Wadau wahimiza uwekezaji, uendelezaji nishati jadidifu Tanzania

January 16, 2019 7:14 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wamesema nishati hiyo ni ya uhakika, endelevu na inaweza kutumiwa na vizazi vijavyo bila kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
  • Pia inasaidia kupunguza gharama na kukatika kwa umeme katika maeneo muhimu ya uzalishaji.
  • Serikali kukaa meza moja na sekta binafsi kuangalia namna ya kuondoa changamoto za nishati.

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kuendelea na utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge, wadau wa nishati wameshauri juhudi zaidi zielekezwe katika uendelezaji wa nishati jadidifu ili kuwahakikishia watanzania upatikanaji wa umeme. 

Mradi wa Stiegler’s Gorge utakaozalisha Megawati 2,100 unatarajiwa kujengwa katika Pori la Akiba la Selous, umekuwa ukipingwa na watetezi wa mazingira kwa madai kuwa siyo rafiki kwa viumbe hai waliopo katika pori hilo. 

Wakati akishuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa mradi huo Desemba 12, 2018, Rais John Magufuli alisema gharama za uzalishaji umeme wa maji ni ndogo kuliko vyanzo vingine na kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza tatizo la umeme nchini. 

Hata hivyo wadau wa nishati nchini wamesema licha ya ukweli kuwa gharama za uzalishaji wa umeme wa maji ni ndogo lakini athari zake kwa mazingira na jamii huenda zikawa kubwa.

Katibu Mtendaji wa Chama cha Wadau wa Nishati Jadidifu (TAREA), Mhandisi Mathew Matimbwi amesema Taifa halitaweza kukwepa gharama za mradi huo kwasababu maendeleo yoyote yanaambatana na athari fulani.

Athari hizo ni pamoja na ukataji wa miti na uharibu wa mimea na viumbe kama wanyama wanaopatikana katika eneo hilo ambalo linapokea maji yake kutoka mto Rufiji.

“Hatuwezi kusema haufai madhara yatakuwepo lakini tumesema hiyo ni gharama ya maendeleo,” amesema Matimbwi. 


Zinazohusiana: 


Kutokana na hali hiyo amesema ni vema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi waangalie namna ya kuongeza uwekezaji katika vyanzo vingine vya nishati jadidifu kwasababu ni vya uhakika, endelevu na rafiki wa mazingira. 

                         

Amesema ikiwa nishati jadidifu inayojumuisha vyanzo kama jua, upepo, jotoardhi, takataka za mimea zitaendelezwa zitasaidia kupunguza gharama na kukatika kwa umeme katika maeneo mbalimbali nchini. 

Lakini ni njia rahisi ya kuyafikia maeneo yasiyofikiwa na gridi ya Taifa ya umeme inayosambazwa na Tanesco. 

“Gharama za umeme zinaweza kupunguzwa ikiwa tutageukia nishati jadidifu,” amesema Matimbwi aliyekuwa akizungumza kuhusu sera na sheria zinazosimamia maendeleo ya nishati jadidifu katika mafunzo maalum ya wanahabari ya nishati yanayofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku nne.

Umeme wa maji ni miongoni mwa nishati jadidifu lakini inaathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa hasa upungufu wa mvua na ukame.

Amebainisha kuwa uwekezaji wa nishati jadidifu utafanikiwa ikiwa sera na sheria zilizopo zitatekelezwa kikamilifu kwa kuimarisha mawasiliano na ushirikiano wa wadau wote ikiwemo sekta binafsi iliyojikita kufikisha nishati mbadala kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na Serikali. 

Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 inayosisitizwa kuendelezwa kwa nishati jadidifu ili kuongeza uchangiaji wa umeme katika gridi ya Taifa ya umeme.

Washiriki wa Mafunzo Maalum ya Wanahabari ya Nishati wakifuatilia mada ya sera zinazosimamia nishati Tanzania kutoka kwa Mhandisi Mathew Matimbwi ambaye hayupo pichani. Picha| Zahara Tunda.

Meneja Masoko wa kampuni ya Mobisoli Tanzania inayotoa huduma ya umemejua, Seth Mathemu ameiambia www.nukta.co.tz kuwa wanakabiliwa na changamoto ya umbali wa vijiji na usafiri jambo linaloongeza gharama za uendeshaji kampuni kutokana na umbali na muda unaotumika kufikisha huduma kwa vijijini.

“Ukubwa wa nchi na umbali wa nyumba moja hadi nyingine ni changamoto katika vijiji huongeza gharama za muda na usafiri kuwafikia wateja wetu,” amesema Mathemu ambaye ni mdau wa nishati jadidifu.

Mathemu amebainisha kuwa utofauti wa kodi za matangazo (branding fees) kutoka eneo moja hadi lingine, nayo ni sababu ya sekta ya nishati jadidifu kutokukua kwa kiwango kinachostahili licha ya Serikali kuondoa kodi kwenye vifaa vya sola vinavyoingia nchini. 

Hata hivyo, wadau hao wamesisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha maeneo yote ambayo umeme wa gridi haujafika watapeleka umeme mbadala ili kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.

Enable Notifications OK No thanks