Uamuzi mgumu UN: Nani apatiwe msaada wa chakula Afrika Mashariki?
- Mamilioni ya wakimbizi wa Mashariki mwa Afrika wako hatarini kutumbukia kwenye njaa kali.
- Ni baada ya mgao wa chakula kupungua.
- UNHCR, WFP zahaha kugawa chakula kilichopo kwa wakimbizi zaidi ya milioni 5.
Dar es Salaam. Mamilioni ya familia za wakimbizi katika eneo la Mashariki mwa Afrika ikiwemo Tanzania ziko hatarini kutumbukia kwenye njaa kali wakati huu ambapo mgao wa chakula unapungua kutokana na rasilimali za misaada ya kibinadamu kuzidiwa uwezo.
Hali hiyo imesababishwa na madhara ya tabianchi, janga la Uviko-19 na ongezeko la bei ya chakula na mafuta, yamesema mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) na mpango wa chakula duniani (WFP).
Mashirika hayo katika taarifa ya pamoja iliyotolewa April 13 Geneva, Uswisi yamesema, licha ya juhudi za kuhakikisha chakula kilichopo kinapatiwa familia kwa misingi ya kipaumbele cha uhitaji, idadi ya wakimbizi wenye uhitaji inaongezeka, sambamba na pengo la rasilimali zilizopo.
Wakimbizi hao wako katika nchi za Burundi, Djibouti, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania na Uganda.
Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, idadi ya wakimbizi Mashariki mwa Afrika imeongezeka mara tatu kutoka milioni 1.82 mwaka 2012 hadi takribani milioni 5 Aprili mwaka huu, ikiwemo wakimbizi wapya 300,000 wa mwaka jana pekee.
WFP imesema ongezeko la idadi ya wakimbizi isiyoendana na chakula kinachopatikana kinaliacha shirika hilo na uamuzi mgumu wa nani apatiwe msaada wa chakula na nani anyimwe.
“Leo hii asilimia 70 ya wakimbizi wenye uhitaji hawapokei mgao kamili wa chakula kutokana na ukata,” amesema Clementine Nkweta-Salami, Mkurugenzi wa UNHCR kwa kanda ya Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu.
Soma zaidi:
-
Ahueni kwa wakulima bei ya mahindi ikipanda kidogo Tanzania
-
Bei ya mahindi yapaa mara mbili Tanzania
-
Maumivu kwa wakulima, bei ya mahindi yaendelea kushuka Tanzania
Amesema watoto wengi zaidi wenye umri wa chini ya miaka 5 wanakumbwa na viwango vya juu vya udumavu na ukuaji usiondana na umri wao kwa kuwa hawana lishe bora na virutubisho vinavyotakiwa wakati wanakua.
“Familia hazijui mlo ufuatao unatokana wapi na wanakumbwa na deni kubwa, wanauza mali zao na hata kuwaondoa watoto wao shulen ili washiriki katika kazi. Hii inaongeza hatari ya ukatili wa majumbani. Kuwaondoa watu kwenye hatari hii inapaswa mahitaji yao ya chakula yaweze kukidhiwa.
“Ukweli wa kusikitisha ni kwamba eneo la Mashariki mwa Afrika linakumbwa na mahitaji ya aina yake ya kibinadamu, yakichochea na mabadiliko ya tabianchi, mizozo, ukosefu wa utulivu na ongezeko la bei za vyakula na nishati ya mafuta,” amesema Michael Dunform, Mkurugenzi wa WFP kanda ya Mashariki mwa Afrika.
Amesema ongezeko la mahitaji kwenye ukanda huo linaakisi kile kinachoonekana pia duniani kote, “hivyo tunaomba dunia isiipe kisogo eneo hili na hususan jamii zilizo hatarini zaidi za wakimbizi ambazo zina fursa finyu ya mbinu za kujipatia kipato na tegemeo lao kuu ni WFP ili ziweze kuishi.”
WFP kwa kuanzia kipindi cha mwezi Aprili hadi Septemba mwaka huu wa 2022, inahitaji dola milioni 226.5 (Sh525.8 bilioni kukidhi mgao kamilifu wa chakula kwa wakimbizi katika nchi zilizoko Mashariki mwa Afrika.