Wafahamu jongoo bahari wanaouzwa Sh120,000 kwa kilo
- Bei hiyo ni mara 12 ya bei ya kilo moja ya nyama ya ng’ombe katika mabucha mengi ya jiji la Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba jijini Dar es Salaam, si bidhaa za viwandani au mitambo ya kisasa pekee iliyowavutia watu, bali pia viumbe wa baharini akiwemo jongoo bahari, au kwa jina la kitaalamu holothuroidea.
Kwenye moja ya mabanda ya Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), kundi la watu lilionekana limezingira meza iliyokuwa na samakigamba hao, wakipiga picha huku wakimsikiliza kwa makini Afisa wa Udahili wa FETA, Coletha Lyatuu.
Wengi walikuwa na maswali yanayofanana: “Hawa ni viumbe gani? Wanaliwa? Wana ladha gani?”
Kwa mujibu wa Lyatuu, jongoo bahari wanaofugwa na kuoneshwa kwenye banda hilo si tu kwamba wanaliwa, bali wanauzwa kwa bei inayovuka mazao mengi ya baharini kilo moja huuzwa kwa Sh120,000.
Bei hiyo ni mara 12 ya bei ya kilo moja ya nyama ya ng’ombe katika mabucha mengi ya jiji la Dar es Salaam ambayo huuza nyama ya ng’ombe kwa wastani wa Sh10,000 kwa kilo.
“Wateja wakubwa ni wa kutoka Zanzibar, nje ya nchi na mahoteli makubwa hapa nchini,” anasema Lyatuu.

FETA inasema kuwa jongoo bahari wanaweza kufikia uzito wa gramu 250 baada ya miezi minane, na kwa mujibu wa tovuti ya Wild Fact Sheet, viumbe hawa hufikia urefu wa kati ya sentimita 15 hadi 20, lakini baadhi hufika hata sentimita 40.
Mwili wao una umbo la mstatili uliolegea, na wanaweza kuwa na gamba gumu au laini kutegemeana na spishi.
Kwa sasa, jongoo bahari ni bidhaa ya thamani kubwa kwenye soko la kimataifa, hasa katika nchi za Asia kama China, Malaysia na Korea Kusini, ambako hutumika kama chakula cha cha starehe na tiba mbadala.
Ripoti ya Shirika la Chakula Duniani (FAO) ya mwaka 2023 inaonyesha kuwa soko la kimataifa la viumbe hao linazidi kukua, na kilo moja ya jongoo waliokaushwa inaweza kuuzwa hadi Dola 600 za Marekani (takriban Sh1.5 milioni) kwenye masoko ya Asia.
Licha ya ladha yake kufanana na pweza, matumizi ya jongoo hawa katika familia za kawaida hapa nchini bado ni machache.
Lyatuu anaeleza kuwa wengi hawajui kama wanaliwa, wala hawajapata elimu ya namna ya kuwapika. “Unawaosha, unawachemsha mara mbili, kisha unaweza kuwakaanga au kuwatengenezea supu.

Kwa wenyeji wa pwani, wanalinganishwa sana na pweza kwa ugumu wa mwili,” anabainisha.
Mbali na kutumika kama kitoweo, ufugaji wa jongoo hawa umeanza kutazamwa kama chanzo kipya cha ajira kwa vijana, hasa waliomaliza vyuo vya uvuvi au wale waliopo mtaani bila ajira rasmi.
“Soko lake liko tayari, changamoto ni elimu na mtaji wa kuanzia,” anasema Lyatuu.
Kwa sasa, ufugaji wa jongoo hawa upo kwenye hatua za majaribio katika maeneo ya pwani, huku taasisi kama FETA zikitumia fursa ya maonesho kama haya kutoa elimu ya moja kwa moja kwa wananchi kuhusu fursa mpya za kiuchumi zilizopo baharini.
Swali linalobaki kwa wengi ni kama ungeweza kulipa Sh120,000 kwa kilo moja ya kiumbe mdogo wa baharini ili kufurahia ladha ya supu yake.