuwa ghala la chakula.

Licha ya ombi hilo, Serikali inaendelea kununua mahindi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Mazao Mchanganyiko (CPB) na  imefungua milango kwa wakulima kuuza mahindi nje ya nchi. 


Zinahusiana: 


Mwakilishi Mkazi wa WFP, Sarah Gibson amesema kuwa msimu huu, shirika lake limenunua tani 76,000 za chakula nchini Tanzania kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 25 (Sh76.7 bilioni) na kuzisambaza kwenye maeneo yenye uhitaji.

“Katika kipindi hicho pia tumetumia kiasi cha Dola za Marekani milioni 19 (Sh43.9 bilioni) kwa ajili ya kuboresha shughuli za uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusafirisha chakula kinachopelekwa kwenye maeneo yenye uhitaji hususan maeneo ya wakimbizi,” amesema Gibson.

Gibson amesema pia kuwa shirika lake limepanga kurejesha huduma ya chakula mashuleni hapa nchini baada ya kusitisha huduma hiyo miaka michache iliyopita kutokana na umuhimu wa chakula kwa watoto wakiwa shuleni.

“Pia tumepanga kuanzisha mpango wa kuwasaidia watu kupata fedha taslimu kwa njia ya kushiriki kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali katika maeneo yao ikiwemo miradi ya kilimo, ujenzi wa miundombinu pamoja na kuwapatia mikopo midogo midogo pamoja na masoko ya uhakika wakulima wadogo wadogo” amesisitiza Gibson

Tanzania yajenga vituo vya nafaka nje ya nchi

Katika kuimarisha soko la nafaka nje ya nchi, Serikali ya Tanzania imejenga vituo viwili vya kuhifadhia nafaka katika jiji la la Juba (Sudan Kusini) na Lumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Congo DRC).

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe katika ukurasa wake wa Twitter amesema juhudi hizo ni kuwawezesha wakulima kupata soko zuri la mazao yao nje ya nchi. Tayari wameshapeleka tani 800 katika vituo hivyo viwili.

 “Katika Wizara ya Kilimo tunaamini upatikanaji wa masoko unawahamasisha wakulima kuongeza uzalishaji,” amesema Bashe na kubainisha kuwa vituo hivyo vitatumiwa na Serikali kupitia sekta binafsi na CPB.

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
15 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
15 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
15 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mwenendo wa deni la serikali

Mwenendo wa deni la serikali

Nukta TV

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Nukta TV

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Nukta TV