Ukweli kuhusu supu ya pweza kuongeza nguvu za kiume

December 10, 2024 9:04 am · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataalamu wa afya wasema kula pweza pekee hakutoshi kuwapa walaji uhakika wa nguvu za kiume.
  • Sababu za upungufu wa nguvu za kiume zatajwa.

Dar es Salaam. Ni kawaida kukuta makundi ya watu yakiwa yamezunguka vibanda vya wauza supu na nyama ya pweza pamoja na aina nyingine za samaki katika maeneo mengi jijini Dar es Salaam hususan muda wa jioni.

Kwa wakati huu si vijana wala watu wazima utakaoweza kuwatoa kwenye msururu wa kununua supu ya pweza ambayo kwa miongo mingi imekuwa ikihusishwa na kuongeza nguvu za kiume.

Miongoni wa watu hao yupo James Haule mkazi wa Mji Mpya, Dar es Salaam ambaye anakiri kutumia Sh1,000 kununua supu ya pweza kila akitoka kazini mida ya jioni.

“Napotoka kazini mara nyingi lazima nipitie kupiga supu ya buku (1,000) kwa sababu inaniongezea nguvu ninazotaka kitandani.” amesema Haule.

Ukweli ni upi?

Mkurugenzi Idara ya Elimu ya Lishe na Mafunzo wa Taasisi ya Chakula na Lishe, Dk Esther Nkuba ameeleza kuwa matumizi ya pweza huupa mwili asidi ya D-aspartic inayoweza kuongeza viwango vya ‘testosterone’ kwa wanaume kwa asilimia 42. 

Dk Nkuba amesema kuwa “Pweza ana vitamini na madini mengi muhimu, ambayo hutoa zaidi ya asilimia 20 ya mahitaji ya mwili kila siku ya chuma, zinki, selenium na vitamini B12. Pia ni chanzo cha kalsiamu, fosforasi, potasiamu, na magnesiamu…

…Virutubishi vilivyomo kwenye gramu 100 ya pweza, ni kalori  163, mafuta gramu 2, sodiamu miligramu 711, wanga gramu 4, protini gramu 30, ‘cholesterol’ miligramu 95, kalsiamu miligramu 106, madini chuma miligramu 9.48, zinki miligramu 3.34, ‘Selenium’ miligramu 89, na Vitamin B12 miligramu35.8,”

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, kula pweza pekee hakutoshi kuwapa walaji uhakika wa nguvu za kiume bali ili mwili ufanye kazi vizuri unahitaji virutubishi zaidi ya 50 kwa siku kwa shughuli za kimetaboliki za seli, stamina, na kudhibiti viwango vya homoni ya testosterone inayohusika kuzalisha wa mbegu za kiume na kuchochea hamu ya tendo la ndoa.

“Kitaalamu tunashauri mtu ale vyakula mchanganyiko kutoka makundi yote sita ya chakula ambayo ni nafaka, mizizi yenye wanga na ndizi mbichi, mbogamboga, matunda, vyakula vya jamii ya mikunde, jamii ya Karanga na mbegu za mafuta, vyakula vya asili ya wanyama, na mafuta yatokanayo na mimea.” amesema Dk Nkuba.

Pweza ni aina ya samaki aliye katika kundi la vyakula asili ya nyama, hivyo kwa mtumiaji kupata matokeo anayotarajia ni lazima kuliwa pamoja na vyakula vingine ili kupata virutubisho vyote muhimu.

Nyama na supu ya pweza iliyoandaliwa tayari kwa kutumiwa na walaji. |Picha Mr Health

Dk Nkuba ameongeza kuwa kutoa elimu juu ya madhara yanayoweza kusababishwa na ulaji wa pweza kwa kiwango kikubwa kwa muda mrefu kutokana na samaki huyo kuwa na kiwango kikubwa cha madini ya sodiamu.

“Kila kitu hakitakiwi kuzidishwa, pweza ana sodiamu nyingi ambayo ni muhimu kwenye afya ya mfumo wa neva, lakini inaweza kuchangia matatizo ya moyo wakati anapotumiwa kwa wingi kwa hiyo hakikisha umeila kwa kiasi,” amebainisha Dk Nkuba.

Sababu za upungufu wa nguvu za kiumwe zatajwa

Daktari Godlisten Shayo kutoka Hospitali ya Arafa iliyopo jijini Dar es Salaam ameiambia Nukta Habari kuwa neno ‘nguvu za kiume’ hutumika kuelezea uwezo wa mwanaume kushiriki katika tendo la ndoa na kupata watoto.

“Kwa ujumla, linahusiana na mambo kama vile uwezo wa kusimamisha uume, kuendelea kuwa na msisimko wa kingono kwa muda mrefu, na uwezo wa kutoa mbegu za kiume zenye afya.” amesema Dk Shayo.

Kwa mujibu wa daktari huyo, upungufu wa nguvu za kiume unasababishwa na hali duni ya kiuchumi inayopelekea mwanaume kushindwa kumudu mahitaji ya kifamilia, matatizo ya afya ya akili na kimwili.

“Mfano umeamka asubuhi huna hata 10 (Sh10,000) mfukoni alafu watoto wanataka hela kwenda shule, utapata nguvu za kiume wapi? Uchumi ukiwa chini inaathiri sana…na vilevile mapenzi sio ya kufanya kila siku unachoka” amesema Dk Shayo.

Utafiti wa Shirika la Afya Dunianii (WHO) umebainisha kuwa upungufu wa nguvu za kiume ni tatizo la kiafya linaloathiri takriban asilimia 15 ya wanaume kila mwaka, ifikapo 2025 wanaume milioni 320 wanakadiriwa kuwa wataathiriwa na tatizo hilo ulimwenguni kote.

Enable Notifications OK No thanks