Washiriki tamasha la nishati 2018 waondoka na matumaini kibao

Daniel Samson 0445Hrs   Disemba 02, 2018 Habari

Wanahabari wakiwa katika picha ya pamoja walipotembelea kituo cha umeme cha Power Corner katika kijiji cha Kitumbeine mkoani Arusha. Picha| K15.


  • Tamasha hilo limefungua mlango kwa wanahabari kujifunza na kupata maarifa, ujuzi na mbinu watakazotumia kuifikia jamii katika sekta ya nishati jadidifu.
  • Ikiwa nishati jadidifu itatumika vizuri itasaidia kuongeza wigo wa mapato katika vyombo vya habari na kuiwezesha jamii kunufaika kiuchumi.
  • Wanahabari wapewa changamoto ya kutumia data katika habari zao ili kuongeza weledi na kuamniwa na wadau wa sekta hiyo.

Arusha. Zilikuwa siku tano za wadau na wanahabari kutoka kona mbalimbali za Tanzania kukutana katika tamasha la Nishati la Wanahabari 2018 lililofanyika Usa River mkoani Arusha kujifunza na kubadilishana uzoefu katika sekta ya nishati jadidifu.

Lilianza Novemba 26 na kufikia kilele chake Novemba 30 mwaka huu halikuwa la kubahatisha bali Wanahabari waliohudhuria wameondoka na matumaini makubwa ya kubobea katika uandishi wa habari za nishati jadidifu ili kuongeza wigo wa mapato katika vyombo vya habari na kuiwezesha jamii kupata taarifa sahihi za nishati kuendeleza maisha yao.

Tamasha hilo liliandaliwa na shirika la Hivos East Africa kwa kushirikiana na kituo cha kijamii cha Energy Change Lab na kampuni ya teknolojia na habari ya Nukta Africa limited  wakiwa na lengo kutanua uelewa wa nishati jadidifu (Renewable Energy) ikiwemo matumizi ya umemejua na umemeupepo.

Baadhi ya washiriki wa tamasha hilo wameiambia Nukta kuwa habari za nishati jadidifu zimekuwa hazipewi kipaumbele kwasababu Wanahabari waliobobea katika sekta hiyo ni wachache, lakini tamasha hilo limefungua mlango wa kujifunza na kupata maarifa, ujuzi na mbinu watakazotumia kuifikia jamii.

"Nimeweza kujifunza mambo mengi kama Mwanahabari katika masuala ya nishati hasa nishati jadidifu, nimeweza kufahamu hata miongoni mwetu sisi wanahabari wengi wetu tulikuwa hatuna uelewa kuhusiana na masuala ya nishati jadidifu lakini "Energy Safari" imetubadilisha, binafsi nimekuwa mtu mwingine kabisa," amesema Vumilia Kondo kutoka Abood Media mkoa wa Morogoro.

Pia, tamasha hilo limewaongezea mwanga na weledi katika kuripoti habari za nishati jadidifu, kwasababu wamefahamu vyanzo vingine vya nishati kuliko uelewa wa awali wa chanzo kimoja cha umemejua ambacho kimekuwa kikisambazwa na makampuni mbalimbali kama Mobisol Tanzania, Ensol Limited na Power Corner Limited.

Mtangazaji na Muundaji wa vipindi kutoka  Radio CG FM ya mkoani Tabora, Vivian Pyuza amesema tamasha hilo limetumika kama jukwaa la kuwaunganisha na kuimarisha ushirikiano kwa wanahabari katika kutimiza majukumu ya kuhabarisha umma.

                      ;

Kwa upande wake, Mwanahabari wa gazeti la Jamhuri mkoani Ruvuma, Andrew Kuchonjoma amesema nishati jadidifu ikutumika vizuri inaweza kuleta maendeleo kwa makundi yote yaliyopo katika jamii endapo wananchi wa vijijini watapelekewa taarifa sahihi za nishati. 

Hata hivyo, wanahabari wamesisitiziwa kutumia takwimu na data katika kubaini changamoto zilizopo katika jamii hasa za watu wasiofikiwa na umeme katika maeneo yao.

"Nimejifunza kitu kingine kuwa uandishi wetu wa sasa ujikite zaidi kwenye data kuliko kuandika tu kama tunataka kukimbia, ili wale wadau au vyombo husika viweze kushughulikia tatizo tunaloliibua kwa lengo la kuleta maendeleo ya nchi kwa wananchi na waandishi wenyewe  kiujumla," Amesema Kuchonjoma.


Zinazohusiana:


Tamasha la Nishati 2018 lilipewa jina la "Energy Safari" liliwakutanisha zaidi ya wanahabari 15 kutoka maeneo mbalimbali nchini ambapo lilihusisha shughuli mbalimbali ikiwemo kutembelea kijiji cha Kitumbeine wilayani Longido ambacho kimeunganishwa na umeme mdogo wa gridi ya Taifa unaozalishwa kwa kutumia paneli za sola. 

Pia washiriki walikutana na kufanya mazungumzo na wadau wa nishati likiwemo shirika la umeme (Tanesco) mkoa wa Arusha, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), vyombo vya habari na wananchi. Yote ni katika kuunganisha nguvu ya kuendeleza nishati jadidifu katika jamii.

Hitimisho la Tamasha hilo ni mwanzo wa kuanza kwa mafunzo maalum ya wanahabari yanayoanza Disemba mwaka huu kujifunza zaidi jinsi ya kuripoti kwa weledi masuala ya nishati jadidifu.

Related Post