Tanzania na Uviko-19: Maambukizi yaongezeka kwa asilimia 62

December 6, 2022 9:15 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni katika kipindi cha mwezi Oktoba 29 hadi Disemba 2, 2022.
  • Asilimia 94 ya walengwa wameshapata chanjo ya Uviko-19.
  • Tahadhari zasisitizwa kuendelea kuchukuliwa.

Dar es Salaam. Ni miaka miwili sasa imepita tangu kiliporipotiwa kisa cha kwanza cha  Uviko-19 nchini Tanzania jambo ambalo huenda limesababisha baadhi ya Watanzania kudhani ugonjwa huo haupo tena.

Hata hivyo, ugonjwa huo bado upo nchini na taarifa zinaonesha visa vya Uviko-19 vimeongezeka kwa asilimia 62 ndani ya mwezi mmoja. 

Taarifa ya mwenendo wa maambukizi ya Uviko-19 iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu imeeleza kuwa ongezeko hilo limetokea kati ya Oktoba 29 hadi Disemba 2 mwaka huu.

“Katika kipindi cha tarehe Oktoba 29  hadi Desemba 2, 2022, jumla ya visa vipya 442 vimethibitika kuwa na maambukizi ya Uviko-19. Idadi hii ni kubwa ukilinganisha na takwimu za mwezi uliopita ambapo kulikuwa na visa vipya 272, sawa na ongezeko la asilimia 62.5, “ inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Pamoja na kuongezeka kwa visa vya maambukizi hakuna mgonjwa aliyelazwa au kifo kilichotokea kutokana na Uviko-19.

Kupungua kwa idadi ya visa vya maambukizi pamoja na vifo vinavyotokana na Uviko-19 kulisababisha baadhi ya watu kutozingatia miongozo iliyotolewa na wataalamu ili kujikinga na ugonjwa huo  kama kuvaa barakoa au kutokaa kwenye misongamano isiyo ya  lazima.

“Tumeaimarisha mapambano”

Katika kuimarisha mapambano dhidi ya Uviko-19 miongoni mwa afua zilizohamasishwa ni kupata chanjo kamili  ya Uviko-19 ambapo kwa mujibu wa taarifa hiyo  mpaka Disemba 2 mwaka huu jumla ya watu milioni 29.1 walikuwa wamepata chanjo kati ya walengwa milioni 30.7 sawa na asilimia 94.7.


Zinazohusiana:


Watanzania wenye dalili za magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa kama homa, mafua, kikohozi, mwili kuchoka, maumivu ya viungo, kuumwa kichwa, vidonda koo na kupumua kwa shida wametakiwa kwenda kwenye vituo vya afya ili kupatiwa matibabu stahiki pamoja na kukumbushwa kuendelea kuchukua tahadhari za ugonjwa huo.

“Wizara inaendelea kutoa tahadhari kwa wananchi wote kuchukua hatua za kujikinga na Uviko-19 na magonjwa mengine ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na kupata dozi kamili za chanjo ya Uviko-19, uvaa barakoa pindi unapokuwa na dalili za mafua au kikohozi na uwapo kwenye mikusanyiko,” inasomeka taarifa hiyo.

Kisa cha kwanza cha Uviko-19 kiliripotiwa nchini Tanzania Machi 16 mwaka 2020 ambapo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO tangu Januari 3 mwaka 2020  mpaka Disemba 5 mwaka huu  vimeripotwa visa 40,656 pamoja na vifo 845.

Enable Notifications OK No thanks