Weledi, takwimu sekta ya nishati kuwatoa Wanahabari Tanzania

January 16, 2019 7:12 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Watakiwa kuzingatia weledi na matumizi sahihi ya takwimu katika kuripoti habari za nishati jadidifu ili kuleta matokeo chanya kwenye jamii.
  • Matumizi ya teknolojia kuwafungulia fursa zaidi zilizomo katika sekta ya nishati.

Dar es Salaam. Mafunzo Maalum ya Wanahabari ya Nishati yamezinduliwa leo huku wanataaluma hao wakitakiwa kuzingatia weledi na matumizi sahihi ya takwimu katika kuripoti habari za nishati jadidifu ili kuleta matokeo chanya kwenye jamii. 

Mafunzo hayo ya siku nne yameandaliwa na shirika la Hivos East Africa kwa kushirikiana na kampuni ya teknolojia na habari ya Nukta Africa na kituo cha kijamii cha Energy Change Lab, kwa lengo la kuongeza wigo wa kuripoti habari za nishati jadidifu zitakazowasaidia wananchi hasa wa vijini kuondokana na umaskini. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen aliyezindua mafunzo hayo jijini Dar es Salaam amesema sekta ya nishati jadidifu ni fursa kwa vyombo vya habari kwasababu inafungua milango ya kupata mapato na kuwaendeleza Wanahabari kitaaluma na kubobea katika kuwafikishia wananchi habari sahihi. 

Dausen ambaye alijikita kuzungumzia umuhimu wa kuhakiki habari kabla ya kuitoa (Fact Checking), amesema wakati wanahabari hao wanaripoti habari za nishati jadidifu ni muhimu watumie vyanzo vya uhakika, takwimu sahihi ili kujiepusha na habari za uongo. 

Sambamba na hilo amewataka Wanahabari kujikita katika uandishi wa habari za uchambuzi zilizofanyiwa utafiti  wa kina ili kuwa na mitazamo tofauti inayobainisha ukweli wa taarifa zinazoripotiwa. 

“Namna ya kuendelea kuwepo (katika tasnia ya habari) kwenye kipindi ambacho wananchi wanatupa habari ni kufanya analysis (uchambuzi),” amesema Dausen.


Zinazohusiana: 


Mafunzo hayo ambayo yatadumu kwa siku nne kuanzia leo (Januari 15, 2019) hadi ijumaa (Januari 18, 2019) ni muendelezo wa mafunzo ya miezi sita yaliyoanza mwishoni mwa mwaka jana ili kuwajengea uwezo Wanahabari katika kuboresha kazi zao za nishati jadidifu. 

Mratibu wa Kitaifa wa Energy Change Lab, Sisty Basil amesema ikiwa Wanahabari wataongeza wigo wa kuripoti habari za nishati jadidifu wataisadia jamii hasa wananchi waishio vijijini kuondokana na umaskini kwa kuwapunguzia gharama za matumizi ya vyanzo vya umeme kama kuni na mkaa. 

“Huwezi kuishi bila nishati, tukiripoti habari hizi (nishati jadidifu) tutawasaidia wananchi kupunguza gharama za nishati,” amesema Basil.

Amesema Tanzania ina vyanzo vingi vya nishati  lakini bado havijaendelezwa kutokana na gharama kubwa za uzalishaji umeme lakini ripoti za Wanahabari waliobobea zitasaidia kuvutia uwekezaji hasa katika nishati mbadala kama jua na maji. 

Mratibu wa Kitaifa wa Energy Change Lab, Sisty Basil amesema hakuna nchi iliyoendelea ambayo ina matumizi madogo ya nishati. Picha| Daniel Samson.

Nishati jadidifu au mbadala hujumuisha umemejua, maji na jotoardhi, umeme utokanao na upepo ambao ni rafiki kwa mazingira hasa katika kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanaathiri mwenendo wa maisha ya mwanadamu.

Katika mafunzo hayo, Meneja wa Maudhui kutoka Nukta Africa, Daniel Mwingira amewakumbusha Wanahabari walioanza safari ya kubobea katika habari za nishati kutumia teknolojia ya mtandao ili kupata marejeo na tafiti mbalimbali zitakazowasaidia kuongeza thamani za habari zao. 

Amesema programu za utafutaji marejeo mtandaoni ni rahisi kupatikana lakini kuna umuhimu wa kuthibitisha kila taarifa wanayoipata mtandaoni kabla ya kuitumia ili kujiepusha na upotoshaji.

Mafunzo hayo yamewakuatanisha Wanahabari 20 kutoka maeneo mbalimbali nchini ambapo baada ya kurudi katika maeneo yao watazalisha habari zinazokusudia kuleta mabadiliko hasa kuchochea matumizi ya nishati jadidifu.

Naye Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema nguzo kuu ya Wanahabari kufanikiwa ni kuboresha nyenzo za mawasiliano yatakayosaidia kuongeza utashi wa kuelewa mambo mtambuka yanayoendelea katika jamii.

Enable Notifications OK No thanks