Mfahamu ‘Seabright’ kuku anayeuzwa Sh 500,000

August 12, 2024 4:37 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Hutumika zaidi kwa mapambo na chakula.
  • Bei yake kwa pea hufikia Sh milioni moja.

Arusha. Kwa mbali ukiwaona unaweza kusema ni aina ya ndege au njiwa, lakini sauti ya kuwika kwa majogoo itakufanya ugundue kuwa unachokiona ni aina fulani ya kuku.

Wana manyoya ya rangi nyeusi na nyeupe yaliyofunika miili yao, macho angavu na mwendo wa madaha unaowafanya kuwa kivutio kikubwa katika maonesho ya kilimo maarufu kama Nanenane kwa kanda ya kaskazini yaliyofanyika katika uwanja wa Themi-Njiro jijini Arusha.

Hao ni kuku aina ya ‘Seabright’ waliolifanya banda la Honest Kitomary muuzaji wa kuku hao kuzungukwa na watu wengi hivyo kumfanya kutumia muda mwingi kujibu maswali ya mara kwa mara anayoulizwa na watembeleaji wa banda hilo.

Hawa kuku mbona wadogo hivi?, Mnawauza shilingi ngapi?, Wana umri gani, Hapo walipo wanataga?, mayai yake mnauzaje?,” ni miongoni mwa maswali ya mfululizo aliyokuwa akiulizwa Kitomary.

Umbo dogo sifa ‘kedekede’

‘Seabright’ ndiyo jina walilopewa kuku hawa wenye asili ya Uturuki wanaotumika zaidi kwa ajili ya urembo na mapambo huku baadhi watu wakiwatumia kwa biashara na wengine kwa ajili ya chakula.

Kwa mujibu wa tovuti ya ‘Livestock conservancy’ ya masuala ya mifugo kuku hao wana urefu wa sentimita 33 na uzito wa kuanzia gramu 500 kwa mtetea (kuku anayetaga) na majogoo hufikia hadi gramu 600 huku wakiwa na uwezo wa kutaga na kuwika wakiwa na miezi saba.

Hiyo ni sawa na kusema urefu wa kuku hao ni sawa na urefu wa rula moja na zaidi huku uzito wao ukiwa nusu kilo pekee.

Seabright wanaweza kutaga mayai 60 mpaka 80 kwa mwaka yanayoweza kuongezeka au kupungua kutoka kuku mmoja hadi mwingine huku wakiwa na uwezo mdogo wa kulalia hadi kuyatotoa.

“Uwezo wao wa kulalia na kulea vifaranga ni mdogo hivyo kama unataka kutotolesha mayai itakulazimu kumpa kuku mwingine alee vifaranga,” imesema tovuti hiyo.

Bei yake imechangamka 

Kitomary ameiambia Nukta Habari kuwa licha ya umbo dogo kuku mmoja huuzwa Sh500,000 huku jogoo na mtetea kwa pamoja wakiuzwa Sh1 milioni jambo lililoshangaza watembeleaji wengi wa banda hilo.

Pamoja na bei hiyo, mfugaji huyo anasema matunzo yake yanafanana na yale ya kuku wa kawaida kuanzia chakula, maji na madawa na utofauti upo kwenye eneo la matunzo pekee.

“Hawana changamoto yoyote, wanaishi mazingira yoyote unaweza kuwafuga kwa kuwaweka bandani au kuwatoa nje ila unatakiwa uwalinde na mwewe kwa sababu ni wadogo hivyo ni rahisi kubebwa,” amesema Kitomary.

Mbali na kuku hao kutumika kwa mapambo pia ni chanzo kizuri cha kujiingizia kipato ambapo Kitomary ameeleza kuwa tangu aanze kuwafunga miaka mitano iliyopita amejipatia fedha zinazotosha kupanua biashara yao na kumudu gharama za maisha.

Kuhusu masoko Kitomary ameeleza kuwa kuku hao wanauzika zaidi kupitia maonesho kama Nanenane, Sabasaba na aina nyingine za maonesho ambayo huwasaidia kujitangaza na kupata wateja zaidi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW