Unavyoweza kuepuka ugonjwa wa ‘red eyes’

Lucy Samson 0324Hrs   Januari 16, 2024 Afya & Maisha
  • Ni pamoja na kuzingatia kanuni za usafi ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara.
  • Wataalamu wa afya watahadharisha matumizi holela ya dawa za mitishamba kutibu ugonjwa huo.

Dar es Salaam. Ugonjwa wa macho mekundu ama ‘red eyes’ kama unavyofahamika na wengi, umewafanya baadhi ya watu kuanza mwaka 2024 kwa maumivu.

Ugonjwa huo unaofahamika kwa jina la kitaalam la ‘Viral Conjunctivitis’  husababishwa na bacteria, virusi au mzio na husambazwa kwa njia ya hewa na kuathiri ngozi ya juu ya gololi la jicho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa January 15, 2024 na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Prof. Pascal Ruggajo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali Prof Tumaini Nagu, visa vya ugonjwa huo vimekuwa vikiongezeka nchini hususan jijini Dar es Salaam.

“Katika kipindi cha Disemba 22, 2023 hadi Januari 11, 2024 kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaosumbuliwa na ugonjwa huu kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya matibabu…

…Kwa mfano katika mkoa wa Dar es Salaam kuna wagonjwa wapya 869 huku hali ya kawaida katika kipindi cha mwezi Disemba 2023 kulikuwa na wagonjwa 17 pekee” amefafanua Prof. Ruggajo.

Mkurugenzi huyo pia amebainisha kuwa dalili za ugonjwa huo ni pamoja na na macho kuwasha, kuchomachoma, kuuma, macho kutoa machozi na kutoa tongotongo za njano.


Soma zaidi:Mwanza na mapambano dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu


Tumia njia hizi kujikinga

Wakati Prof. Pascal Ruggajo akisisitiza suala la usafi kama njia ya kujikinga, tofauti ya masuala ya afya ‘Medical News Today’ inafafanua kuwa njia hizo za usafi kuwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara kwa wagonjwa na wasio wagonjwa.

“wagonjwa walioambukizwa wanapaswa kuzuia maambukizi kwa kunawa mikono mara kwa mara, kutumia taulo tofauti, na kuepuka kugusana kwa karibu na wengine,” imesema tovuti ya Medical News Today.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanafafanua kuwa ugonjwa huu sio wa hatari kiasi cha kusababisha madhara mengine ya kiafya kama upofu.

“Kama nilivyosema, ni ugonjwa unaoisha wenyewe baada ya siku tano mpaka 14 Ila ukionyesha kuzidi ndipo unaweza kumuona mtaalamu akakushauri na kukupa dawa (antiviral),” anasema Samwel Mazengo, muuguzi katika kitengo cha macho Hospitali ya Wilaya ya Kiteto Manyara. 

Aidha, mtaalamu huyo amekemea vitendo vya baadhi ya wananchi kujitibu nyumbani kwa kutumia dawa za asili ikiwemo mitishamba hali inayoweza kusababisha madhara zaidi kwenye jicho.

“Macho ni kiungo ‘sensitive’ sana hivyo sio cha kufanyia majaribio ya matibabu…dawa za kienyeji ni moja ya sababu zinazopelekea upofu, hivyo ni vema kujihadhari,” amefafanua Mazengo.

Hii si mara ya kwanza kwa ugonjwa huu kuripotiwa nchini, itakumbukwa kuwa miaka ya 2017 na 2021  pia kuliibuka visa vingi vya ugonjwa huu hivyo ni vyema wananchi kuchukua tahadhari za kiafya muda wote.

Related Post