Wagonjwa wa ukoma wapungua kwa asilimia 57 Tanzania

January 28, 2024 8:53 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wamepungua kutoka wagonjwa 2,297 mwaka 2015 hadi wagonjwa 1,309 mwaka 2023.
  • Halmashauri 19 katika mikoa tisa hatarini.

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha siku ya ukoma, nchini Tanzania idadi ya wanaougua ugonjwa huo imepungua kwa asilimia 57 ndani ya kipindi cha miaka tisa.

Taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu, leo Januari 28, 2024 inaeleza kuwa kupungua kwa visa vya ugonjwa huo kunaifanya Tanzania kufikia kiwango cha awali cha Shirika la Afya Duniani (WHO) cha kutokomeza ugonjwa wa Ukoma.

“Idadi ya wagonjwa wapya imepungua kutoka wagonjwa 2,297 mwaka 2015 hadi wagonjwa 1,309 mwaka 2023 sawa na punguzo la asilimia 57. Kwa tafsiri hii, mwaka 2023 nchi yetu ilikuwa na wagonjwa 3 kwa kila watu 100,000,” inasema taarifa ya Prof. Nagu.

Ili kupambana na ugonjwa huo, WHO iliweka malengo kwa kila nchi duniani kupunguza wagonjwa wa ukoma hadi kufikia mgonjwa mmoja katika kila watu 10,000, ambapo Tanzania ililifikia tangu mwaka 2006.

Hata hivyo, bado WHO inaendeleza mapambano ili kumaliza kabisa ugonjwa huo katika nchi zote duniani kupitia kampeni mbalimbali hususani ya ‘zero Leprosy’ inayotekelezwa kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2030.

Maadhimisho ya ugonjwa huo kwa mwaka 2024  yana kaulimbiu isemayo “thamini Utu, tokomeza unyanyapaa dhidi ya waathirika wa ukoma” ikilenga kutoa hamasa kwa jamii juu ya wajibu wa kuendelea kupambana na kuutokomeza kabisa Ugonjwa wa Ukoma.


Soma zaidi:Unavyoweza kuepuka ugonjwa wa ‘red eyes’


Mikoa tisa hatarini 

Licha ya mafanikio ya kufikia malengo ya kutokomeza ukoma nchini, taarifa ya Prof. Nagu inabainisha kuwa bado kuna halmashauri 19 kutoka mikoa tisa ambazo hazijafikia viwango vya utokomezaji wa ugonjwa huo.

Halmashauri hizo zipo katika mikoa ya Morogoro, Lindi, Dar es Salaam, Mtwara, Kigoma, Tanga, Dodoma, Geita, na Pwani.

Kutokana na hayo, Prof. Nagu ametoa wito kwa wanajamii  kutambua dalili za ukoma na kuhakikisha wote wenye dalili wanafika katika kituo cha afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.

“Waganga wakuu wa mikoa na halmashauri, kushirikiana na vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa ugonjwa wa ukoma katika kaya zote zenye wagonjwa wapya wa Ukoma na kutoa tiba kinga,” ameongeza Prof. Nagu.

Aidha, ametoa rai kwa halmashauri zote nchini kuhakikisha inafanya juhudi kuibua wagonjwa, kufuatilia mwenendo wa ugonjwa, na kuwa na takwimu sahihi za kufuatilia wagonjwa kulingana na maeneo au vijiji au mitaa wanakopatikana.

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV