Maeneo unayoweza kujivinjari msimu huu wa sikukuu
- Ni pamoja na Ndege Beach na Cocomus beach iliyopo Ununio
- Maeneo haya yanaweza kukupa utulivu na burudani katika msimu huu wa sikukuu.
Dar es Salaam. Msimu wa sikukuu na mapumziko ya mwisho ya mwaka tayari umewadia, kipindi hiki huambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo kwenda maeneo ya kujivinjari.
Suala hili si la lazima sana, ingawa baadhi ya watu kwao ili sikukuu inoge, hupendelea kutembelea maeneo mbalimbali kama fukwe, ili kutuliza akili, kujiburudisha na kutafakari.
Ikiwa  bado hujapata  mahali pa kwenda kutembelea katika sherehe za mwisho wa mwaka huu, Nukta Habari imekuandalia  maeneo unayoweza kutembelea ndani ya jiji la Dar es Salaam ukiwa peke yako, familia au marafiki bila kutoboa mfuko wako zaidi.
Soma zaidi:Fukwe tano zisizo na kiingilio unazoweza kutembelea Dar
1.Ndege Beach
Je unataka kula chakula kitamu huku ukipigwa na upepo mwanana kutoka bahari ya hindi? Vipi kuhusu kulisha wanyama kama pundamilia, swala na twiga, basi ndege Beach ndiyo mahala pake.
Hayo yote unaweza kuyapata hapa hapa pembezoni kidogo mwa jijini Dar es Salaam kilomita 10 tu kutoka kituo cha mabasi Mbweni.
Ikiwa utapendelea kulala katika fukwe hiyo basi utatumia Sh60,000 pekee itakayokuwezesha kupata kifungua kinywa chenye ladha ya kipekee.Â
2.Msitu wa Pugu  kazimzumbwi
Unaonaje kama msimu huu sikuu ukajipa mtoko wa kutembelea msitu wa Pugu Kazimzumbwi uliopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Msitu huu uliopo chini ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) umesheheni vivutio vingi hasa kama wewe ni mpenzi wa mazingira yenye uoto wa asili, kupanda milima, miti, ndege, wanyama wadogo wadogo, mito pamoja na  kupiga picha.
Kwa umbali wa kilomita 3.5 kutoka kituo cha mabasi Kisarawe utaweza kufika katika kivutio hicho kilichozungukwa na milima na mandhari nzuri ya bwawa la kuogelea ambalo pia unaweza kutumia mtumbwi kwa ajili ya kutalii zaidi.
Kuhusu usalama hilo ondoa shaka kabisa kwa kuwa kuna waangalizi maalumu wanaohakikisha michezo yote haihatarishi usalama wa wageni.
Panzi aliyepambwa kwa rangi za bendera ya Taifa nimiongonimwa vivutiomaarufu katika msitu wa Kizimzumbwi kwa jina la kitalaamu huitwa ‘Cyphocerastis Uruguruensis’.Picha|Michael Dalali/Medium.
3.Mbweni Jkt camp
Kempu hii iliyopo kilomita chache tu kutoka kituo cha mabasi Mbweni, inamilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) hivyo ukiwa hapo usalama ni asilimia 100.
 Tofauti na Kempu nyingine zenye mahema ya kulalia pekee, ukiwa hapa utafurahia mandhari nzuri iliyotulia itakayo kuwezesha kutafakari vizuri mipango yako kwa mwaka ujao.
Pia kama unapenda kuogelea hapa ndiyo penyewe, wana mabwawa ya kuogelea na kisiwa cha mchanga  kilichopo umbali wa dakika 45 kutoka eneo mahema yalipo.
Kisiwa hicho kina mandhari nzuri ya kupendeza ambayo yatakuwezesha kuona aina mbalimbali za ndege wanaopenda kutua maeneo hayo, bila kutusahau msosi mtamu wa baharini unaoweza kujipatia kwa gharama nafuu ukiwa kisiwani hapo au eneo lolote utakalo lichagua.
Ili uweze kulala katika mahema hayo utalaziika kutoa Sh120,000 kwa hema la watu wawili  kwa siku au wapendanao na kama upo mwenyewe utalipia Sh100,000 gharama inayojumuisha hadi kifungua kinywa.
Mbali na chakula kitamu, ukiwa Cocomas utafurahia vinywaji vya kishua vitakavyochangamsha mapumziko yako ya mwisho wa mwaka.Picha|Cocomas Beach/Instagram.
4.Cocomas Beac
Hii ni moja ya fukwe ya kishua yenye bajeti ndogo unayoweza kutembelea kabla mwaka 2023 haujaisha.
Fukwe hii ipo umbali wa  mita 600 kutoka kituo cha mabasi Ununio jijini hapa inasifika kwa ‘location kali’ namaanisha mazingira mazuri, tulivu na yanayovutia kwa picha nzuri na matukio ya muhimu kama sikukuu za kuzaliwa na sherehe nyingine.
Ukiwa na mpango wa kutembelea cocomas hauhitaji kubeba pesa ya kiingilio ila utahitaji kutunisha mfuko wako ili uweze kupata huduma nyingine zinazotolewa katika fukwe hiyo ikiwemo chakula na vinywaji
Kuhusu ‘vibe’ wala usijali, lipo kama lote kuanzia kwenye muziki, chakula kizuri hadi kwenye mazingira ambayo yanashawishi kuendelea kubaki maeneo hayo.