Uviko-19 waendelea kuwatesa mamia kimya kimya Tanzania

February 12, 2023 10:25 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Mamia waambukizwa Uviko-19 mwezi Januari 2023 huku mmoja afariki.
  • Wataalamu wa afya wasisitiza watu wote kupata dozi kamili ya chanjo ya ugonjwa huo.  

Dar es Salaam. Iwapo wewe ni miongoni mwa wanaopuuza madhara ya Uviko-19 sasa utalazimika kufikiria mara mbili uamuzi wako baada ya takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kubainisha kuwa mamia ya Watanzania bado wanaathiriwa na ugonjwa huo ulioua mamilioni ya watu ulimwenguni.  

Data za WHO zinaonesha kuwa Tanzania imeripoti wagonjwa wapya 321 wa Uviko-19 ndani ya mwezi mmoja na nusu. 

Katika takwimu hizo zilizochapishwa katika tovuti ya shirika hilo, Tanzania ilikuwa imeripoti jumla ya visa 42,717 mpaka kufikia Februari 10, 2023 kutoka visa 42, 396 vilivyorekodiwa Disemba 26, mwaka jana. 

Wizara ya Afya ya Tanzania haijitoa takwimu mpya siku za hivi karibuni juu ya mwenendo wa maambukizi ya ugonjwa huu ambao kirusi chake kimeendelea kujibadili siku hadi siku. 

Mbali na uwepo wa visa hivyo 321 vilivyotokea ndani ya mwezi Januari, WHO imeripoti kifo kimoja kilichotokana na Uviko-19 ambacho kilitokea Januari 2 mwaka 2023 na kufanya mpaka Februali 10 mwaka huu idadi ya vifo vya Uviko-19 kufikia 846.


Zinazohusiana


Ongezeko la maambukizi na uwepo wa kifo hicho ni moja ya taa nyekundu ya kuwataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19. 

Itakumbukwa mara ya mwisho Serikali kutoa taarifa za Uviko-19 ni Disemba 23,  2022 ambapo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu katika taarifa yake ya salamu za mwisho wa mwaka aliripoti ongezeko la kasi ya visa vipya vya Uviko-19 kutoka asilimia 4.1 mwezi Novemba 2022 hadi asilimia 5.5 mwezi Disemba 2022.

Miongoni mwa hatua ambazo Wizara ya Afya iliwashauri Watanzania kuzichukua ni pamoja na kupata dozi kamili ya chanjo ya Uviko-19, kuvaa barakoa pale inapobidi, kuepuka mikusanyiko pamoja na kunawa mikono na sabuni pamoja na maji tiririka.

Kwa mujibu wa WHO mpaka sasa Tanzania imepokea dozi milioni 36 za chanjo ya Uviko-19 ambapo watu milioni 31 wamepatiwa dozi moja ya chanjo huku watu milioni 29 wakipata dozi kamili.

Wataalamu wa afya wanaendelea kushauri kuwa watu wanapaswa kupata chanjo kamili ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza pale watakapokumbwa na ugonjwa huo. 

Mpaka kufikia Februali 10 mwaka huu kulikuwa na  jumla ya visa milioni 755 vya Uviko-19 ulimwenguni kwa mujibu wa WHO huku watu milioni 6.8 wakipoteza maisha tangu kuanza kwa janga la Uviko-19 mwaka 2019.

Idadi ya watu walifariki dunia kwa Uviko-19 ni sawa na zaidi ya watu wote waliopo Dar es Salaam na Njombe kwa mujibu wa takwimu za Sensa za mwaka 2022. 

Enable Notifications OK No thanks