Mambo yatakoyasaidia kupunguza tabia ya utupaji chakula
- Nunua chakula kulingana na mahitaji yako.
- Hifadhi sehemu salama chakula chako kwa matumizi ya baadaye.
- Gawa chakula kwa wenye uhitaji na siyo kutupa.
Dar es Salaam. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema kupunguza upotevu na utupaji wa chakula ni muhimu katika dunia ambayo mamilioni ya watu wanalala njaa kila siku.
Kwa mujibu wa takwimu za FAO, tani milioni 931 sawa na asilimia 17 ya chakula kilichozalishwa mwaka 2019 kiliishia kwenye mapipa ya taka ya kaya, wauzaji, migahawa na wadau wengine wa chakula.
Pia shirika hilo limeeleza kuwa watu milioni 811 wana njaa na milioni 132 wanakabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula na lishe kutokana na janga la Corona (Uviko-19).
Upotezaji wa chakula wa kila mwaka unakadiriwa kuwa ni wa gharama ya Dola za Marekani bilioni 400 (Sh922.6 trilioni).
Takwimu hizi zimetolewa jana wakati dunia ikiadhimisha siku ya kimataifa ya uhamasishaji kuhusu upotezaji na utupaji wa chakula ambayo itakuwa ikiadhimishwa Septemba 29 kila mwaka.
Shirika hilo limeongeza kuwa chakula kisichotumiwa hupoteza rasilimali ikiwemo ardhi, maji, nishati, udongo, mbegu na pembejeo zingine zinazotumika kwa uzalishaji wake.
Kupunguza upotevu na utupaji wa chakula kutaboresha mifumo ya chakula, kuchangia uuhakika wa chakula na kuhakikisha ubora wa chakula ambao unaonekana katika lishe.
Hifadhi chakula sehemu salama kwa matumizi ya baadaye. Picha| Gift Mijoe.
FAO imeainisha hatua rahisi ambazo kila mmoja anaweza kuchukua ili kukithamini na kukienzi chakula na kuepuka utupaji wa hovyo:
Kutumia lishe bora na endelevu
Maisha yanaenda kwa kasi na kuandaa chakula chenye lishe inaweza kuwa changamoto, lakini milo yenye afya si lazima itumie muda mrefu kuandaliwa. Mtandao umejaa mapishi ya haraka yenye afya ambayo unaweza kushiriki na familia yako na marafiki zako.
Panga chakula chako. Fanya orodha ya ununuzi na uizingatie, na epuka ununuzi wa kukurupuka. Siyo tu utapoteza chakula kidogo, bali pia utaokoa pesa yako.
Usihukumu chakula kwa muonekano wake. Matunda na mboga zenye umbo la kushangaza au zilizopondwa mara nyingi hutupiliwa mbali kwa sababu hazifikii viwango vya kupendezesha macho. Tumia matunda yaliyokomaa kwa kutengeneza urojo, juisi na kuyala jinsi yalivyo.
Hifadhi chakula kwa busara
Sogeza bidhaa za zamani mbele ya kabati yako au jokofu na mpya weka nyuma. Tumia vyombo visivyoingiza hewa kuweka chakula wazi kwenye jokofu na hakikisha vikasha vimefungwa ili kuzuia wadudu kuingia.
Pia ni muhimu kufahamu tarehe ya kuisha kwa matumizi ya chakula husika ili kuepuka kununua chakula kingi na baada kutupwa muda ukiisha.
Endapo hutoweza kula kila kitu, kihifadhi kilichosalia kwenye jokofu kwa ajili ya baadaye au tumia mabaki hayo kuandaa mlo mwingine.
Badala ya kutupa mabaki ya chakula chako, yatumie kama mbolea. Kwa njia hii unarudisha virutubishi kwenye mchanga na kupunguza kiwango cha uzalishaji wako wa hewa ukaa.
Kijali chakula chako na kitumie vizuri ili kuepuka kuharibika na kutupa. Picha| Gift Mijoe.
Heshimu chakula
Chakula kinatuunganisha wote. Ungana tena na chakula kwa kujua mchakato wa kukiandaa. Soma juu ya uzalishaji wa chakula na uwajue wakulima wako.
Kwa kununua mazao yanayozalishwa ndani ya nchi unasaidia wakulima wa familia na wafanyabiashara wadogo katika jamii yako. Unasaidia pia kupambana na uchafuzi wa mazingira kwa kupunguza umbali wa kusafirisha chakula kwa malori na magari mengine.
Unashauriwa kula aina mbalimbali za samaki ikiwemo sato na sangara badala ya zile zilizo katika hatari ya kuvuliwa kupita kiasi, kama papa au jodari. Nunua samaki waliovuliwa au kufugwa kwa njia endelevu, kama samaki waliowekwa alama ya kujali mazingira au waliothibitishwa.
Hatuwezi kuzalisha chakula bila maji. Ingawa ni muhimu kwa wakulima watumie maji kidogo kukuza chakula, kupunguza taka ya chakula kunaokoa rasilimali zote za maji zilizoingia katika kuzalisha chakula.
Punguza matumizi yako ya maji kwa njia zingine pia kama kukarabati mabomba yanayovuja au kufunga mabomba ya maji wakati unasafisha meno yako!
Taka zingine za nyumbani zina hatari na hazipaswi kutupwa kwenye pipa la taka za kawaida. Vitu kama betri, rangi, simu za rununu, dawa, kemikali, mbolea, matairi, makasha ya wino zinaweza kuingia kwenye mchanga na mfumo wa usambazaji wa maji, na kuharibu rasilimali za asili zinazozalisha chakula chetu.
Wape chakula watu wenye uhitaji. Kama umenunua chakula kingi na haukitumii gawa kwa watu wengine kuliko kukitupa.
Latest