ACT- Wazalendo yaibuka na hoja 8 bajeti Wizara ya Kilimo 2023-24
- Yasema bajeti ya mwaka 2023/24 haiakisi mahitaji ya sasa ya wakulima.
- Serikali yashauriwa kuongeza uwezo wa kuhifadhi vyakula, na kutoa pembejeo na kuimarisha sekta ya umwagiliaji.
Dar es Salaam. Chama Cha ACT-Wazalendo kimesema bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2023/24 haiakisi mahitaji ya sasa ya wakulima nchini huku kikiangazia maeneo nane ambayo yanapaswa kushughulikiwa na Serikali ili kuleta ahueni kwa wakulima.
Hatua hiyo ya ACT inakuja ikiwa imepita siku moja tu tangu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aombe Bunge liidhinishe jumla ya Sh970 bilioni kwa ajili ya mwaka 2023/24 ambapo asilimia 84 ya bajeti hiyo imeelekezwa katika miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Bashe, fedha hizo zinatarajiwa kutekeleza vipaumbele kadhaa ikiwamo kuimarisha utafiti wa kilimo, uzalishaji wa mbegu, utoaji wa ruzuku, kilimo cha umwagiliaji, miundombinu ya uhifadhi wa mazao, na huduma za ugani.
Mtutura Abdallah Mtutura ambaye ni Waziri Kivuli wa Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi amewaambia wanahabari Leo Mei 9, 2023 kuwa wamepitia na kuchambua bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa makini wameibuka na hoja nane zinazotakiwa kupatiwa ufumbuzi.
Upatikanaji na uzalishaji wa chakula usioridhisha
Mtutura amebainisha kuwa kutokana na kupungua kwa kiwango cha uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2021 kwa asilimia 15, baadhi ya maeneo yanakabiliwa na mfumuko wa bei pamoja na uhaba wa chakula licha ya kuwa na ziada ya tani milioni 2 za chakula
“Pamoja na hali ya uzalishaji wa chakula kwa ujumla umeonyesha tumejitosheleza, lakini kuna baadhi ya maeneo yamekumbwa na uhaba wa chakula na kusababisha mfumuko mkubwa wa bei za chakula katika nchi kwa ujumla wake,” amesema Mtutura katika ofisi za Chama hicho jijini Dar es Salaam.
Mtutura amebainisha kuwa licha ya Wizara ya Kilimo kuwa na mpango wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka hadi kufikia tani 500,000, bado kiwango hicho ni kidogo kukabiliana na mfumuko wa bei au baa la njaa hivyo waongeze mpaka tani milioni 1.5.
“Hatua hii itawezakana kwa Serikali kuongeza bajeti kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ya kutosha kununua chakula (Tani Milioni 1.5 za Mahindi, Tani laki 5 za Mpunga, Maharagwe tani Milioni 1) badala ya tani laki 5 pekee,” amesisitiza Mtutura.
Mtutura Abdallah Mtutura, Waziri Kivuli wa Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi akisoma uchambuzi wa najeti ya Wizara ya Kilimo katika Ofisi za ACT-Wazalendo. Picha l Esau Ng’umbi/Nukta Africa.
Kasi ya Ukuaji wa sekta ya kilimo haitoshi kusukuma gurudumu la maendeleo
Pamoja na Wizara ya Kilimo kuweka mikakati ya kufikisha asilimia 10 ya kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo mwaka 2030, chama hicho kimedai kuwa Serikali haijafanya jitihada za kutosha kuhakikisha hilo linatokea kwani hakuna mikakati iliyowekwa wazi juu ya namna ya kulifanikisha hilo.
“Kwa mfano mwaka 2021 kasi ya ukuaji wa sekta ilikuwa asilimia 3.9 waziri hajaiambia nchi 2023 wanatarajia kasi ya ukuaji kufikia asilimia ngapi? Kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo haiwezi kufika tu asilimia 10 ifikapo 2030. Lazima ipande kutoka ilipo sasa hadi kufikia huko. Waziri hajalieleza bunge tunafikaje asilimia 10 mwaka 2030,” amebainisha Mtutura.
ACT wamebainisha kuwa ili kufikia lengo hilo uchumi unatakiwa ukue kwa kasi ya wastani wa asilimia 8 kwa mwaka kwa miaka 10 mfululizo ya mwanzo na kasi isipungue asilimia 6 kwa miaka mingine 10 hadi kufikia 2050.
Kuboreshwa kwa usambazaji wa pembejeo za kilimo
Kwa mujibu wa Mtutura katika misimu iliyopita hali ya upatikanaji wa pembejeo ulikuwa si wa kuridhisha, jambo lililosababisha kupanda kwa gharama ya mazao kutokana na gharama za uzalishaji licha ya Serikali kuweka ruzuku katika pembejeo, ugawaji ulikuwa na dosari ikiwemo usimamizi mbovu na kusababisha hasara.
ACT imeishauri Serikali pamoja na kuweka nia ya kuendelea kutoa ruzuku ioneshe namna itakavyoenda kukabiliana na changamoto zilizobainika ikiwemo umbali wa vituo vya kugawa mbolea, kuboresha mfumo wa ugawaji wa mbolea, pamoja na kuiongezea bajeti Kampuni ya Mbolea ya Taifa ili iweze kuagiza mbolea kwa wingi.
Hoja nyingine iliyowasilishwa ni pamoja na kutofungamanishwa kwa sekta ya viwanda na kilimo wakati muundo na sifa za uchumi wa Tanzania unatawaliwa kwa sehemu kubwa na sekta ya uzalishaji wa malighafi hususani kilimo, uvuvi, misitu na madini.
“ACT Wazalendo, tunaendelea kusisitiza kuwa ni wakati sasa wa kuunganisha maendeleo ya viwanda na ukuaji wa kilimo. Serikali iweke mkazo kwenye viwanda vidogo maeneo ya vijijini vinavyoendeshwa, kumilikiwa na kusimamiwa na wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya ushirika ambavyo vitaweza kuzalisha ajira na kuchakata mazao kwa dhamira ya kuyaongezea thamani,” amesema Mtutura.
Soma zaidi
-
Kufa kufaana: Bei ya mahindi yapaa Tanzania
-
Majaliwa aingilia kati sakata kelele zilizopitiliza nyumba za ibada
-
Mifugo ni fursa unaitumiaje?
Migogoro ya ardhi
Ili kukabiliana na migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiibuka mara kwa mara na kuathiri sekta ya kilimo, ACT Wazalendo wameishauri Serikali kuharakisha na kukamilisha zoezi la kupima, kurasimisha na kumilikisha ardhi kwa wananchi ili kuepusha migongano na mivutano.
“Mamlaka za Halmashauri zijengewe uwezo stahiki na kuwezeshwa ipasavyo ili ziweze kushugulikia migogoro ya ardhi upesi na kwa ufanisi pamoja na kuhakikisha ardhi imepimwa na kurasimishwa kwa wananchi,” amesema Waziri huyo Kivuli.
Mturura amesisitiza kuwa Serikali inapaswa kusitisha kabisa tabia ya kupanua maeneo ya hifadhi kwa kuwanyang’anya wananchi maeneo yao ya kulisha mifugo na kilimo kwani upanuzi huo unafifisha jitihada za wafugaji na wakulima katika uendeshaji wa shughuli zao za uchumi.
Kilimo cha umwagiliaji kiwanufaishe wakulima
ACT wamedai kuwa pamoja na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji (Irrigation Development Fund (IDF)) kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), bado sekta hiyo ya umwagiliaji haiwanufaishi wakulima.
Serikali imeshauriwa kuwekeza nguvu zaidi kwenye mabonde ya Mto Ruvu, Rufiji, Pangani, Kilombero, Ruvuma, Mbwenkuru, Ruaha, Kihansi, Mara, na mabonde ya Ziwa Tanganyika na Victoria ambayo yatalisaidia Taifa kuwa na akiba ya chakula cha kutosha na ziada kujipatia pesa za kigeni.
Sheria na mfumo wa kodi wa kilimo uanzishwe
Kwa mujibu wa ACT kukosekana kwa mfumo wa kodi unaoeleweka na usiotetereka katika kuisimamia sekta ya kilimo inarudisha nyuma maendeleo ya wakulima na kusababisha kuporomoka kwa bei ya mazao na wakulima kutooana tija ya jasho lao.
Kutokana na umuhimu wa sekta ya kilimo nchini ACT wameishauri Serikali kutunga mfumo wa kodi unaoeleweka na usiotetereka (stable fiscal regime) katika sekta ya kilimo ili kuhakikisha kuwa mkulima anabakia na sehemu kubwa ya mapato yake.
“Ili kukabiliana na upungufu mkubwa wa chakula unaotazamiwa kutokea nchini, tunaitaka Serikali iongeze bajeti ya NFRA itakayoiwezesha kununua na kuhifadhi chakula kinachoweza kulilisha taifa walau kwa miezi mitatu.”
Waziri Kivuli wa Kilimo@AMtutura#TaifaLaWote#MaslahiYaWote
pic.twitter.com/ZYjnODAIan— ACT-Wazalendo (@ACT_wazalendo1) May 9, 2023
Latest
